March 28, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Dkt. Samia kufanya ziara Namibia, kushiriki uapisho wa Rais Mpya

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dar es Salaam

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kufanya ziara rasmi nchini Namibia kesho, Machi 21, 2025, ili kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais Mteule wa nchi hiyo, Netumbo Nandi-Ndaitwah.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa na kusainiwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Ikulu, Rais Dkt. Samia amepokea mwaliko kama Mgeni Rasmi na anatarajiwa kuhutubia katika sherehe hizo zitakazofanyika sambamba na Maadhimisho ya Miaka 35 ya Uhuru wa Namibia.

Tanzania na Namibia zina uhusiano wa kihistoria na wa kidugu, ulioasisiwa na viongozi waasisi wa mataifa hayo, Hayati Julius Nyerere na Hayati Sam Nujoma, wakati wa harakati za ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika. Mahusiano hayo yameendelea kuimarishwa kupitia ushirikiano wa kidiplomasia, kiuchumi, na kijamii kati ya nchi hizo mbili.

Mbali na kuhudhuria sherehe za uapisho, Rais Dkt. Samia anatarajiwa kukutana na mwenyeji wake, Rais Mteule Netumbo Nandi-Ndaitwah, kwa mazungumzo yanayolenga kukuza na kuimarisha uhusiano wa Tanzania na Namibia.

Hafla hii ina umuhimu wa kipekee, kwani kwa mara ya kwanza Namibia inapata Rais Mwanamke, jambo linaloifanya Afrika kuwa na marais wawili wa kike waliopo madarakani kwa sasa, akiwemo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wa Tanzania.

Sherehe hizi zinatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi wa mataifa mbalimbali pamoja na wawakilishi wa taasisi za kimataifa, zikionesha mshikamano wa Afrika katika demokrasia na maendeleo ya kisiasa.