Na Esther Macha, Timesmajira online Mbeya
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli ameamuru Wakala wa Barabara (Tanroads) kuachana na mpango wake wa kutwaa eneo la wananchi katika Kijiji cha Isyonje, Wilayani Rungwe kwa ajili ya kujenga mizani ya kupima uzito wa magari kwenye Barabara Kuu ya Tanzania na Malawi.
Dkt. Magufuli alitoa agizo hilo alipopigiwa simu na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila na kuzungumza moja kwa moja na wananchi wa Kijiji cha Isyoje waliokuwa wamekusanyika kwenye mkutano wa hadhara.
Akizungumza na wananchi kwa njia ya simu akiwa Ikulu ya Chamwino, mkoani Dodoma, Rais Magufuli amesema, amesikia kilio chao baada ya kuona kwenye televisheni wakilalamika kuhusu Tanroads kuchukua ardhi yao bila kuwalipa fidia.
Amesema, Sheria ya Ardhi namba tatu na namba nne ya mwaka 1999 inaamuru kulipa fidia kabla ya kuchukua ardhi ya wananchi, lakini Tanroads hawakuizingatia na badala yake walichukua ardhi ya wananchi kwa zaidi ya miaka mitatu sasa bila kulipa fidia jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
“Naamuru Tanroads kuachana na eneo hilo na badala yake wananchi waendelee na shughuli zao za kiuchumi, kama ni nyumba wajenge na kama ni mizani itajengwa sehemu nyingine sio hapo,” amesema Rais Magufuli.
Pia aliwaomba radhi wananchi hao kwa watendaji wake kuwacheleweshea maendeleo kutoka na kitendo hicho cha kuwazuia kuendeleza maeneo yao bila kuwalipa fidia kwa kipindi cha miaka mitatu.
Mkuu wa Mkoa huo, Albert Chalamila amesema, Rais Magufuli anawapenda na hapendi wananchi wanyonge waonewe na ndio sababu baada ya kusikia kilio chao alimpigia simu na kumuamuru afike kijijini hapo kuwarejeshea eneo lao ambalo lilikuwa limechukuliwa na Tanroads.
Amesema, baada ya uamuzi wa Rais, hakuna mtu yoyote anakayewasumbua na kuwataka kuendelee na shughuli zao bila wasiwasi.
More Stories
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa
NLD kipo tayari kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa