Na George Mwigulu,Timesmajira Online,Katavi.
RAIS Dkt.Samia Suluhu Hassan ameshtushwa na takwimu za mimba za utotoni pamoja na udumavu kwa watoto mkoani Katavi licha ya Mkoa huo kuwa kinara kwenye uzalishaji wa mazao ya chakula.
Mkoa wa Katavi unaonesha kuwa asilimia 32.2 ya watoto chini ya umri wa miaka 5 wanaudumavu unaotokana na tatizo la lishe duni na mimba za utotoni ni asilimia 19.4.
Rais Dkt Samia Julai 13, 2024 akihutubia wananchi kwenye kilele cha wiki ya Wazazi kitaifa kilichofanyika uwanja wa CCM Azimio Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda,amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko kushughulikia matatizo hayo ambayo ni kikwazo kwa ustawi wa jamii.
Wakati akisisitiza juu ya uadilifu kwa mawakala wa usambazaji mbolea kuepuka kuzichepusha kwa magendo nje ya nchi kuwa unahatarisha uzalishaji bora wa mazao ya kilimo nchini amesema licha ya mchango mkubwa wa Katavi kwa uzalishaji wa chakula lakini bado unalishe duni.
“Taarifa za kitaalamu zinasema kwamba asilimia 32.2 ya watoto chini ya miaka 5 ndani ya Mkoa huu wa Katavi wanaudumavu tufanyie kazi suala hili ili kuokoa jamii yetu na taifa kwa ujumla,” amesema Rais Samia na kuongeza kuwa;
“Nimemuona Mkuu wa Mkoa wa Njombe ndugu yangu Mtaka nilimsema hadharani nikamtia aibu na Mkoa wake lakini aliporudi tu amekwenda kufanya programu nzuri ambayo mpaka leo inaendelea na ninampa muda kumpima amepunguza kwa kiasi gani”.
“Sasa nikuombe Mama yangu Mwanamvua hebu soma kwa mwenzio uone utafanya nini ili kupunguza udumavu ndani ya Mkoa wako lile gamba mnaloniletea kila baada ya miezi sita sitaki tena kuona zile rangi nyekundu zinajitokeza udumavu uzito mdogo yasijitokeze fanyeni kazi chakula kipo cha kutosha” Amesisitiza Rais Dkt Samia.
Rais amefafanua kuwa shughuli nyingi za wazazi hawana muda wa kutunza watoto na kusababisha mtoto kulelewa na mtoto chakula kinachoachwa wakubwa wanakula na kuwanyima wadogo.
“Katika maeneo mengine ili mama hakikishe mtoto hatasumbua akitoka kwenye safari zake baada ya uji aliompatia asubuhi anamuwekea na vyakulevya kidogo na mtoto analewa,kipindi mtoto amelala anakosa milo miwili anakuja kupewa mlo usiku analala tena kwaio niombe sana Wakuu wa Mikoa,Wakuu wa Wilaya lishughulikieni hili kwa kutoa elimu kwa wazazi,”.
Katika kutekeleza sera mpya ya elimu serikali imetoa kipaumbele kwenye elimu ya ujuzi ambapo amewaomba wananchi kuhakikisha watoto wanasoma kwa bidii na wasikatishe masomo.
Amewataka wananchi wa Mkoa wa Katavi wasikatishe masomo ya wanafunzi wa kike na watu wasio kuwa na maadili kwani takwimu ndani ya Mkoa huo zinaonesha kuwa asilimia 19.4 ya wasichana ni wajazazito na wazazi ni watoto wa miaka 14 hadi 19.
“Sasa jifikirie nyumbani kwako unamsichana wa miaka 14 ana tumbo limevimba kama mzazi unakuwa na mambo mengi sana unayafikiria je ataweza kujifungua? Je itakuwaje? imekuwaje?…kwaio hili nalo Mkuu wa Mkoa na viongozi liangalie vizuri,”amesisitiza Dkt Samia.
Makamo Mwenyekiti wa CCM Bara Abdulrahman Kinana kwa upande wake ametoa tahadhari kwa wagombea na wananchi kuelekea uchanguzi wa serikali za mitaa mwaka huu na uchanguzi Mkuu utakao fanyika mwakani suala la kuepuka rushwa ni muhimu ili kupata viongozi waadilifu.
Kinana amesema kuwa maadili ni muhimu katika kupata viongozi bora ambao wanauwezo wa kuongoza jamii hivyo ameshangazwa tabia iliyozuka hivi karibu ya wananchi wenyewe kuwa chachu ya kuomba rushwa jambo ambalo wanapaswa kuliacha.
Kwa upande wa wananchi wa Mkoa wa Katavi, Mariamu Hussein mkazi wa Wilaya ya Tanganyika amesema kuwa ni muhimu jamii kwa pamoja ikachukua jukumu la kuwalinda watoto dhidi ya watu wasio kuwa na maadili ambao wamekuwa chanzo cha wasichana wengi kukatishwa masomo kwa kupata mimba.
Aidha Mariamu amewaomba viongozi kuanzia ngazi ya kijiji/mtaa hadi Mkoa kutoa elimu ya umuhimu ya lishe kwa watoto kwani jamii haifahamu namna bora ya utoaji wa chakula kwa watoto.
More Stories
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa
NLD kipo tayari kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa