Na Joyce Kasiki, Timesmajira online,Dodoma
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Leo amewaapisha Mawaziri na Manaibu Mawaziri wa Baraza jipya aliloliteua na kulitangaza Novemba 17, 2025, huku akiwaagiza kufanya kazi kwa bidii na kuwatumikia wananchi badala ya kujivunia nafasi walizopewa.
Akizungumza Ikulu ya Chamwino, Dodoma, muda mfupi baada ya hafla ya uapisho, Rais Dkt. Samia alisema Serikali kupitia kampeni za uchaguzi iliahidi mambo mengi kwa wananchi, hivyo ni wajibu wa Baraza hilo kutumia kikamilifu muda wa miaka mitano iliyopo kuhakikisha ahadi hizo zinatimia.
Rais Samia alisema ana imani kuwa majukumu aliyowapa Mawaziri yanaenda kubebwa kwa weledi na kwa kuzingatia misingi ya utumishi wa umma.
Alisisitiza kuwa dhamana wanayopewa ni ya kufanya kazi kwa niaba ya Watanzania, na sio ya kujiona au kudhani kuwa uwaziri ni cheo cha kujitapa.
Akitangaza kaulimbiu ya kipindi hiki kuwa “Kazi na Utu, Tunasonga Mbele”, Rais Samia alieleza kuwa maana yake ni kuzingatia utu wa wananchi, kuanzia kwa viongozi wenyewe na kisha kwa watumishi wanaowahudumia Watanzania.
“Utu uanze na sisi, kisha tukawatumikie wengine. Utu ni neno pana. Watakaobeba uwaziri kama fahari kwamba watanijua huko mitaani, Mimi nitakuwa nafuatilia ,na sioni shida kubadilisha. Nitabadilisha mpaka nipate yule atakayefanya kazi ya kuwatumikia na kuwaletea wananchi maendeleo kwa moyo mmoja,” alisema Rais Samia.
Aliongeza kuwa kazi ya msingi kwa Baraza hilo ni kuwajibika kwa Watanzania, kwani ahadi walizopewa wananchi ni nyingi huku muda wa kuzitekeleza ukiwa mfupi.
“Kwa hiyo, kwa majukumu niliyowapa leo, aliye mzito apunguze kilo ili tukimbie,” alisisitiza Rais Dkt Samia
Kuhusu rasilimali, Rais Samia alisema kuwa Tanzania inakabiliwa na upungufu wa rasilimali za ndani na mara nyingi imekuwa ikitegemea mikopo kutoka mataifa rafiki.
Hata hivyo alisema changamoto zilizojitokeza katika siku za karibuni zimeleta doa linaloweza kuchelewesha kupata fedha hizo.
Kutokana na hilo, alisisitiza umuhimu wa kutumia kikamilifu rasilimali za ndani ambazo nchi imejaaliwa na Mungu, na kwamba Serikali ya Awamu ya Sita katika kipindi chake cha pili itahakikisha miradi mingi inatekelezwa kwa fedha za ndani kabla hata ya fedha za nje kupatikana.
“Hatutasubiri. Tutaanza kwa fedha za ndani, na wao wakimaliza ‘objection’ zao watatukuta tunaendelea,” alisema.
Aidha, Rais Samia aliwakumbusha Mawaziri kuwa Serikali iliahidi kufanikisha mambo kadhaa ndani ya siku 100 za kwanza za kazi, hivyo aliwataka kuhakikisha ahadi zinazogusa wizara zao zinatekelezwa mara moja.
Akitangaza ratiba ya kazi, alisema Mawaziri wote watakutana naye Ikulu kesho Nov 20,2025 kwa ajili ya kuchambua ahadi zote walizoahidiwa wananchi na kupanga utekelezaji wake kwa wakati.
“Nataka matokeo katika miradi tunayokubaliana kwa wananchi
Aidha Rais Samia aliwapongeza kwa kuaminiwa lakini akawakumbusha kuwa dhamana mbele yao ni nzito .“Hongereni sana, lakini mna kazi kubwa mbele yenu,” alisema.

More Stories
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina
Kihongosi: Msigombane kwa itikadi za vyama