March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Dkt.Samia kuzindua Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

RAIS Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuzindua Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 Julai 17, 2025 jijini Dodoma baada ya kukamilika kwa mchakato wa maandalizi uliodumu kwa takribani miaka miwili.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa leo Julai 15,2025 Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango,Dkt. Fred Msemwa amesema maandalizi ya Dira hiyo yamefanyika kwa ushirikishwaji mpana wa wananchi, ambapo zaidi ya watanzania milioni 1.17 walitoa maoni yao kupitia njia mbalimbali huku zaidi ya watu 20,000 wakishiriki makongamano ya kitaifa.

“Kazi ya ukusanyaji maoni ilifanyika kwa njia ya mbalimbali ikiwemo kupita kwenye familia moja moja,njia ya ujumbe wa simu njia ya makongamano na mikutano kwa takribani Kanda zote za Tanzania Bara na Zanzibar pamoja na njia ya mitandao ya kijamii,”amesema.

Dkt.Msemwa amesema Tume ilijifunza kutoka kwa nchi zilizofanikiwa kufikia uchumi wa kati, ili kubaini mbinu bora zinazoweza kutumika nchini, kabla ya kurejesha rasimu kwa wananchi kwa ajili ya uhakiki wa mwisho.

Amesema Dira hiyo ilijengwa kwa kuzingatia uzoefu na maarifa kutoka kwa nchi zilizoendelea kiuchumi kama Botswana ,Afrika Kusini,Brazil,Malaysia na Singapore kwa kupitia tafiti na mawasiliano ya moja kwa moja

Ameeleza kuwa Utekelezaji wa Dira hiyo utaanza rasmi Julai 2026 baada ya kumalizika kwa Dira ya Maendeleo ya 2025, ikiwa ni mwongozo mpya wa maendeleo kwa miaka 25 ijayo.