December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Qwihaya yazishika mkono kaya zaidi ya 50,nyumba zao zilizoathiriwa na mvua Ilemela

Na.Daud Magesa, Timesmajira Online,Mwanza

KAYA zaidi ya 50 zilizoachwa bila makazi wilayani Ilemela baada ya mvua zilizonyesha zikiambatana na upepo mkali, kubomoa na kuezua nyumba zao zimekabidhiwa mbao 2200 zenye thamani ya milioni 13.2.

Mvua hizo zilizonyesha Septemba 6, mwaka huu, zikiambatana na upepo mkali zilisababisha baadhi ya nyumba kubomoka na kuanguka huku zingine zikiezuliwa mapaa na hivyo kuziacha kaya hizo kubaki bila makazi ya kuishi.

Wakazi wa Mtaa wa Buganda, Kata ya Shibula, Foibe Kipese (kulia) na Kurwa Samwel , kushoto wakitabasamu baada ya kupokea msaada wa mbao kutoka kampuni ya Qwihaya General Enterprises, baada ya nyumba zao kuezuliwa na upepo na zingine kubomoka kutokana na mvua.

Akikabidhi msaada huo wa mbao 1100 kati ya 2200 kwa kaya 29 za Mtaa wa Buganda,Kata ya Shibula,Mkurugenzi wa Kampuni ya Qwihaya General Enterprises Ltd, Benedicto Mahenda, amesema zitazisaidia kurekebisha na kuboresha makazi yao na kurejea katika hali ya zamani.

“Kampuni ya Qwihaya kupitia vyombo vya habari iliguswa na tatizo lililowapata,kuona watoto wadogo,wazee na wanawake wakitaabika na kulala nje kwa kukosa makazi,hivyo kidogo hiki kipokeeni mkitumie kuboresha makazi yenu muendelee na maisha kama awali na kushiriki shughuli za uzalishaji na maendeleo,”amesema.

Diwani wa kata ya Shibula (CCM) Dede Swila akiwaeleza jambo wananchi wa Mtaa wa Buganda ambao walikumbwa na maafa ya nyumba zao kubomoka na kuezuliwa mapaa kwa upepo kabla ya kupokea msaada wa vifaa vya ujenzi vilivyotolewa na kampuni ya Qwihaya General Entrprises.

Msemaji wa kampuni hiyo,James Steven amesema washukuru kupokea hicho kidogo kwani kadhia hiyo si kwa kaya za Mtaa wa Buganda pekee,imezikumba pia kaya za Kata ya Ilemela,hivyo hawatatenda haki wasipowashika mkono kwa kuwapatia msaada wa vifaa vya ujenzi.

Mkurugenzi wa Qwihaya General Enterprises, Benedicto Mahenda, akizungumza na wananchi wa Buganda ambao nyumba zao zilibomoka na zingine kuezuliwa na upepo katika Wilaya ya Ilemela

Mratibu wa Maafa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,Jamses Wembe,amewataka wananchi kuchukua tahadhari huku akisema kuwa Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) imetahadharisha kunyesha mvua zikiambatana na upepo mkali ndani ya siku tano.

“Serikali haiwezi kuzuia majanga na TMA imetahadhari upepo mkali utavuma ndani ya siku tano ukiambatana na mvua katika ukanda wa Ziwa Victoria,hivyo wavuvi na wamiliki wa vyombo vya usafiri wa majini wazingatie hilo kuepuka athari zinazoweza kujitokeza,”amesema Wembe.

Baadhi ya wahanga wameishukuru kampuni ya Qwihaya kwa msaada huo wa vifaa vya ujenzi ikiwemo Serikali ya awamu ya sita kwa uratibu uliowezesha wadau hao kuwasaidia na kuomba wengine watakaoguswa wawasaidie saruji,misumari na mabati.

Regina Chrisant Mkazi wa Mtaa wa Buganda, Kata ya Shibula, ameishukuru kampuni hiyo ya Qwihaya kwa uzalendo,upendo na ubinadamu kwani siku mvua inanyesha huku upepo mkali ukivuma ilikuwa patashika na kuahidi watautumia vyema msaada huo kuboresha makazi yao na kuweza kushiriki shughuli za maendeleo na uzalishaji.

Aidha Stanslaus Francis mbali na kushukuru kampuni hiyo amemshukuru Mungu kuwa hakuna vifo vilivyosababishwa na mvua hiyo zaidi ya nyumba kubomoka na kuezuliwa mapaa,ingawa ajali ni ajali na maumivu yanatofautiana,hivyo wanafarijika na hakuna kunung’unika kwani hawakuwa na fedha za kurejesha nyumba zao katika hali ya zamani.

Moja ya nyumba iliyoezuliwa sehemu ya paa kwa upepo Septemba 6, mwaka huu, katika Mtaa wa Buganda invyoonekana.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtaa wa Buganda,Kata ya Shibula,Evarist Chikanga,amesema serikali haiwezi kutoa fedha mkononi inatoa vitu, hivyo kupitia wadau msaada ulitolewa kwa wananchi wa kata hizo mbili si kidogo na haufungamani na siasa,vyama vya siasa,dini,kabila wala makampuni binafsi.

“Siku ya tukio hatukulala wakiwemo viongozi,walihaingaika kuhakikisha tunakaa salama licha ya kukosa makazi,tunawashukuru Qwihaya kwa msaada wa mbao, tatizo kubwa ni mabati, hivyo wengine watakaoguswa watusaidie mabati ama saruji,”amesema Abubakar Nzumbi, mkazi wa Mtaa wa Bulyele, Kata ya Ilemela.

Madiwani wa kata za Shibula na Ilemela (wote CCM),Swila Dede na Wilbroad Kilenzi kwa nyakati tofauti wamewashukuru wadau hao (Qwihaya General Enterprises) kwa msaada huo wa kijamii.

“Mahitaji bado ni makubwa nyumba zimebomoka na kuanguka kabisa, watakaoguswa watusaidie saruji na mabati ambapo mbao hizi 1,100 kaya 16 zilizoathirika zaidi zitapata mbao zisizopungua 40 na zilizobaki 13 zitapata mbao 30,”amesema Dede na kuwataka wananchi kupanda miti kuzuia na kujikinga na upepo.

Kilenzi yeye amesema milango iko wazi kwa wadau wengine kusaidia waathirika hao lakini msaada huo usitafsiriwe kisiasa kwani hakuna siasa katika majanga,alitaka tathmini ifanyike kwa uadilifu na hofu ya Mungu ili walioathirika zaidi wapate kikubwa.