Na Allan Kitwe, Timesmajiraonline,Tabora
RAIS Samia Suluhu Hassan, amepongezwa kwa kudumisha demokrasia na kulinda tunu ya amani nchini.
Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tabora, Said Juma Nkumba, alipokuwa akiongea na mwandishi wa gazeti hili ofisini kwake jana.
Alieleza tangu aingie madarakani Rais Samia amekuwa kinara wa demokrasia na maendeleo na ameunganisha Watanzania wote pasipo kujali itikadi zao za kisiasa, kabila wala dini, na ameendelea kuwahakikishia usalama wao.
“Tunampongeza sana Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kinara wa demokrasia na kudumisha tunu ya amani nchini na kutoa fursa kwa wanasiasa wa vyama vyote kufanya shughuli zao pasipo kuvuruga amani ya nchi,”alieleza.
Alibainisha kuwa mwamko na ushiriki mkubwa wa vyama vya siasa katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliomalizika hivi karibuni ni ushahidi tosha kuwa serikali ya awamu ya 6 inayoongozwa na CCM imedumisha demokrasia nchini.
Nkumba alisisitiza kuwa hata maeneo ambako CCM imeshindwa ni ushahidi tosha kuwa wananchi wana haki ya kuamua nani awe kiongozi wao kupitia karatasi ya kura na serikali imeheshimu demokrasia hiyo.
Akizungumzia mafanikio chanya ya miaka 63 ya Uhuru, alisema kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa kimaendeleo na wananchi sasa wanatembea kifua mbele kutokana na maboresho makubwa ya huduma za kijamii katika maeneo.
Alitaja baadhi ya mafanikio hayo kuwa ni kujengwa kwa zahanati, vituo vya afya, hospitali za Wilaya, Mikoa na zile za Rufaa, na hii imesaidia kumaliza au kupunguza kero ya upatikanaji huduma za afya kwa kiasi kikubwa sana.
Mengine ni kuboreshwa miundombinu ya barabara na kujengwa barabara za lami, shule za kisasa, umeme kila kijiji na kitongoji, wananchi kuwezeshwa mikopo na serikali na kutekeleza miradi ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa-SGR.
Nkumba aliongeza kuwa ushiriki wa wananchi katika shughuli za kiuchumi umeongezeka sana kutokana na mazingira mazuri yaliyowekwa na serikali, na hii imechochea ongezeko la wawekezaji, uhuru wa wananchi kuanzisha biashara (maduka na vibanda), aidha kuwepo usafiri wa mabasi masaa 24 ni matunda ya kudumishwa usalama nchini.
More Stories
Wizara ya madini yakusanya bil.521 nusu ya kwanza mwaka wa fedha 2024/25
Meya awafunda wenyeviti Serikali za Mitaa
Mgeja aipongeza CCM kwa uteuzi Wagombea Urais