January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Dkt. Samia, Umaro Sissoco Embalo wa Guinea Bissau walivyoimarisha ushirikiano

Na Jackline Martin,TimesmajiraonlineDar

ZIARA zinazofanywa na marais wa mataifa mbalimbali nchini zimeendelea kufungua fursa mbalimbali. Tumeshuhudia tangu Rais Samia Suluhu Hassan, aingie madarakani ameweza kuimarisha uhusiano wa Tanzania na mataifa mengine.

Hatua hiyo imewezesha marais na viongozi wa juu wa mashirika ya kimataifa kufanya ziara za kikazi hapa nchini. Lakini pia tumeshuhudia mikutano mikubwa ya kimataifa yakifanyika nchini.

Katika mwendelezo wa ziara za marais hapa nchini, mwishoni mwa wiki Tanzania ilikuwa na ugeni wa Rais wa Guinea Bissau, Umaro Sissoco Embalo, ambaye alifanya ziara yake ya siku tatu nchini.

Kupitia ziara hiyo, Serikali ya Tanzania na Guinea Bissau, zimekubaliana kushirikiana katika kilimo cha korosho, afya, elimu, ulinzi na usalama.

Aidha, nchi hizo mbili zimesaini mkataba wa makubaliano wa ushirikiano katika sekta ya uwekezaji na biashara. Akizungumza na waandishi wa habari Rais Samia Suluhu Hassan, baada ya mazungumzo yake ya faragha na Rais wa Guinea Bissau, Umaro Embalo, Rais Samia amesema kwa kuwa mataifa hayo mawili ni wazalishaji wakubwa wa korosho, hivyo wamekubaliana kushirikiana katika kilimo cha zao hilo.

Ushirikiano huo kwa mujibu wa Rais Samia, ni katika utafiti wa kilimo cha zao hilo na uchakataji wake ili zipelekwe sokoni zikiwa zimeshaongezewa thamani.

“Kwa kuwa nchi zetu ni wazalishaji wakubwa wa korosho tumeona tuanze kwa kushirikiana kwenye eneo hili, hasa kufanya utafiti na uchakataji wa korosho,” anasema Rais Samia. Sambamba na ushirikiano huo, maeneo mengine watakayoshirikiana amesema ni katika biashara na uwekezaji.

Anaeleza Afrika kwa sasa ipo mbioni kufungua soko huru, hatua inayotarajia kuongeza viwanda, hivyo ushirikiano ni jambo muhimu ili kuvuna fursa tarajiwa. Ushirikiano mwingine, amesema utafanyika katika afya, elimu, ulinzi na usalama, utalii na masuala ya fukwe.

“Nchi zetu mbili zina eneo kubwa la mwambao wa pwani na zote zipo katika nafasi nzuri ya kufanya biashara na zinapakana na nchi zisizo na mwambao, tutashirikiana katika hili pia,” amesisitiza.

Hata hivyo, anasema katika mazungumzo yao ya faragha pamoja na mambo mengine, wamegusia kuhusu maeneo huru ya uwekezaji na kwamba Rais Embalo atatembelea EPZA.
Nchi mbili hizo, Rais Samia anasema zimekubaliana kushirikiana na mataifa mengine kuhakikisha bidhaa zake za mazao ya kilimo zinauzwa kwa bei nzuri.

Tanzania, Guinea Bissau kushirikiana maeneo haya Mkuu huyo wa nchi, amesema ziara ya Rais Embalo ni mara ya kwanza na kwamba amemwalika naye kwenda kutembelea nchini Guinea Bissau.

Katika hotuba yake, Rais Embalo anasema kuna umuhimu wa mataifa hayo kushirikiana ili kujenga nguvu ya pamoja. Nguvu ya pamoja, amesema itaiwezesha Afrika kufikia malengo yake ya mwaka 2063 ya kuandaa mustakabali wa dunia. Kwa kuwa nchi hizo zina historia ya ushirikiano tangu harakati za ukombozi, Rais Embalo anasema ni muhimu hilo liendelezwe.

“Mataifa ya Afrika yakishirikiana yana uwezo wa kuandaa mustakabali wa dunia, kwa kuwa ina rasilimali za kutosha,” anasema. Ameikaribisha sekta binafsi ya Tanzania kuona fursa zilizopo katika taifa la Guinea Bissau, akidokeza ni lango rahisi la kuzifikia nchi za Magharibi.

“Ni muhimu kubadilisha uhusiano uwe imara zaidi kwani Guinea hawawezi kusahau kuhusu Tanzania na wamekuwa wakifunzwa kuhusu Mwalimu Nyerere shuleni,” ameeleza. Hata hivyo, ameahidi kuleta wanafunzi mbalimbali kwa ajili ya kujifunza Kiswahili, akisema ndiyo lugha inayoiunganisha Afrika.

Akiwa Mamlaka ya Eneo Huru la Uwekezaji kwa Mauzo Nje (EPZA) Rais Sissoco Embaló, alielezwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Charles Itembe, jinsi mamlaka hiyo ilivyoweza kuvutia mtaji wenye thamani ya dola za kimarekani zaidi ya bilioni 2(zaidi ya sh. trilioni 5.3 ) katika Kipindi cha miaka 10.

Akiwa EPZA, ambapo Rais Sissoco Embaló alipata fursa ya kutembelea eneo Maalum la Uwekezaji la Benjamin William Mkapa (BWM-SEZ), Mabibo, aliambiwa na Itembe kuwa kuwa mauzo nje ya nchi katika kipindi hicho yalifikia kiasi cha dola za kimarekani zaidi ya bilioni 2.5 (Zaidi ya sh. trilioni 6.5 za kitanzania).

“Mafanikio haya ya kuvutia mitaji na mauzo nje ya nchi yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na juhudi za Serikali katika kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji, hivyo kuvutia wawekezaji wengi nchini,” alisema.

Anasema kuwa katika Kipindi hiki, EPZA iliweza kusajili zaidi ya viwanda 250 kwenye sekta mbalimbali ambavyo vimetengeneza ajira za moja kwa moja zaidi ya 60,000 na zisizo za moja kwa moja zaidi ya 100,000 kwenye sekta za kilimo, uchakataji wa madini, vifungashio, nyama na bidhaa za miti.

Kati ya viwanda alivyotembelea Rais wa Guinea Bissau ni kile cha Tanzania Tooku Garment ambacho huuza bidhaa zake nchini Marekani.

Rais wa Guinea Bissau alionesha kufurahishwa na namna ambavyo viwanda vinafanya kazi kwa ufanisi mkubwa huku akitoa ujumbe kuwa bara la Afrika litafanikiwa kujenga Uchumi Imara wa viwanda kupitia programu za EPZ and SEZ.

Itembe alimwambia Rais wa Guinea Bissau kuwa eneo la BWM-SEZ lina miundo mbinu ya majengo 21 ambayo yana viwanda mbalimbali vinavyozalisha bidhaa mbalimbali na kuajiri Zaidi ya watanzania 4500 kwa ajira za moja kwa moja na ajira zisizo za moja kwa moja 8600.

Pia eneo la BWM-SEZ limeweza kuvutia mitaji yenye thamani ya dola za kimarekani milioni 51.9 na mauzo nje ya nchi yenye thamani ya dola za kimarekani milioni 82.9 hasa katika sekta za uchakataji wa mazao ya kilimo, kadi Maalum za kielektroniki, Kahawa na nguo.

Anasema kuwa EPZA imejikita katika kutengeneza Maeneo huru za kiuchumi ili kuvutia Uwekezaji kutoka sekta za umma na binafsi.

Serikali imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa programu hizi za SEZ na EPZ zinafanikiwa ili kuweza kuvutia Uwekezaji mkubwa Zaidi na kuchangia katika ujenzi wa Uchumi wa viwanda.

Anasema EPZA inatoa fursa na vivutio mbalimbali kwa wawekezaji ambavyo vinawahakikishia Usalama wa mitaji yao na kupata faidi kutokana na Uwekezaji huo.

Na mfano dhahiri wa juhudi za Serikali katika kuendeleza maeneo ya SEZ ni ile ya mradi wa BWM-SEZ ambapo viwanda mbalimbali vimeanzishwa na kuweza kujengwa na kufanya mchango mkubwa sana katika Uchumi wa viwanda.

Mwishooooooooooooooo