January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Dkt.Samia akemea vitendo vya mauaji ya watoto

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

RAIS Dkt.Samia Suluhu Hassan (Chifu Hangaya)amekemea vitendo vya utekaji na mauaji ya watoto kwa imani potofu za ushirikina ambayo ni kinyume cha maadili ya Watanzania.

Amekemea vitendo hivyo jijini hapa leo,Julai 20,2024 wakati akizungumza na viongozi wa Kimila na Machifu kutoka Tanzania nzima kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino ambapo aliwasihi Machifu na wananchi wote kukemea vitendo hivyo.

Amesema Machifu huwa na heshima katika jamii zao na wanaweza kutoa mwongozo kwa vijana na wanajamii wao kuhusu maadili na mila za kabila hivyo ni muhimu kukemea vitendo vya utekaji pamoja na mauji ya watoto wakiwemo watu wenye ualibino hivi sasa vimeibuka kwa wingi katika maeneo mengi ya nchi hali ambayo inapaswa kukemewa na kuchukuliwa hatua kali.

“Hivi sasa vitendo vya utekaji pamoja na mauaji ya watoto vimekuwa vikiripotiwa kila siku na namna vinavyoripotiwa serikali ndiyo inalaumiwa sana wakati kule yanakotokea mambo haya viongozi wa chini wapo,viongozi wa mitaa wapo lakini hata machifu wapo wamekaa kimya.

“Nawaombeni muende mkayakemee mambo haya kwani yanatokea huko kwenye jamii zetu na yanachafua taswira ya taifa letu lenye sifa nje leo hii watu wakisikia mtu katekwa ama mtoto kuuwawa siyo picha nzuri na kama kunawageni wanayaleta muwakatae,

“Mambo ya mauaji ya alibino yalishapotea kabisa lakini sasa yanarudi kwa kasi na ukiuliza watu wanadai ni uchaguzi lakini uongozi anatoa Mungu siyo kwa kuuwa mtu unaweza ukaua hata watu 10 na uongozi usipate”amesema Dkt.Samia.

Aidha Dkt Samia ameilekeza Wizara ya Utamaduni,Sanaa na Michezo kukamilisha mwongozo wa utambuzi wa Machifu na viongozi wa kimila katika Wilaya na Mkoa utakaoainisha majukumu yao ya kimila na kijadi.

“Viongozi wa kimila na machifu mnamchango mkubwa katika kulinda maadili na kutatua changamoto za kimaadili katika jamii licha ya kuwa yanashughulikiwa katika ngazi ya serikali,”amesema.

Vilevile,Rais Dkt.Samia ameitaka Wizara hiyo kuimarisha michezo ya umoja wa Michezo ya shule za msingi na sekondari (UMISETA na UMITASHUMTA)ikiwa ni sehemu ya kuwafundisha na kudumisha mila na desturi zetu.

“Dunia inaposhuhudia mabadiliko mbalimbali,Serikali ya Tanzania itahakikisha kuwa inashuhudia maendeleo ambayo yanadumisha mila na desturi za watanzania,”amesema Rais Dkt.Samia.