Na Jackline Martin,Timesmajiraonline,Da
RAIS Samia Suluhu Hassan anatarajia kufanya ziara ya kikazi nchini China kuanzia leo Septemba 2 hadi 6, 2024 ameanza ziara nchini China ambapo pamoja na mambo mengine atashiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (Forum on China-Africa Cooperation-FOCAC) utakaofanyika jijini Beijing na kutafuta fedha za miradi minne.
Kupitia ziara hiyo Rais Samia atakutana na mwenyeji wake Rais wa China, Xi Jinping kwa mazungumzo yanayolenga kuimarisha uhusiano mzuri na wa kihistoria kati ya nchi hizo mbili ulioasisiwa miaka 60 iliyopita.
Marais hao wawili pamoja na Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema watashiriki na kushuhudia uwekaji saini wa Hati za Makubaliano ya Uboreshaji wa Reli ya Tazara.
Rais Samia anatarajiwa kuwasilisha miradi minne kwa Serikali ya China kwa lengo la kusaka fedha za mkopo nafuu na msaada ya utekelezaji wake.
Miradi hiyo anatarajia kuiwasilisha katika FOCAC ambao kwa miongo zaidi ya miwili sasa umekuwa ukitumiwa na wakuu wa nchi za Afrika kwa madhumuni yanayofanana na hayo.
Pamoja na mambo mengine, miongoni mwa maeneo yanayotarajiwa kupewa kipaumbele kwenye mkutano wa FOCAC ni uendelezaji wa miundombinu, kukuza uwekezaji, uendelezaji wa viwanda, kilimo cha kisasa na amani na usalama.
Pia Rais Samia anatarajia kuwa miongoni mwa wakuu wa nchi watakaohutubia ufunguzi wa mkutano wa FOCAC, akizungumza kwa niaba ya Kanda ya Afrika Mashariki.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa mwishoni mwa wiki na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, kwa wanahabari, Rais Samia ataenda China kutafuta fedha za miradi mine. \
“Tanzania inatarajia kuwasilisha miradi mbalimbali ikiwemo mipya na ile ambayo haikuweza kutelezwa kwenye mpango uliopita wa FOCAC kwa sababu mbalimbali, ili iweze kupatiwa fedha za mkopo nafuu na msaada na kutekelezwa chini ya mpango kazi wa FOCAC mwaka 2025-2027,” alisema Balozi Kombo.
Tangu kuanza kwake mwaka 2000 FOCAC imewezesha miradi mikubwa ya miundombinu barani Afrika, kama vile ujenzi wa barabara, reli, viwanja vya ndege, bandari pamoja na uwekezaji katika nishati.
Ushirikiano chini ya FOCAC umeongeza biashara kati ya Afrika na China huku nchi za Afrika zikipata soko kubwa kwa bidhaa zao za kilimo, madini na malighafi nyingine, na kunufaika na uagizaji wa bidhaa za bei nafuu kutoka China.
Miradi minne itakayowasilishwa na Rais Samia kwenye mkutano huo ni ujenzi wa mtandao wa mawasiliano vijijini awamu ya pili, ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa kilovoti 400 awamu ya pili na ya tatu, ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi (Veta) awamu ya pili na ujenzi wa barabara za Zanzibar zenye urefu wa kilomita 277.
Balozi Kombo alitaja malengo matatu ya Tanzania kushiriki mkutano huo; mosi ni kuendelea kudumisha ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na China ambao mwaka huu umetimiza miaka 60.
Jambo la pili ni kujadiliana na kukubaliana na Serikali ya China namna ya kuendelea kuongeza ushirikiano katika maeneo ya kipaumbele kama sekta ya miundombinu, mifumo ya chakula, biashara na uwekezaji, kubadilishana ujuzi, upatikanaji wa nishati safi na salama na kusaidia ujenzi wa uchumi wa kidijitali.
“Pia kuibua fursa mpya za ushirikiano kwa manufaa ya pande zote mbili, kutangaza maboresho makubwa yaliyofanywa na Serikali katika sheria za sekta ya biashara na uwekezaji ili kuvutia wawekezaji wengi zaidi,” alisema.
Balozi Kombo alisema Rais Samia atafanya mazungumzo na kampuni za China ambazo zipo tayari kufanya uwekezaji mkubwa na kufungua ofisi zao nchini Tanzania.
“Atakutana na kampuni kubwa za China kwa pamoja katika hafla ya chakula cha jioni, yenye lengo la kuhamasisha kufanya uwekezaji nchini Tanzania,” alisema.
Kwa mujibu wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo uwekezaji wa China nchini umefikia sh. trilioni.30
More Stories
Premier Bet yamtangaza mshindi mkubwa
Dkt. Kazungu atembelea miradi ya umeme Dar es Salaam
MSF ilivyojidhatiti kusaidia serikali katika utoaji wa huduma za afya