December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Dkt. Samia ana kwa ana na matajiri wa dunia Brazil leo

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline

MKUTANO wa 19 wa viongozi kundi la G20 unaanza leo Jumatatu mjini Rio De Jenairo Brazil ambapo ushiriki wa Tanzania unatajwa kusaidia kupata fedha za masharti nafuu, na ushirikiano kwa ajili ya kupanua upatikanaji wa nishati safi.

Rais Samia Suluhu Hassan tayari yuko Rio De Jenairo kushiriki katika mkutano huo wa kilele wa siku mbili na ushiriki wake unakuwa ni mara ya kwanza kwa Rais mwanamke kutoka Afrika kushiriki kwenye G20.

G20 pia inajulikana kama kundi la nchi ishirini ni jukwaa la kimataifa linalojumuisha nchi wanachama 19 pamoja na Umoja wa Ulaya, Umoja wa Afrika (AU).

Umoja wa Afrika unashiriki katika mkutano huo kama mwanachama kwa mara ya kwanza tangu kukubaliwa kama mwanachama wa kundi hilo mnamo Septemba 2023.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmoud Thabit Kombo, alisema mwishoni mwa kuwa Tanzania imepewa nafasi adhimu ya kukaa mezani na kundi ambalo linashikilia asilimia 75 ya biashara ya kimataifa na asilimia 85 ya pato la dunia.

“Huu ni ushuhuda wa kazi ya Rais wetu bila kuchoka katika azma yake ya kutoa njia za kuhamisha teknolojia na msaada wa kifedha kwa Tanzania na nchi nyingine za Afrika,” alisema waziri huyo katika taarifa yake.

Alisema ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo utasaidia juhudi za serikali katika mapambano dhidi ya umaskini na njaa pamoja na kufikia malengo ya maendeleo endelevu.

Waziri Kombo alisema ushiriki wa Rais Samia pia utaongeza mipango ya upishi safi na miundombinu mbadala muhimu kwa maisha endelevu.

Alisema mkutano huo utaipa Tanzania fursa ya kuvutia uwekezaji katika mipango ya usalama wa chakula kwa kukuza kilimo kinachozingatia hali ya hewa, kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi hususan kwenye mifumo ya chakula na kuimarisha ustahimilivu wa kikanda.

Waziri alisema ushiriki wa Rais Samia katika mkutano wa G20 unatarajiwa kuinua hadhi ya Watanzania katika ngazi ya dunia ili kukuza ushirikiano wa muda mrefu katika kufikia dira ya muda mrefu inayoendana na malengo ya maendeleo.

Alisema mkutano wa viongozi wa G20 utajadili vipaumbele vya maendeleo endelevu ambavyo ni ushirikishwaji wa kijamii na mapambano dhidi ya njaa na umaskini, mabadiliko ya nishati sambamba na kukuza maendeleo endelevu katika nyanja zote za kiuchumi, kijamii na kimazingira.

“Maeneo haya yanawiana vyema na vipaumbele vilivyomo katika Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Tanzania 2025 na Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2050,” alisema.

G20 inaundwa na Argentina, Australia, Brazili, Canada, China, Ufaransa, Ujerumani, India, Indonesia, Italia, Japan, Mexico, Urusi, Saudi Arabia, Afrika Kusini, Korea Kusini, Uturuki, Uingereza na Marekani.

Kundi hilo linaangalia ukuaji wa uchumi duniani, kushughulikia masuala muhimu ya kimataifa kama vile mabadiliko ya hali ya hewa, usalama wa nishati na maendeleo, na kukuza ushirikiano wa kimataifa katika masuala muhimu kama vile biashara, fedha na uwekezaji.

Mkutano wa 18 wa G20 mwaka 2023 ulifanyika New Delh India, mwaka 2022 ulifanyika kwenye mji wa Bali Indonesia, mwaka 2021 ulifanyika Roma Italia, mwaka 2020 ulifanyika Saudi Arabia.

Mwaka 2019 ulifanyika Osaka Japan, mwaka 2018 ulifanyika Buenos Aires Argentina, 2017 ulifanyika hamburg Ujerumani, mwaka 2016 Hangzough China, mwaka 2015 ulifanyika kwenye mji wa Antalya Uturuki.

Mwaka 2014 ulifanyika Australia, mwaka 2013 St Petersburg Urusi, mwaka 2012 Los Cabos Mexico, 2011 ulifanyika kwenye mji wa Cannes Ufaransa, mwaka 2010 ulifanyika mji wa Seoul Korea, mwaka 2009 mji wa Pittsburgh Marekani na mkutano wa kwanza ulifanyika Washingtom Marekani mwaka 2008.

Tanzania ilishiriki kwa mara ya kwanza katika mkutano wakati huo ukiitwa G8 kabla ya kundi la nchi hizo kuongezeka mwaka 2009 na ni Rais Benjamin Mkapa wakati huo ndiye wa kwanza kuhudhuria mkutano huo uliofanyika kwenye mji wa Gleneaagles Scotland mwaka 2005.

Rais wa awamu ya nne Jakaya Kikwete nayeye aliwahi kuhudhuria mkutano wa G 8 katika Mji wa Tokyo, Japan mwaka 2008.