January 2, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Dkt. Samia: Tamasha la Taifa Utamaduni kudumisha Muungano

*Dkt. Ndumbaro ampongeza

Na Mwandishi Wetu, Timesmajiraonline, Songea 

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Tamasha la Taifa la Utamaduni lililofungwa jana Mkoani Ruvuma litaenda kudumisha Muungano kutokana na kushirikisha vikundi kutoka Zanzibar.

Hata hivyo Dkt. Samia aliwapongeza Waandaji na Washiriki wa Tamasha hilo, Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kutokana juhudi kubwa walizozifanya mpaka kufana.

“Nitumie nafasi hii kuwapongeza na kuwashukuru washiriki wote waliofanikisha Tamasha hili la tatu la utamaduni la Kitaifa. Tamasha hili linadumisha muungano kwa kualika vikundi kutoka upande wa pili wa muungano,” alisema Dkt Samia.

Aidha, Rais Samia alivipongeza vikundi vyote kutoka mikoani vikiongozwa na maafisa utamaduni kwa kuonesha umahiri wao mkubwa.

“Nimeambiwa hapa kuna vikundi zaidi ya 20 vilivyoshiriki Tamasha hili na la faraja zaidi linalotia moyo tamasha hili lina dumisha Muungano Nimeaona kikundi kutoka Zanzibar kilichokuwa kikicheza lakini maneno yaliosemwa nilikuwa nafahamu mimi,” alisema Rais.

Mbali na hivyo, Rais Samia alisisitiza umuhimu wa kuhifadhi na kufundisha mila na desturi za kitanzania kwa kizazi kijacho.

Alisema, Serikali itaendelea kuwekeza katika sekta ya utamaduni na sanaa, ikiwa ni pamoja na kuboresha miundombinu ya maeneo ya kihistoria kama vile Uwanja wa Majimaji, ambao una umuhimu mkubwa kwa historia ya Tanzania.

Aliwataka wananchi kushirikiana na Serikali katika kuhifadhi mazingira, hasa maeneo yenye urithi wa kitamaduni, akibainisha kwamba urithi huu ni rasilimali isiyoweza kurejeshwa mara inapoharibika.

Aliwaasa Watanzania kuenzi na kuthamini utamaduni wao kwa kuhakikisha kuwa mila, desturi na lugha zetu za asili zinaendelea kudumishwa

Naye Waziri wa Utamaduni, Sanaa na michezo, Dkt. Damas Ndumbaro alimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kukubali kuhudhuria Tamasha hilo lililofanyika Songea mkoani Rauvuma.

“Rais ulielekeza Rais kuwa matamasha haya yafanyike kwa mzunguko katika mikoa yote tulianza Dar es Salaam 2022, tulienda Njombe 2023, na sasa tupo mkoa wa Ruvuma mjini katika Tamasaha la tatu hii ni sehemu ya utekelazaji wako Rais

“Tunashukuru zaidi umetupa upendeleo mwaka huu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushiriki na kuungana nasi katika Tamasha hili,

“Kauli mbiu ya mwaka huu ‘Utamaduni wetu ni utu wetu tuuenzi na kuuendeleza’, na sisi wizara tunatekeleza kwa vitendo kauli mbiu hiyo kwa kufuata maelekezo yako,” alisema Dkt Ndumbaro.