November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais magufuli anavyopania uwekezaji wenye tija

Na Grace Semfuko- MAELEZO

JITIHADA za dhati za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli za kutaka Tanzania kusonga mbele kimaendeleo zinaonesha mafanikio makubwa kutokana na kile alichokisimamia tangu mwanzo wa uongozi wake alipoingia tu madarakani Novemba 5 mwaka 2015,ambapo aliweza kusimamia na kuhakikisha mianya ya ufujaji wa mali za Taifa inazibwa.

Jitihada hizo zimewezesha uanzishwaji wa miradi mbalimbali ya kijamii ikiwepo ujenzi wa miundombinu ya barabara,uboreshaji wa sekta ya elimu ikiwepo utoaji wa elimu bila malipo,ujenzi wa madarasa na miundombinu mingine huku sekta za afya, maji na maendeleo mengine ya kijamii kutoachwa nyuma.

Rais Magufuli mara nyingi anasisitiza kuwepo kwa uwekezaji wenye tija katika sekta zote,na tumeona jinsi ambavyo Serikali yake inavyosimamia na kuweka sera rafiki kwa wawekezaji ambao ndio chachu ya kuimarisha uchumi wa Taifa.

Sera na Sheria nyingi za Uwekezaji zimeimarishwa na hivyo kuwafanya wawekezaji kuwa na mazingira rafiki katika uwekezaji wao ambapo aliweza pia kuanzisha Wizara maalum itakayoshughulikia uwekezaji tu ambayo imefanikisha kuongeza uwekezaji.

Ni dhahiri,Tanzania kama zilivyo nchi nyingine duniani inahitaji uchumi wa viwanda ili kuleta mageuzi ya haraka na kujenga msingi imara wa uchumi.

Uamuzi wa Serikali wa kujenga uchumi wa viwanda unalenga kuleta maendeleo jumuishi na endelevu kwa kutumia ipasavyo rasilimali zilizopo na hivyo kuchangia katika kukuza Pato la Taifa, kutoa nafasi nyingi na endelevu za ajira, kuzalisha na kukuza teknolojia zinazohitajika na kuwa chachu ya maendeleo ya sekta zinazohusiana na kuzalisha bidhaa bora kwa ajili ya masoko ya ndani na nje ya nchi.

Ujenzi wa uchumi wa viwanda unahitaji umadhubuti na nguvu za ziada katika kusimamia na kutekeleza kwa vitendo uvutiaji wa wawekezaji, ujenzi wa viwanda,kulea na kulinda viwanda vya ndani na pia kupambana na nguvu za ushindani katika soko.

Kwa hiyo Serikali inayo kila sababu ya kuendelea kuweka mazingira wezeshi ili kila Mtanzania kwa nafasi yake awe na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika kuzalisha bidhaa kwa kuzingatia matakwa ya soko, kuwa tayari kuwekeza na pia kutoa kipaumbele katika kutumia bidhaa zinazozalishwa nchini.

Maendeleo ya sekta binafsi na uwekezaji ndio msingi wa mipango mikuu ya maendeleo ya nchi yetu.Sera,mipango na mikakati mbalimbali ambayo Serikali imekuwa inaandaa,kuboresha na kutekeleza siku zote ina lengo la kuweka mazingira wezeshi ili sekta binafsi iendelee kuwa mhimili wa uchumi na kuchangia ipasavyo katika maendeleo ya viwanda.

Serikali imeendelea na jitihada za kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi kuchangia ipasavyo katika uwekezaji nchini, kutokana na jitihada hizo,sekta ya uwekezaji imeendelea kukua ikilinganishwa na nchi nyingi za Afrika Mashariki kwani ripoti mbalimbali za uwekezaji duniani zinaonesha Tanzania imeongoza kwa kuvutia uwekezaji.

Kwa mfano,Ripoti ya Uwekezaji ya Dunia (World Investment Report) ya mwaka 2016 inayotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na Maendeleo (UNCTAD) ilionesha kuwa Tanzania imevutia uwekezaji wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 1,532 mwaka 2015, ikifuatiwa na Kenya Dola za Kimarekani 1,437 na Uganda Dola za Kimarekani 1,057.

Vilevile,ripoti ya Shirika la Quantum Global inayotafiti hali ya uwekezaji katika nchi 54 za Afrika iliiweka Tanzania katika namba nane kutoka nafasi ya 19 mwaka 2015, ikiwa ni nchi pekee katika Afrika Mashariki kuwa katika nafasi kumi za juu.

Ripoti hiyo inaangalia vigezo sita vikiwemo ukuaji wa uchumi, mzunguko wa fedha, ubadilishaji wa fedha, mazingira ya biashara, wingi wa watu na matumizi ya teknolojia na ubunifu.

April 8, 2019 Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa wakati akiwasilisha taarifa ya mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha katika ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2019/2020 alisema Tanzania inaongoza kwa uwekezaji katika Afrika Mashariki na imeweza kuvutia uwekezaji wenye thamani ya dola za Marekani bilioni 1.18, ikifuatiwa na Uganda dola za Marekani bilioni 0.7 na Kenya dola za Marekani bilioni 0.67.

“Kutokana na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali kuvutia uwekezaji nchini, hali ya uwekezaji imeimarika ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika Mashariki. Ripoti mbalimbali za uwekezaji duniani zinaonesha kuwa Tanzania imeongoza kwa kuvutia uwekezaji miongoni mwa nchi za Afrika Mashariki,” anasema.

Anasema Taarifa ya Uwekezaji ya Dunia (World Investment Report) ya mwaka 2018 inayotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na Maendeleo (UNCTAD) ilibainisha kiasi hicho kikubwa cha uwekezaji.

“Taarifa nyingine ya“The Africa Investment Index (AII) 2018” inaonesha kuwa Tanzania imeshika nafasi ya 13 kati ya nchi 54 za Afrika katika kutoa fursa za masoko na vivutio vya uwekezaji.” anasema.

Vilevile,Waziri Mkuu anasema kuwa taarifa ya “Where to Invest in Africa” ya mwaka 2018, nayo imeonesha kuwa Tanzania imeshika nafasi ya saba kati ya nchi 52 zinazovutia zaidi kwa uwekezaji barani Afrika.

Kutokana na uwekezaji huo mkubwa, ambapo aliwataka Watanzania wachangamkie fursa zinazojitokeza kutokana na ukuaji wa uchumi, maendeleo ya kijamii na pia uwekezaji wa sekta ya umma kwenye miundombinu kwa kuthubutu kuwekeza kwenye uzalishaji wa bidhaa na utoaji wa huduma.

Katika hotuba yake ya Novemba 13 wakati akizindua Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Rais Magufuli alionesha nia ya dhati ya kuhakikisha uwekezaji unasimama na kuamua kukihamishia Kituo cha Uwekezaji Tanzania-TIC katika Ofisi yake ili aweze kusimamia suala zima la uwekezaji yeye mwenyewe.

TIC awali ilikua chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara ambapo Rais Magufuli alikihamishia kituo hicho katika Ofisi ya Waziri Mkuu na kuunda Wizara ya Uwekezaji mahsusi kwa ajili ya kusimamia suala hilo ambapo January 8, 2019 Rais alimteua Angellah Kairuki kusimamia Wizara hiyo na sasa ameamua kukihamishia kituo hicho katika ofisi yake.

Kuhamishwa kwa TIC katika Ofisi ya Rais ni dhahiri kabisa kwamba Rais Magufuli anataka uwekezaji uwe ni wenye tija, anataka Uwekezaji uwanufaishe wananchi kwa kupata ajira, kuongeza uchumi kutokana na kodi mbalimbali pamoja na kuiweza Tanzania katika ramani ya Dunia ya uchumi kupitia uwekezaji.

Rais Magufuli anasema ili kuvutia wawekezaji kwenye sekta za viwanda Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ikiwepo kuangalia masuala ya kodi na kuondokana na vikwazo na urasimu katika sekta hiyo.

Rais anasema katika miaka mitano iliyopita kulikuwa na urasimu mkubwa uliosababisha Wawekezaji kusumbuliwa kwa kuzungushwa hali iliyosababisha wengi kukata tamaa ya kuwekeza.

“Nataka mwekezaji mwenye fedha akija apate kibali ndani ya siku 14, kwa sabau hiyo nimeamua suala la uwekezaji ikiwa ni pamoja na kituo cha Uwekezaji Tanzania-TIC kukihamisha kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu kwenda Ofisi ya Rais ili hao wanaokwamisha nikapambane nao mwenyewe” anasema rais huku akionesha msisitizo.

Lengo la Rais Magufuli la kuihamishia TIC katika ofisi yake bila shaka linaweza kushangaza watu wengi, lakini sio la ajabu hata kidogo kwa sababu masuala ya uwekezaji ni mawsuala muhimu kuchumi na yenye kuzalisha ajira nyingi kwa wananchi wa nchi husika na hivyo kuwafanya kuwa na uhakika wa kipato kwa ajili ya kuendesha maisha yao.

Pamoja na ajira pia mapato yataongezeka kupitia sekta hiyo kwani takwimu za uwekezaji za TIC katika kipindi cha January 2016 hadu Juni 2020 walisajili miradi 1,312 ya uwekezaji yenye mtaji wa thamani ya Dola za Marekani Bilioni 20 ikiwa ni takribani shilingi Trilioni 46 miradi ambayo ilitoa ajira kwa watanzania 178,101.

Katika usajili huo sekta ya usindikaji na uzalishaji wa viwanda iliongoza kwa asilimia 54 ya miradi yote na kutoa ajira kwa watanzania 67,992.

TIC ilianzishwa mwaka 1997 kwa sheria ya uwekezaji Tanzania ili kiwe Taasisi kuu ya Serikali ya kuratibu, kuhimiza, kukuza, kuwezesha na kushauri kuhusu Sera za Uwekezaji na masuala yanayohusiana na Uwekezaji nchini Tanzania.