January 24, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Magufuli awapongeza wasanii kumpa kura za kishindo

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli, amewapongeza Wasanii wa fani mbalimbali hapa nchini kwa kushiriki vyema kwenye Kampeni yake ya Uchaguzi, kugombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kufanikiwa kupata kura kwa kishindo.

Akitoa pongezi hizo leo, kwenye Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma katika sherehe za kuapishwa kwa ajili ya kuliongoza Taifa la Tanzania kwa kipindi cha miaka mitano mingine, Dkt. Magufuli amesema Wasanii walikuwa kivutio kikubwa kwenye Kampeni zake jambo lililochangia kupata kura nyingi.

Rais Magufuli amesema, katika kampeni zake Wasanii walikuwa mstari wa mbele kwa kuhamasisha wananchi Tanzania nzima kuhakikisha Chama Cha mapinduzi (CCM), kinashinda kwa kishindo na kuongoza kwa miaka mitano mingine.

“Sina budi kuwapongeza Wasanii wa Tanzania kwa jitihada kubwa walizozifanya katika kipindi cha Kampeni, hivyo nitahakikisha nasimamia vyema maslahi yao ili wafanye sanaa huku wakiwa na kipato cha kutosha,” amesema Dkt. Magufuli.