December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Dkt.Samia atoa agizo waathirika maporomoko ya udongo kupatiwa viwanja

Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya

RAIS Dkt.Samia Suluhu Hassan ametoa agizo Serikali mkoani Mbeya kuwapatia viwanja vya kujenga nyumba waathirika 21 wa maporomoko ya udongo yaliyotokea katika mlima Kawetele Kata ya Itezi baada ya makazi yao kufunikwa na tope April 13 mwaka huu

Kauli hiyo imetolewa April 21,2024 na Spika wa Bunge na Mbunge wa Jimbo la Mbeya na Rais Umoja wa Mabunge Duniani (IPU)Dkt.Tulia Ackson wakati akizungumza na waathirika hao ambao wamehifadhiwa katika vyumba vya madarasa shule ya msingi Tambukareli.

Dkt.Tulia amesema alipokea taarifa ya maporomoko kutoka kwa uongozi wa mkoa lakini anashukuru wadau mbalimbali wamejitokeza kutoa misaada akiwepo Rais .

“Leo nimekuja na ujumbe maalum wa Rais Samia kwanza kabisa alimuagiza katibu mkuu Dkt,Emmanuel Nchimbi alileta Sh 10 milioni na pia kiasi cha Sh 42 milioni zilizokolewa na Mkuu wetu wa mkoa ambazo zimesaidia kununua mahitaji kama magodoro,blanketi,chakula na vinginevyo.

“Dkt.Tulia amesema changamoto kama hizo zimetokea mikoa mingi hapa nchini lakini wana Itezi wamepata kitu cha ziada,”amesema.

Hata hivyo Dkt.Tulia amesema baada ya kupatiwa viwanja waathirika hao bado watahitaji kujenga nyumba hivyo ameomba wadau mbalimbali kuendelea kujitokeza kuchangia vifaa vya ujenzi ikiwemo Saruji,tofari ,bati na vitu vingine muhimu ambavyo vitahitajika katika ujenzi katika kuwasaidia wahanga hao.

Dkt.Tulia ameleeza kuwa viwanja hivyo vimetolewa maalum kwasababu ya namna changamoto hiyo ilivyotokea na kuwa suala la nyumba kumezwa na maporomoko ya udongo ulioambatana na tope lenye uji uji kutokana na kumeguka kwa mlima Kawetele kata ya Itezi.

“Mnafahamu nyumba zilibomoka Uyole, Nsalaga,Igawilo hawakupatiwa viwanja lakini nyinyi mmepatiwa viwanja,nashangaa nasikia kuna watu wanasema mbona hawajengewa nyumba ndugu zangu wana Itezi msikubali kusikiliza maneno ya uchonganishi “amesema Dkt.Tulia.

Aidha Dkt.Tulia amesema anafahamu kuwa kuna kundi la waathirika lipo tofauti ambapo wapo ambao nyumba zao zimefunikwa na tope na wengine nyumba kupona na kuwa na hofu sababu tope hilo halijamaliza safari kutokana na mvua kuendelea kunyesha ,uongozi wa mkoa utengeneze mazingira kuelekeza tope hilo ili mvua inayoendelea kunyesha tope hilo liekee huko ili athari isitokee tena.

William Lukuvi ni Mshauri wa Rais kutoka Ikulu na Mbunge wa Jimbo la Isimani amesema kuwa mh .Rais alitoa salamu kupitia kwa mkuu wa mkoa wa Mbeya hivyo Dunia na Tanzania nzima imejua Rais amefika Mbeya ndo sababu wasaidizi wengi wanafika kutoa msaada kwa waathirika.

“Lakini kwa haraka Rais akatoa agizo kwa waziri mkuu kufungua Ghara la kuhifadhi chakula na anasema hatawaacha wananchi wake waliopatwa na janga hilo wakakosa chakula na hawezi kuwaacha mkafa njaa “amesema Lukuvi.

Hata hivyo amewataka wananchi kuzingatia masuala ya mazingira na sasa mmejifunza hata yake mambo ambayo hamjawahi kuona lakini yanatokea na kuwataka kuwa macho kuacha kulima kwenye Milima
kwani wanalainisha udongo ili yasitokee tena .

Mkuu wa mkoa wa Mbeya,Juma Homera amekiri kupokea maelekezo kutoka Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kuwapatia viwanja waathirika wa maporomoko ya udongo mlima Kawetele kata ya Itezi wa watu 21 na utekelezaji huo utaanza wiki ijayo.

“Tutatoa viwanja sehemu nzuri kabisa,Dkt.Tulia na wasaidizi wa Rais nakiri kupokea maelekezo ndani ya wiki tatu naenda kutekeleza na waathirika wote waorodheshwe majina ili wapatiwe viwanja maeneo mazuri”amesema.