July 8, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika Ibada ya Ijumaa Kuu iliyofanyika katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Yohana-Maria Mzeyi Parokia ya Mlimani Chato mkoani Geita leo tarehe 10/04/2020.(Ikulu)

Rais Magufuli ashiriki Ibada ya Ijumaa Kuu Chato

Na Mwandishi Wetu,

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 10 Aprili, 2020 ameungana na Waumini wa Kanisa Katoliki katika Parokia ya Mlimani, Wilaya ya Chato Mkoani Geita kusali Ibada ya Ijumaa Kuu iliyoongozwa na Padre Prof. Innocent Sanga kutoka Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya.

Ibada ya Ijumaa Kuu huadhimishwa ikiwa ni kumbukumbu ya kusulubiwa na kufa kwa Bwana Yesu Kristo, zaidi ya miaka 2,000 iliyopita.

Katika salamu zake, Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Padre Sanga kwa mahubiri yaliyowakumbusha Wakristo kuwa msalaba unaokoa, na kwamba kupitia msalaba Mungu ataikoa dunia dhidi ya majanga mbalimbali ukiwemo ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na virusi vya Corona (Covid-19).

Mhe. Rais Magufuli amesema mpaka sasa idadi ya Watanzania waliothibitika kuwa na virusi vya Corona ni takribani 29, Watanzania 5 waliopatwa na maambukizi wamepona, Watanzania 3 wamefariki dunia na kwa takribani asilimia 90 ya waliopatwa na virusi hivyo wanaendelea vizuri.

Amebainisha kuwa kutokana na madhara ya ugonjwa huo duniani, upo uwezekano wa kutokea upungufu wa chakula, hivyo ametoa wito kwa Watanzania kuzalisha chakula cha kutosha na pia amewataka Watanzania kuendelea kuchapa kazi kila mahali walipo huku wakichukua tahadhari za kutoambukizwa kama wanavyoelekezwa na wataalamu.

Mhe. Rais Magufuli amesisitiza kuwa Serikali imeamua kutowazuia watu ndani ya nyumba zao wala kufunga mipaka kwa kutambua madhara makubwa yanayoweza kujitokeza kutokana na kufanya hivyo ndani ya nchi na kwa nchi 8 ambazo zinategemea kupata huduma na bidhaa kupitia Tanzania hususani Bandari ya Dar es Salaam.

Amewataka Watanzania wote kuendelea kumuomba Mwenyezi Mungu ili aiepushe dunia na janga la ugonjwa wa Corona.