January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Dkt. Samia, Mwinyi na dhamira isiyotiliwa shaka ulinzi wa Muungano

Na Penina Malundo,Timesmajiraonline,Dar

JANA Tanzania imeingia kwenye historia kwa kuadhimisha miaka 60 ya Muungano. Tanzania ina kila sifa za kujivunia Muungano huo, kwani mataifa mengi yakiwemo yenye nguvu za kiuchumi yalipojaribu kuungana, yalishindwa.

Matokeo yake, mataifa mengi yanabaki kuutazama Muungano wetu kwa jicho la usuda, huku wakijiuliza Watanzania wameweza. Pamoja na Tanzania kuna na makabila zaidi ya 121, lakini wanaongea lugha moja ndani ya Muungano.

Sifa hizi ni lazima ziwaendee viongozi wakuu wa nchi katika awamu zote, upande wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzaia na upande wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Leo hii tunaendelea kushuhudia jinsi Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, wanavyoendelea kuulinda Muungano.

Ili kuhakikisha Muungano unaendelea kuwa imara, Rais Samia anawataka Watanzania kuendelea kudumisha amani, umoja na mshikamano wa Taifa kwa kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kudumisha uzalendo kwa kuwaenzi kwa vitendo waasisi wa Muungano.

Rais Samia ametoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki wakati wa uzinduzi wa vitabu viwili vya Muungano, ikiwemo Kitabu cha Miaka 60 ya Historia Ofisi ya Makamu wa Rais na Kitabu cha Safari ya Picha ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania miaka 60 kilichoandaliwa na sekta binafsi.

Rais Samia anasema ais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa amesimama wakati Wimbo wa Taifa wa Tanzania na ule wa Afrika Mashariki ukiimbwa katika Sherehe za Miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar tarehe 26 Aprili, 2024

“Namshukuru Mungu kwa neema hii ya kukutana katika tukio la uzinduzi wa vitabu vyetu a kuelekea katika kilele cha maadimisho ya miaka 60 ya tanganyika na zanzibar tunamshukuru Mungu kwa amani na utulivu kwa muungano wetu,”alisema. kama nchi kuna umuhimu wa kutunza historia, ambapo itaeleza tumetoka wapi, tulipo na tunapokwenda hata vijana ambao wamezaliwa baada ya Muungano wataweza kusoma na kujua historia.

Anasema ana uhakika Watanzania wakisoma vitabu vyote viwili watapata mambo ambayo hawakuwa wanayajua.

“Mimi ninajaribu kidogo tu kwa Baraza langu (la mawaziri) naona wote wanaangaliana machoni na wote wamezaliwa baada ya Muungano,”anasema na kuongeza;

“Kwa hiyo hii pengine hatujaweka kipaumbele kwa watu kuelewa Muungano wetu, hivyo niombe watu wasome na kuweka vizuri kumbukumbu hizi katika maeneo yetu ya historia.”

Rais Samia anasema nakala za vitabu hivyo vyote viwili vinapaswa kutolewa na kila mtu havisome vitabu hivyo, kwani watapata vitu ambavyo hawakuwa wanavijua vinavyohusu Muungano.

“Napongeza wazo zuri la Ofisi ya Muungano ya Makamu wa Rais na pia nawashukuru Sekta Binafsi kwa kuandika kitabu cha pili ili kuonesha tunatambua mchango wao ni vema kusoma vitabu hivi na kuzingatia yaliyomo katika vitabu hivyo,”anasema.

Anasema taarifa zilizopo katika vitabu hivyo zinaweka historia nzuri ya nchi na kutumika kwa mambo kadhaa ikiwemo kwa watu wanaotaka kujua historia ya nchi.

“Taarifa hizi zinaweka historia ya nchi yetu katika nafasi nzuri na kuweza kutumika kwa mambo kadhaa, kwani kuna wenzetu wanasomesha kwa African Study ambapo wao uwa wanapelekwa nchi mbalimbali kujifunza na kujua historia za nchi hivyo wanaweza kusoma vitabu hivi na kujua mapito ya muungano wetu,”anasema na kuongeza;

“Juzi nilikuwa nchini Uturuki tuliona namna wenzetu wanavyotunza utalii kwa historia zao,hivyo ni muhimu na sisi kutunza historia hizi.”

Anasisitiza uwekwaji mzuri na utunzwaji wa vitabu hivyo ili kusaidia watu watakaokuja kusoma na kupitia vitabu hivyo kwa kujua historia.

Aidha, Rais Samia anawataka waandishi na waandaaji wa vitabu hivyo kuandikwa kwa lugha mbili ya Kiingereza na Kiswahili ili kurahisisha Watanzania wengi kusoma na kukielewa.

“Hiki Kitabu cha kwanza kwa kuwa kipo kwa kiswahili, hivyo kinatakiwa kutafsiriwa kwa lugha ya Kiingereza pia ili watu wengine waweze kusoma na kukielewa pia kwa hiki kitabu kilichotolewa na sekta binafsi nacho kitafsiriwe kwa lugha ya Kiswahili ili Watanzania waweze kusoma na kuelewa historia ya Muungano,”anasema.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwapungia mkono wananchi mara baada ya kuwasili katika uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam wakati wa Sherehe za Miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar tarehe 26 Aprili, 2024.

Kwa Upande wake Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, anaishukuru Ofisi ya Makamu wa Rais pamoja na Sekta Binafsi kwa kutengeneza vitabu hivyo vya Muungano, kwani watu wengi wamezaliwa baada ya Muungano.

Anasema ndani ya vitabu hivyo kutakuwa na mafanikio mengi yaliyozungumziwa pamoja na changamoto mbalimbali ambazo baadhi ya changamoto hizo zimeweza kutatuliwa.

“Tunaowajibu wa kuwakumbuka na kuwaenzi waasisi wetu na hakuna njia nzuri zaidi ya kufanya hivi na kuwaweka katika kumbukumbu ili vijana wetu wakisoma waweze kujifunza,”anasema Dkt. Mwinyi.

Naye Makamu wa Rais, Dkt. Philipo Mpango, anasema ni jambo la kumshukuru Mungu kwa kufikisha miaka 60 sasa ya Muungano.

“Nakushukuru Rais Samia na Rais wa Zaznzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Mwinyi kwa kuendelea kudumisha Muungano, kwani uongozi wenu umewezesha Taifa kuendelea kuwa imara, kudumisha undugu, maendeleo ya kiwango,” anasema Dkt. Mpango.

Anasema mwaka 2022 Ofisi ya Makamu wa Rais iliandaa kitabu ambacho kinaitwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar chimbuko la Misingi na Maendeleo na hiyo ilikuwa sehemu ya maadhimisho ya miaka 58 ya Muungano.

Anasema kitabu hicho kiliandaliwa kutokana na takwimu za kidimographic kwa Sensa ya mwaka 2022 Watanzania ambao wamezaliwa baada ya Muungano ni asilimia 77.3, ambapo Watanzania karibu robo tatu ni vijana ambao wanahusikia Muungano au kuusoma .

“Kwa sababu hiyo Watanzania wengi tulionao wanahusikia Muungano, hivyo kuna uhitaji mkubwa wa kupata uelewa na kufahamu historia ya Muungano , mafanikio yaliyotokana na pande zote mbili ,changamoto mbalimbali za Muungano na namna zilivyo tatuliwa,”anasema na kuongeza,

“Na pia natoa wito kwa wananchi wote kutimiza wajibu wao wa kuuenzi na kudumisha Muungano ili kuweza kuendeleza kwa faida ya vizazi vya sasa na vizazi vijavyo,”anasema.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Samia Suluhu Hassan akikagua Gwaride la Heshima lililoandaliwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wakati wa Sherehe za Miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Sherehe hizo zimefanyika katika uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam tarehe 26 Aprili, 2024.

Anasema katika kuadhimisha miaka 60 ya Muungano nchini, mwaka huu Ofisi ya Makamu wa Rais iliamua kuendeleza jitihada ya kuongeza elimu kuhusu Muungano na kwa kufanya hivyo wameweza kuandika kitabu .

“Nawashukuru viongozi wote 13 walihudumu katika wadhifa ya makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tangu kuanzishwa kwake mwaka 1964.”

Anasema viongozi hao waliweka msingi imara wa utekelezaji wa majukumu ya kazi ya ofisi ya makamu wa Rais ambayo imemuwezesha kutekeleza majukumu yake ya kikatiba pamoja na kuratibu masuala ya Muungano na kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika mambo ambayo yasiyoya muungano.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Dkt. Mohamed Said Dimwa, anasema chama hicho kinaridhishwa na juhudi za Serikali zote mbili katika kuimarisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Anasema Muungano huo unaendelea kuvunja rekodi ya kudumu kwa miaka mingi zaidi ya Miungano ya nchi nyingine barani Afrika na duniani kwa ujumla, kutokana na dhamira ya dhati ya kuasisiwa kwake.

Anasema kuimarika kwa Muungano huo ni kutokana na mchango wa viongozi wote katika Serikali ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kusimamia, kudumisha na kuimarisha umoja, amani na mshikamano.

Dkt. Dimwa anawapongeza Rais Samia na Rais Mwinyi kwa ushirikiano mzuri na kazi kubwa wanayoifanya kuhakikisha Muungano huo unaendelea kuwa na tija kwa nchi zote mbili.

“Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/2025 ibara ya 246 (b), Chama Cha Mapinduzi imeelekezwa kudumisha Muungano, hivyo hiki ni kipaumbele kwetu na lazima tusimamie kwa vitendo na gharama yoyote.”Anasema.

“Hakuna mwananchi wa Zanzibar na Tanzania bara asiyenufaika na Muungano huu, kwani umegusa kila sehemu kuanzia katika asili zetu, maisha yetu ya kila siku ya kutafuta riziki, fursa za kiuchumi na kijamii pamoja na ukuaji wa demokrasia inayotegemea utashi wa kisiasa.” anasema Dkt. Dimwa

Anasema wapo baadhi ya wanasiasa na wasomi wanaoukosoa Muungano huo kutokana na utashi wa itikadi za vyama vyao, bila kuridhia hoja ya kutafuta suluhu ya kumaliza kasoro ndogo ndogo zilizopo katika Muungano huo.

Pamoja na hayo, anasema watu wanaoukosoa Muungano huo wajue kwamba haukuundwa kwa msukumo wa kisiasa, bali ni kutokana na maslahi mapana ya kiuchumi na kijamii, yaliyolenga kuleta manufaa kwa wananchi wa pande zote mbili.

Anasema Zanzibar imeendelea kuimarika kutokana na uwepo wa taasisi za Muungano zinazotoa huduma bora kwa wananchi wote bila ubaguzi.

Dkt. Dimwa anasema Chama Cha Mapinduzi kinaamini kuwa uimara wa uchumi na maendeleo endelevu ya kuivusha Zanzibar kufikia katika hadhi ya nchi za visiwa zilizoendelea kiuchumi, ni kuimarika kwa tunu ya Muungano huo.

Dkt. Dimwa anataja mafanikio ya Muungano ni wananchi wa pande zote mbili kuendelea kuwa huru katika kutembea na kuishi sehemu yoyote ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hatua ambayo ni fursa kubwa kwa wananchi wa Zanzibar.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwapungia mkono wananchi mara baada ya kushuka kwenye gari Maalum la Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wakati wa Sherehe za Miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Sherehe hizo zimefanyika katika uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam tarehe 26 Aprili, 2024.

Anasema kuimarika kwa undugu, amani, utulivu, mshikamano baina ya wananchi wa pande zote mbili ni hatua kubwa ya mafanikio, kwani hakuna kiashiria chochote cha uwepo wa migogoro ya kijamii inayoweza kuingiza nchi katika machafuko.

Pamoja na hayo, Dkt.Dimwa, anasema kuimarika kwa fursa za ajira na biashara ni sehemu ya mafanikio ya uwepo wa Muungano huo.

Mafanikio mengine ni utatuzi wa changamoto za Muungano ambazo kwa miaka mingi zilikuwa zikilalamikiwa ambapo kwa sasa zimebaki chache na muda wowote zitatatuliwa zote.

Dkt.Dimwa, anaeleza kuwa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar kitaendelea kusimamia misingi yake ya kuendeleza utawala wa haki, sheria, uwajibikaji na utawala bora ili wananchi waendelee kunufaika na matunda ya Muungano.

Anaongeza kwamba ndani ya Muungano huo CCM Zanzibar itahakikisha inasimamia kwa vitendo sera zake ili ziwe chachu ya kunufaisha wananchi wa visiwa vya hivyo vya kihistoria.