October 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Magufuli azindua kiwanda cha bidhaa za ngozi mkoani Kilimanjaro

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Kilimanjaro

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akifatilia hotuba mbalimbali kabla ya kuzindua Kiwanda hicho cha Ngozi cha Kilimanjaro International leather Industries Co Ltd kilichojengwa kwenye eneo la Gereza Kuu la Karanga mkoani Kilimanjaro leo

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amezindua kiwanda cha bidhaa za ngozi cha Kilimanjaro (Kilimanjaro International Leather Industries Co. Ltd) kilichojengwa katika eneo la Gereza Kuu la Karanga, Moshi Mkoani Kilimanjaro kwa ubia wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (PSSSF) na Jeshi la Magereza Tanzania.

Mradi wa ujenzi wa kiwanda hicho umehusisha uboreshaji wa kiwanda cha zamani kilichojengwa na Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mwaka 1978 kwa ajili ya kuzalisha viatu vya kijeshi ambapo kilikuwa kikizalisha jozi 150 kwa siku, na sasa kimeboreshwa na kuongeza uzalishaji hadi kufikia viatu 400 kwa siku.

Kiwanda kipya na cha teknolojia ya kisasa kilichowekezwa hivi sasa na ambacho kimeanza uzalishaji kina uwezo wa kuzalisha jozi milioni 1.2 za viatu kwa mwaka, soli za viatu jozi milioni 2.1 kwa mwaka pamoja na bidhaa mbalimbali za ngozi kama vile mikanda, mabegi, pochi na makoti, na pia kitakuwa na uwezo wa kuchakata futi Milioni 13 za ngozi ambazo kwa asilimia 60 zitatumika kiwandani hapo na asilimia 40 kuuzwa ndani na nje ya nchi.

Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Hosea Kashimba amesema uwekezaji wa kiwanda hicho umegharimu shilingi Bilioni 136, kinatarajiwa kutoa ajira takribani 3,000 za moja kwa na 7,000 zisizo za moja kwa moja, na kwamba katika kujihakikishia upatikanaji wa malighafi za uhakika PSSSF inashirikiana na wadau wengine kuwekeza katika machinjio ya kisasa nchini ili kupata ngozi bora za kukilisha kiwanda hicho.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na wananchi kabla ya kuzindua Kiwanda cha Bidhaa za Ngozi cha Kilimanjaro International leather Industries Co Ltd kilichojengwa kwenye eneo la Gereza Kuu la Karanga Moshi mkoani Kilimanjaro leo

Baada ya kuzindua kiwanda hicho, Rais Magufuli amejionea jinsi vijana wa Kitanzania wanavyofanya kazi kwa kutumia mitambo ya kisasa ya kutengeneza viatu bora vya aina mbalimbali na pia amenunua jozi kadhaa za viatu vilivyokuwa tayari kwa kuuzwa.

Akizungumza na wananchi waliohudhuria tukio hilo jana, Rais Magufuli ameelezea kufurahishwa kwake na kukamilika kwa kiwanda hicho ambacho kimeboreshwa na kuwekezwa mitambo na majengo mapya kwa maelekezo yake, na amesema anaamini uzalishaji wake utaendelea kupanuliwa ili kupunguza matumizi makubwa ya fedha za kigeni zinazotumika kuagiza viatu nje ya nchi ambapo takwimu zinaonesha Tanzania inaagiza jozi Milioni 52 za viatu kwa mwaka.

Rais Magufuli amesema, pamoja na ajira za moja kwa moja zitakazozalishwa na kiwanda hicho, ajira nyingine takribani Milioni 3 zitazalishwa kutokana na mnyororo wa thamani, soko la ngozi litapanuliwa na hivyo ametoa wito kwa wafugaji kuzalisha ngozi bora.

Ameipongeza PSSSF yenye asilimia 86 ya hisa za kiwanda hicho na Jeshi la Magereza kwa kufanikisha uwekezaji huo, na ametoa wito kwa mifuko ya hifadhi ya jamii na wadau wengine kuendelea kuwekeza katika viwanda kama ambavyo wamefanya katika miaka mitano iliyopita ambapo Tanzania imefanikiwa kujenga viwanda vipya 8,470.

Rais Magufuli amewataka Watanzania wote kuendelea kudumisha amani ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya viwanda, hasa wakati huu ambapo Tanzania imeingia katika uchumi wa kati, na amesisitiza kuwa Serikali itahakikisha inaendelea kujenga mazingira bora ya uwekezaji ili Watanzania wanufaike.

Sherehe ya uzinduzi wa kiwanda hicho imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu)   Jenister Mhagama, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi   George Simbachawene, Kamishna Jenerali wa Magereza Suleiman Mzee, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Anna Mghwira, viongozi wa Dini, viongozi na watendaji wakuu wa mifuko ya hifadhi ya jamii.