Judith Ferdinand, Mwanza
Shirika la Railway Children Afrika(RCA) limesema litaendelea kushirikiana na serikali katika kukabiliana na wimbi la watoto wa mitaani sambamba na kuhakikisha wanawaunganisha watoto hao na familia zao.
Meneja Mradi wa shirika hilo mkoani Mwanza Irene Wampemba, ameeleza kuwa pia wanalenga kuimarisha mifumo ya ustawi wa jamii ambayo itawezesha kuendelea kuwatambua watoto wanaoishi mitaani kwa idadi hadi sasa shirika hilo limeendelea kuwawezesha Maofisa Ustawi wa Jamii wa Ilemela kuunganisha watoto na familia zao.
Irene ameeleza hayo wakati wawakikishi wa shirika hilo akiwemo yeye walipomtembelea Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Hassan Masala ofisini kwake kwa ajili ya kutoa taarifa na mwendelezo wa shughuli wanazofanya katika kukabiliana na ongezeko la watoto wa mitaani.
Ofisa Utekelezaji wa Shirika hilo Dionis Shimbi ameahidi kuendeleza ushirikiano na serikali pamoja na wadau wengine ili kuweza kufanikisha malengo yao.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Hassan Masala amewaahidi ushirikiano wa kutosha na kuwa iwapo zipo changamoto zozote zinazowakabili katika utekelezaji wa malengo yao basi wasisite kumshirikisha ili kuwez kupata ufumbuzi.
Sanjari na hayo Masala amemuagiza Ofisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kuhakikisha anawasilisha mpango kazi ikiwa ni pamoja na kuyaalika mashirika yasiyo ya kiserikali ili kuweza kukutana na kuzijadili changamoto mbalimbali katika jamii hususani masuala ya ukatili.
Naye Ofisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Pamela Kijazi, amewahakikishia kuwa wataendelea kushirikiana kikamilifu katika kuwatambua watoto wanaishi na kufanya kazi mtaani na kuwaunganisha na familia zao.
More Stories
TASHICO,yatoa ufafanuzi Mv.Serengeti kutitia upande mmoja
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua