January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Dkt. Samia alivyofanikiwa kuongeza kasi ya uwekezaji 2023

Na Mwandishi Wetu,TimesmajiraOnline,Dar

KASI ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, imeendelea kushangaza watu wengine zikiwemo taasisi za kimataifa.

Miongoni mwa taasisi hizo ni pamoja na Benki ya Dunia (WB) ambayo hivi karibuni imeweka wazi kwamba kasi ya ukaji wa uchumi wa Tanzania unazizidi nchi nyingi zinazoendelea hata wakati na baada ya janga la UVIKO-19.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa Benki ya Dunia nchini, Nathan Belete, ambapo kwa kuthibitisha hilo, anasema;

“Ukuaji uchumi Tanzania ni wa kustaajabisha, japo unahitaji kuwa wa haraka, bora, na jumuishi zaidi.

Matokeo ya ukuaji huo wa uchumi wa Tanzania unatokana na jitihada za Rais Samia ambazo amezichukua kwa takribani miaka miwili ambayo amekaa madarakani. Rais Samia alishika wadhifa huo Machi 19, 2021.

Mfano, TIC imesajili jumla ya miradi mipya ya uwekezaji 367 katika kipindi cha Januari-Septemba, 2023 iliyozalisha jumla ya ajira 116,701.

Uwekezaji wa moja kwa moja wa Nchi za Nje (FDI) nchini Tanzania umeongezeka karibu mara mbili kwa mwaka mmoja hadi kufikia dola bilioni 1.05 kati ya Julai na Septemba, 2023 ikilinganishwa na dola milioni 524.4 katika kipindi kama hicho mwaka 2022.

Pia chini ya uongozi wa Rais Samia, TIC imefanikiwa kusajili miradi 504 kwa mwaka 2023 yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 5.6 ambayo kukamilika kwake kutasaidia kuzalisha ajira 230,000.

Vile vile, Serikali imekipa Kituo hicho lengo la kusajili miradi yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 15 ambazo ni sawa na sh.trilioni 35 ifikapo mwaka 2025.

Rais Samia Suluhu Hassan akishiriki kwenye mkutano wa wafanyabiashara wanawake Afrika

Hiyo ni kwa mujibu wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Profesa Kitila Mkumbo, wakati akizungumza jijini Dar es Salaam wiki iliyopita.

Anasema kwenye miradi hiyo 504, asilimia 47 ni miradi ya Watanzania, asilimia 29 ni miradi ya watu wa nje na miradi 26 ni ya ubia baina ya wageni na wazawa.

“Nilipoteuliwa Julai mwaka jana nilitembelea taasisi nyingi ikiwemo TIC na niliwaambia kuwa kuna hisia kwamba tunapozungumzia uwekezaji tunamaanisha wa kutoka nje ya nchi, niliagiza kwamba lazima tufute dhana hiyo ndipo tukasema tuwe na kampeni maalum,” anasema Prof. Kitila

Profesa Mkumbo anasema kupitia utekelezaji wa Sera na Sheria, Serikali imeendelea kupata mafanikio mbalimbali katika kuhamasisha, kuvutia na kuwezesha uwekezaji nchini.

Aidha, anasema hivi Karibuni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amezindua rasmi kampeni ya kitaifa ya kuhamasisha uwekezaji kwa lengo la kutoa msukumo maalum kwa Watanzania kuchangamkia fursa za uwekezaji zilizoko nchini.

Kwa mujibu wa Prof. Kitila anasema kama sehemu ya utekelezaji wa kampeni hiyo, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji imeamua kuufanya mwaka 2024 kuwa mwaka wa kitaifa wa kuhamasisha uwekezaji nchini hasa kwa watanzania.

Anafafanua kwamba katika kutekeleza mpango huo, kuanzia Januari hadi Februari mwaka huu (2024) ofisi yake kwa kushirikiana na TIC wataendesha kampeni maalum nchi nzima kupitia vyombo mbalimbali vya habari.

Anasema baada ya kukamilika kwa kampeni ya vyombo vya habari, kampeni hiyo itaendelea kwa mwaka mzima kupitia semina na makongamano katika mikoa na wilaya zote nchini na kwamba itahitimishwa na kongamano la kitaifa la uwekezaji.

Anasema kampeni hiyo ina malengo saba mahsusi ya kutoa elimu ya uwekezaji kwa Watanzania ikiwemo kuondoa dhana kwamba uwekezaji ni kwa ajili ya wageni na kwamba ili uwekeze lazima uwe tajiri.

“Unajua huwezi kukuza uchumi au kuongeza ajira nchini bila uwekezaji mpya ndiyo maana tumewapa TIC malengo makubwa ya kusajili miradi ya Dola za Marekani bilioni 15 mwaka 2025 na bodi imeyakubali kwa hiyo menejimenti ya TIC ni kutekeleza na kuhakikisha tunayafikia,” anasema

Anasema kampeni hiyo itasaidia kuwaelimisha wananchi kuhusu taratibu za kusajili miradi ya uwekezaji kupitia TIC na kuwaeleza kuhusu vivutio mbalimbali vya kikodi na visivyo vya kikodi.

Anasema vivutio hivyo vinatolewa kwa wawekezaji wa ndani na nje wanaposajili miradi kupitia TIC lakini uzoefu umoenesha kwamba Watanzania wengi hawavijui.

Anasema kwenye kampeni hiyo pia wataonesha mafanikio ambayo Watanzania wameyapata na kuonesha fursa zilizopo pamoja na kupokea changamoto zinazowakabili Watanzania kwenye uwekezaji na kuzitatua.

Profesa Mkumbo alisema kampeni hiyo itatumika kukuza ushirikiano na wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa mamlaka za serikali za mitaa na viongozi wa sekta binafsi ili watumie fursa za uwekezaji kwenye maeneo yao.

Profesa Mkumbo anasema malengo mahsusi ya serikali katika kuhamasisha, kuvutia na kuwezesha uwekezaji ni kuvutia mitaji na teknolojia mpya nchini kutoka mataifa mengine yaliyopiga hatua kiteknolojia.

“Matokeo ya uwekezaji katika nchi hujitokeza katika kuongeza ajira, kuongeza mapato ya kodi, kupunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje na kuongeza mauzo ya bidhaa zilizoongezwa thamani nje ya nchi kwa ujumla uwekezaji ni nyenzo muhimu katika kukuza uchumi na kuleta maendeleo,” alisema Prof. Mkumbo.

Kwa upande wake mmoja wa wawekezaji kutoka China akizungumza kwa sharti la jina kutochapishwa gazetini, anapongeza juhudi za Serikali ya Rais Samia, ambazo zimeleta utulivu kwa wawekezaji, hivyo kufanya wawezaji wengi kuja kuwekeza nchini.

Anasema uwekezaji ni bidhaa yenye aibu sana, inaona aibu kuwepo mahali ambapo siyo sahihi, jambo ambalo halipo sasa kwa Tanzania.

“Kama mazingira ya biashara siyo ya rafiki, wawekezaji wapya wanaogopa kuja, bado hata wale waliopo watakuwa wakitamani kuondoka.

Nchi yoyote ikitengeneza mazingira ya biashara yasiyokuwa rafiki, wawekezaji wapya ni lazima wataogopa kuja na waliopo watakuwa hawana uhakika na biashara zao, kwani wanakuwa hawaelewi kesho yake itakuwaje,” anasema.

Anapongeza Serikali ya Rais Samia, kwa kuwa mstari wa mbele kuboresha mazingira ya uwekezaji, ambapo kwa sasa nchi nchi inazidi kupata wawekezaji wapya na wale waliopo wakiridhishwa na utulivu wa mazingira ya uwekezaji nchi.

“Serikali ya Rais Samia imekuwa mstari wa mbele kuondoa vikwazo vya kibiashara na yale mazuri kwa wawekezaji ikiendelea kuyakumbatia.

Ndiyo maana hata sisi tukirudi nyumbani iwe ni kwa mapumziko tunakuwa na uhakika kwamba mitaji hiyo ipo eneo sahihi,”anasema na kuongeza;

“Kwa kufanya hivyo tumeshuhudia uchumi wa Tanzania ukiendelea kukua vizuri tangu Rais Samia aliposhika wadhifa huo, Kwa ukuaji wa uchumi huo tija inaonekana pande zote mbili.”

Aidha, dhamira ya Rais Samia, kuifungua Tanzania na kuwa kivutio cha kufanyabiashara na uwekezaji, imechangia kufuta na kupunguza tozo, ada na faini zisizopungua 232 kati ya 380 zilizobainishwa katika utekelezaji wake sawa na asilimia 61.

Hatua hiyo imefikiwa na Serikali kupitia Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara (MKUMBI).

Akizungumza katika Kikao Maalum cha Kikundi Kazi cha Mazingira ya Biashara jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera na Uratibu wa Bunge, Dkt. Jim Yonazi, anasema tozo, ada na faini hizo zilikuwa kero kubwa kwa ustawi, ukuaji na maendeleo ya biashara na uwekezaji hapa nchini.

“Maamuzi haya yanaonesha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia ya kuifungua Tanzania na kuwa kivutio cha kufanya biashara na uwekezaji,” anasema Dkt. Yonazi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kikundi kazi hicho cha Baraza la Taifa la Biashara(TNBC).

Akielezea zaidi mafanikio yaliyopatikana tangu MKUMBI uanze kutekelezwa, Dkt. Yonazi anasema jumla ya Sheria, Kanuni na Taratibu zipatazo 40 kati ya 88 sawa na asilimia 45.5 zimeshapitiwa na kufanyiwa marekebisho.

“Maboresho haya yote ya Sheria, Kanuni na Taratibu yamesaidia kuchochea ukuaji wa sekta za uchumi hapa nchini zikiwemo sekta za uwekezaji, viwanda na biashara, kilimo, mifugo, afya, maliasili na utalii,” anasema.

Dkt. Yonazi anasema Rais Samia ambaye pia ni Mwenyekiti wa TNBC ameelekeza kuendelea kusimamia utekelezaji stahiki wa MKUMBI sambamba na uhamasishaji wa matumizi ya mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa lengo la kuongeza ufanisi kwa wafanyabiashara na wawekezaji hapa nchini.

Aidha, ukuaji wa uchumi chini ya uongozi wa Rais Samia, unathibitishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uwekezaji) Prof. Kitila, akisema kiongozi huyo amefunguka nchi kwa kuboresha miundombinu ikiwemo kuboresha bandari, viwanja vya ndege, barabara, reli, umeme na maji ili kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Anasema Rais Samia anafanya hivyo kwa sababu ili nchi iweze kuwa na uchumi imara na endelevu ni lazima Sekta Binafsi iwe na nguvu.

Profesa Kitila, alitoka kauli hiyo wakati akifungua Kongamano la Uwekezaji, Biashara na Utalii, na Uzinduzi wa Mwongozo wa Uwekezaji wa Mkoa wa Tanga.

“Rais Dkt. Samia alipokuwa Nairobi alisema nakwenda kuifungua nchi. Watu wengi hawakumuelewa, lakini aliposema kufungua nchi ni kuimarisha uchumi kwa kuimarisha Sekta Binafsi na kuwavutia wawekezaji.

Serikali haifanyi biashara wala kuajiri watu. Kazi ya kufanya biashara ama kuajiri watu ni ya Sekta Binafsi ikiwemo wawekezaji.

Hivyo, Serikali haitengenezi ajira, bali inaweka mazingira mazuri ya kufanya biashara na uwekezaji,” anasema Prof. Kitila.

Anasema katika ajira 100 Tanzania, ajira 95 zinatolewa na Sekta Binafsi, na Serikali inatoa ajira tano tu.

“Na ili kuvutia uwekezaji katika Sekta Binafsi, kazi ya Serikali ni kujenga miundombinu na mazingira wezeshi, na kazi hiyo imefanywa na Rais Dkt. Samia kwa kujenga miundombinu ya bandari, barabara, umeme, upatikanaji wa maji, na uboreshaji huduma za jamii,” anasema Profesa Mkumbo.

Profesa Mkumbo anasema tangu nchi ipate Uhuru mwaka 1961, maadui watatu wa Taifa walikuwa ujinga, maradhi na umasikini, lakini maadui wa sasa ni watu wanaokwamisha uchumi wa Tanzania kukua kwa kuwawekea vikwazo vingi wawekezaji.

“Moja ya vikwazo vitatu vya uchumi ni udhibiti uliopitiliza kwenye uwekezaji. Na Rais Dkt. Samia anataka kubomoa mnyororo unaokwanza Sekta Binafsi.

Lugha sasa sio kudhibiti bali kuwezesha. Afisa Biashara ukimkuta mfanyabiashara hana leseni, afanyekazi ya kumsaidia apate leseni. Afisa Biashara anayetutia umasikini ni yule anayemkuta mfanyabiashara ambaye hana leseni na kumueleza leo utanikoma, funga biashara yako.

“Askari wa usalama barabarani wanaosimamisha malori nchi nzima kila mahali, wanatutia umasikini. Hata sisi mawaziri tuna suti nzuri na magari mazuri ni sababu wafanyabiashara wanalipa kodi.
Hata askari anaposimamisha lori, ajue nguvu ya kuinua mkono anaipata sababu ya kodi ya wafanyabiashara, hivyo tuondoe urasimu kwa wafanyabiashara na wawekezaji,” anasema Prof. Kitila.

Kwa kutambua umuhimu huo wa wawekeaji, ndiyo maana Serikali ya Rais Samia ilianzisha Kikosi Kazi cha Mazingira ya Biashara.

Katibu Mtendaji wa TNBC Dkt. Godwill Wanga, anasema Kikosi Kazi cha Mazingira ya Biashara kina jukumu kubwa la kuhakikisha mazingira ya kufanya biashara yanaendelea kuwa rafiki kwa biashara, uwekezaji na uchumi kwa ujumla na kuvutia uwekezaji kujenga uchumi wan chi.

“Kikundi kazi hiki kina jukumu kubwa la kuondoa na kupunguza gharama za kufanya biashara na uwekezaji. Hivi hatuna budi kufanya kazi kwa bidii na kuhakikisha tunajiandaa kuwakilisha mapendekezo yenye tija kwa Baraza,” anasema Dkt. Wanga.

Anasema TNBC hufanya kazi kupitia mikutano na vikao katika ngazi mbalimbali kama vile ya Baraza, Kamati Tendaji za Baraza, Mashauriano ya Kiwizara kati ya Sekta Binafsi na Umma (MPPD), Kikosi Kazi cha Kiufundi cha Kiwizara(MTWG), Mikutano ya Baraza la Biashara ngazi ya Mkoa (RBC) na Wilaya (DBC).

Kwa upande wake Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, anapongeza jitihada zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia, kukuza uwekezaji nchini.

Kikwete ametoa pongeza hizo juzi jijini Dodoma kwenye Mkutano wa Nne wa Maendeleo ya Biashara na Uchumi uliofanyika katika Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE).

“Hayo ndiyo tulikuwa tunasema kama mazingira ni rafiki wale wasiokuwepo wanatamani kuja, lakini mazingira kama sio rafiki wanaogopa kuja na waliopo wanatafuta namna ya kutoka, hawaongezeki zaidi ya pale,” alisema Kikwete na kuongeza;

“Wale wanaokuja wanauliza wamebadilika kweli wale! Ebu ngoja tuone, tupime upepo.”

Anasema kwao (kama yeye Kikwete) wanaozunguka duniani, wanaona wawekezaji wanajiamini kuja kuwekeza nchini, wanasema tunapenda kuja kuwekeza Tanzania, tunawaambia njoo.”