Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
RAIS wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuongoza Mkutano wa 15 wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) utakaofanyika Ikulu Jijini Dar es Salam kesho
Akizungumzia mkutano huo muhimu wa baraza hilo jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mtendaji wa TNBC, Dkt. Godwill Wanga amesema mkutano huo unalenga kuangazia mazingira bora ya ufanyaji biashara na uwekezaji kupitia Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara (MKUMBI).
“Kupitia mkutano huu, tunaenda kufanya tathimini ya mambo yote ambayo yamekuwa ni kikwazo katika kufanikisha ufanyaji biashara na uwekezaji nchini sambamba na kuja na mapendekezo ya nini kifanyike ili kuchochea matokeo chanya katika kukuza na kuboresha biashara nchini,” alisema Dkt Wanga
Aidha, Dkt Wanga alisema mkutano huu utapitia ajenda za mkutano wa 14 na kuangalia ni jinsi gani mapendekezo hayo yaliyo tolewa na wajumbe katika mkutano huo yalivyotekelezwa.
Lakini pia, mkutano huo utajadili juu ya changamoto ambazo hazikuweza kutatuliwa sambamba na kuja na mapendekezo yatakayo chagiza kasi ya maendeleo.
Kwa mujibu wa Dkt Wanga, katika mkutano uliopita, wajumbe wa mkutano walitoa mapendekezo yao katika maeneo ambayo waliona yanakwamisha mazingira ya biashara na Rais Samia akatoa maelekezo kwa watendaji husika kuzitatua changamoto hizo.
Hivyo, alisema katika mkutano huu wataona wapi palikuwa na ugumu na nini kifanyike ili kuondoa kero au changamoto hizo.
Dkt. Wanga aliongeza kuwa katika mkutano huu, miongoni mwa mambo mengi yatakayojadiliwa ni pamoja na ushiriki wa wananchi katika miradi ya kimkakati, ambapo mkutano utajadili ni kwa namna gani wananchi wanapewa kipaumbele katika utekelezaji wa miradi hiyo.
Hata hivyo mkutano utajadili juu ya mapinduzi ya uchumi wa kidigitali (Tehama) ambapo wanachi wengi watakuwa wanufaika kwani kupitia mfumo huu wataweza kufikia kundi kubwa la wananchi ambao kwa sasa imekuwa ngumu kulifiikia kwa wakati stahiki.
Rais Dkt. Samia alikuwa akisisitiza kufanya kazi pamoja kwa mifumo ya taasisi zote za Serikali, ili kuhakikisha huduma zote stahiki zinawafikia mwananchi kwa wakati kupitia mfumo wa kidigitali ambao utarahisisha utoaji huduma sambamba na kuvutia uwekezaji nchini,” alisema Dkt. Wanga
Alisema katika mkutano huu, pia watajadili namna Mkumbi unavyolenga kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji nchini kwa kupunguza au kuondoa na kuboresha changamoto mbalimbali zinazokumba ufanyaji biashara nchini.
TNBC kimekuwa ni chombo muhimu cha majadiliano kati ya sekta ya umma na binafsi katika kufikia mwafaka wa masuala ya kijamii na kiuchumi kwa ajili ya mustakabali wa ustawi na maendeleo endelevu ya Taifa.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakani
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best