October 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Raia Kenya, Tanzania waburutwa Mahakamani kwa uhujumu uchumi

Na Grace Gurisha TimesMajira Online

RAIA wawili wa Tanzania na wawili kutona nchini Kenya, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi ikiwemo kuisababisha Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), hasara ya Sh milioni 16.6.

Washitakiwa hao ni Beth Ngunyi (43) mfanyabiashara na Mkazi wa Kasaram Nairobi, Frolence Dirango (34)  mfanyakazi wa Kampuni  ya Betlee kama Ofisa wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Alven Swai (26) mkazi wa Mbezi Beach na Godluck  Macha (28) mfanyabiashara na Mkazi wa Mbezi beach.

Akisoma hati ya mashtaka, Wakili wa Serikali, Batilda Mushi akisaidiana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Saimon amedai leo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Yusto Ruboroga kuwa kati ya Julai  Mosi na Julai 26, mwaka huu katika  maeneo mbalimbali, washitakiwa kwa pamoja walikula njama ya kutumia vifaa vya mawasiliano.

Mushi amedai, Julai 13, mwaka huu maeneo ya Tarakea Wilayani Rombo Mkoani Kilimanjaro, Ngunyi na Dirangu waliingiza vifaa vya kielekroniki nchini pasipo kuwa na leseni ya TCRA.

Pia Julai 20, mwaka huu maeneo Kibona Lodge Mbezi Beach jijini  Dar es Salaam, washitakiwa hao walisimika vifaa vya mawasiliano bila kuwa na leseni  kutoka TCRA.

Wakili huyo, amedai kuwa katika shtaka ya nne, imedaiwa kati ya Julai 20 na 26, 2020 maeneo ya Kibona lodge Mbezi beach, kinyume  na sheria walifanyia marekebisho ya vifaa hivyo vya kielektroniki huku wakiendesha mitambo ya mawasiliano bila kuwa na leseni ya TCRA.

Mushi amedai, kinyume na sheria washitakiwa hao walitumia vifaa vya mawasiliano vilivyounganishwa na vifaa vingine vya mawasiliano kwa nia ya kupokea na kusambaza mawasiliano bila kupata uthibitisho wa TCRA.

Washitakiwa hao wanadaiwa walikwepa kufanya malipo ambayo yalipaswa kufanyika kwa kuruhusu mawasiliano nje ya nchi kutokana na kutumia kifaa hicho cha mawasiliano bila kuwa na leseni.

Katika mashitaka  ya tisa, imedaiwa Julai 13, mwaka huu maeneo ya Kibona Lodge, Mbezi beach, washitakiwa Ngunyi na Dirangu kuwepo nchini bila kuwa na kibali.

Mshitakiwa  Macha anadaiwa Julai 15, mwaka huu kinyume na sheria aliwahifadhi Ngunyi na Dirangu kuishi kwenye Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  wakati wakijua hawana kibali.

Katika mashitaka ya 11, imedaiwa kati ya Julai 20 na 26, mwaka huu maeneo ya Kibona Lodge Mbezi beach jijini Dar es Salaam washitakiwa hao waliisababishia TCRA hasara ya Sh 16,634,400.

Washitakiwa  hao hawakutakiwa kujibu chochote  kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu  uchumi huku Wankyo, akidai kuwa upelelezi  wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuomba tarehe nyingine  kwa ajili ya kutajwa.

Baada ya maelezo hayo, Hakimu Ruboroga aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 20 mwaka huu kwa ajili ya kutajwa na washitakiwa  wote wamerudishwa rumande  kwa sababu mashitaka  hayo hayana dhamana.