July 3, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Qatar, Iran zaijadili Afghanistan

TEHRAN, DOHA-Mawaziri wa Mambo ya Ndani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran,Muhammad Javad Zarif na Qatar, Muhammad binj Abdul-Rahman bin Jassem Aal Thani wamejadili katika mazungumzo yao kwa njia ya simu matukio ya hivi karibuni nchini Afghanistan.

Dkt.Zarif na Thani walifanya mazungumzo hayo mwishoni mwa wiki kwa njia ya simu ambapo mbali na kujadili matukio ya hivi karibuni nchini Afghanistan walibadilishana mawazo pia kuhusiana na juhudi za Tehran za kuhakikisha inapatikana serikali jumuishi katika nchi hiyo.

Mazungumzo hayo yalifanyika baada ya yale ya Rais Hassan Rouhani wa Iran na Amir wa Qatar Sheikh Tamim bin Hammad Aal Thani.

Rais Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema katika mazungumzo hayo kwa njia ya simu na Amir wa Qatar kwamba, Iran inafuatilia kwa karibu nyendo za Marekani na kuongeza kuwa: “Iran kamwe haitakuwa muanzishaji wa taharuki na mapigano katika eneo”.

Aidha, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Amiri wa Qatar walisema, uhusiano wa Tehran na Doha ni chanya na unazidi kuimarika na walisisitiza kuhusu udharura wa kuimarisha uhusiano wa pande mbili katika nyanja zote.

Viongozi wa Qatar wamekuwa wakisisitiza mara kwa mara kwamba, kamwe hawatazisahau nchi kama Iran iliyoisaidia nchi hiyo katika kipindi cha vikwazo na mashinikizo.

Juni 5, 2017, Saudi Arabia iliongoza nchi nyingine za Kiarabu ikiwemo Misri, Emirates na Bahrain kuiwekea vikwazo vya angani, baharini na ardhini nchi ya Qatar na kukata kabisa uhusiano wao na Doha.