Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dodoma
RAIS John Magufuli amewashukuru Viongozi wa Dini na Watanzania wote kwa kuitikia wito wa kumuomba Mwenyezi Mungu aepushe janga la ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na virusi vya Corona (Covid-19).
Rais Magufuli ametoa shukrani hizo jana alipokaribishwa kuwasalimu waumini wa Kanisa Katoliki, Parokia ya Bikira Maria Imakulata, Chamwino Mkoani Dodoma baada ya kuhudhuria Misa Takatifu ya Sikukuu ya Utatu Mtakatifu iliyoongozwa na Paroko wa Parokia hiyo, Padre Paulo Mapalala.
Rais Magufuli amesema Mwenyezi Mungu amejibu maombi ya Watanzania ambao wamesali, wamefanya toba na kufunga, na matokeo yake ni kuwa maambukizi ya virusi vya Corona yamepungua na wananchi wanaendelea na maisha yao huku wakichapa kazi za uzalishaji mali, tofauti na ilivyodhaniwa kuwa ugonjwa huo ungesababisha madhara makubwa.
Ametoa wito kwa Watanzania wote kuendelea kuwa makini dhidi ya mbinu zozote zinazoweza kufanywa kuwaambukiza ugonjwa huo ama magonjwa mengine, huku wakimshukuru na kumtumaini Mwenyezi Mungu aliye muweza wa yote.
Akiwa Kanisani hapo, Rais Magufuli ameendesha harambee ya kuchangia upanuzi wa Kanisa hilo na kufanikiwa kuchangisha shilingi 17,229,000/- (ikiwemo shilingi Milioni 10 aliyochangia yeye mwenyewe) na mifuko 76 ya saruji, na ametaka upanuzi wa Kanisa hilo uanze kesho.
More Stories
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili
ACT-Wazalendo,waitaka Polisi kutobeba chama kimoja