January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Dkt. Samia awahimiza Watanzania kudumisha amani

Na Penina Malundo,Timesmajiraonline, Dodoma

RAIS Samia Suluhu Hassan amewaomba Watanzania kuendelea kudumisha Amani, Umoja na Mshikamano wa Taifa kwa kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kudumisha uzalendo kwa kuwaenzi kwa vitendo waasisi wa Muungano.

Rais Samia aliyasema hayo jana wakati wa uzinduzi wa vitabu viwili vya Muungano, ikiwemo Kitabu cha Miaka 60 ya Historia Ofisi ya Makamu wa Rais na Kitabu cha Safari ya Picha ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania miaka 60 kilichoandaliwa na sekta binafsi.

Aidha, katika hafla hiyo amewatunuku nishani viongozi mbalimbali viongozi ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha miaka 60 ya Muungano.

“Namshukuru Mungu kwa neema hii ya kukutana katika tukio la uzinduzi wa vitabu vyetu a kuelekea katika kilele cha maadimisho ya miaka 60 ya tanganyika na zanzibar tunamshukuru Mungu kwa amani na utulivu kwa muungano wetu,”amesema.

Rais Samia amesema kama nchi kuna umuhimu wa kutunza historia, ambapo itaeleza tumetoka wapi, tulipo na tunapokwenda hata vijana ambao wamezaliwa baada ya Muungano wataweza kusoma na kujua historia.

Amesema ana uhakika Watanzania wakisoma vitabu vyote viwili watapata mambo ambayo hawakuwa wanayajua.

“Mimi ninajaribu kidogo tu kwa Baraza langu (la mawaziri) naona wote wanaangaliana machoni na wote wamezaliwa baada ya Muungano,”amesema na kuongeza;

“Kwa hiyo hii pengine hatujaweka kipaumbele kwa watu kuelewa Muungano wetu, hivyo niombe watu wasome na kuweka vizuri kumbukumbu hizi katika maeneo yetu ya historia.”

Rais Samia alisema nakala za vitabu hivyo vyote viwili vinapaswa kutolewa na kila mtu havisome vitabu hivyo, kwani watapata vitu ambavyo hawakuwa wanavijua vinavyohusu Muungano.

“Napongeza wazo zuri la Ofisi ya Muungano ya Makamu wa Rais na pia nawashukuru Sekta Binafsi (Private Sekta) kwa kuandika kitabu cha pili ili kuonesha tunatambua mchango wao ni vema kusoma vitabu hivi na kuzingatia yaliyomo katika vitabu hivyo,”amesema.

Amesema taarifa zilizopo katika vitabu hivyo zinaweka historia nzuri ya nchi na kutumika kwa mambo kadhaa ikiwemo kwa watu wanaotaka kujua historia ya nchi.

“Taarifa hizi zinaweka historia ya nchi yetu katika nafasi nzuri na kuweza kutumika kwa mambo kadhaa, kwani kuna wenzetu wanasomesha kwa African Study ambapo wao uwa wanapelekwa nchi mbalimbali kujifunza na kujua historia za nchi hivyo wanaweza kusoma vitabu hivi na kujua mapito ya muungano wetu,”alisema na kuongeza

“Juzi nilikuwa nchini Uturuki tuliona namna wenzetu wanavyotunza utalii kwa historia zao,hivyo ni muhimu na sisi kutunza historia hizi,”amesema.

Amesisitiza uwekwaji mzuri na utunzwaji wa vitabu hivyo ili kusaidia watu watakaokuja kusoma na kupitia vitab hivyo kwa kujua historia.

Aidha Rais Samia aliwataka waandishi na waandaaji wa vitabu hivyo kuandikwa kwa lugha mbili ya Kiingereza na Kiswahili ili kurahisisha watanzania wengi kusoma na kukielewa.

“Hiki Kitabu cha kwanza kwa kuwa kipo kwa kiswahili hivyo kinatakiwa kutafsiriwa kwa lugha ya Kiingereza pia ili watu wengine waweze kusoma na kukielewa pia kwa hiki kitabu kilichotolewa na sekta binafsi nacho kitafsiriwe kwa lugha ya Kiswahili ili Watanzania waweze kusoma na kuelewa historia ya Muungano,”alisema.

Kwa Upande wake Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi , Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameishukuru Ofisi ya Makamu wa Rais pamoja na Sekta Binafsi kwa kutengeneza vitabu hivyo vya Muungano, kwani watu wengi wamezaliwa baada ya Muungano.

Amesema ndani ya vitabu hivyo kutakuwa na mafanikio mengi yaliyozungumziwa pamoja na changamoto mbalimbali ambazo baadhi ya changamoto hizo zimeweza kutatuliwa.

“Tunaowajibu wa kuwakumbuka na kuwaenzi waasisi wetu na hakuna njia nzuri zaidi ya kufanya hivi na kuwaweka katika kumbukumbu ili vijana wetu wakisoma waweze kujifunza,”amesema Dkt. Mwinyi.