Na Mwandishi Wetu,TimesMajiraOnline,DSM
KAMPUNI ya PZG-PR ilitangazwa kushinda tuzo ya ‘Best PR Agency 2024’ nchini Tanzania katika Tuzo za Umahiri wa Mawasiliano na Uhusiano wa Umma Mwaka 2024, zilizofanyika Dar es Salaam na kuandaliwa na Public Relations Society of Tanzania (PRST).
Tuzo hii ni mara ya kwanza kwa PZG-PR kuipata, ikiwa ni mafanikio makubwa kwa kampuni hii ambayo imekuwa ikitoa huduma za ushauri wa kitaalamu katika mawasiliano ya kimkakati kwa zaidi ya miaka mitano. PZG-PR imejijengea jina kubwa kutokana na ubunifu wake na dhamira yake ya dhati katika kuboresha sekta ya mawasiliano na uhusiano wa umma hapa nchini Tanzania.
Ikiongozwa na Afisa Mtendaji Mkuu, Prudence Zoe Glorious, PZG-PR imefanikiwa kujijengea sifa ya kutoa huduma bora za uhusiano wa umma, na imekuwa kinara katika sekta ya mawasiliano katika kanda ya Afrika Mashariki. Katika kipindi chote cha miaka mitano, kampuni hii imejizolea mafanikio makubwa na sifa nzuri kwa kubuni na kutekeleza mikakati mbalimbali ya mawasiliano.
PZG-PR imekuwa na wateja maarufu na wa kimataifa, ikiwa ni pamoja na UNICEF Tanzania, Ubalozi wa Denmark nchini Tanzania, Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Mitaji (UNCDF), Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), Shirika la Ndege la Jambojet, IYF & MasterCard Foundation, Aga Khan Foundation, Segal Family Foundation, Benki ya Stanbic Tanzania, Taasisi ya Jakaya Mrisho Kikwete, na AGRA.
Akizungumza kuhusu tuzo hiyo, Prudence Zoe Glorious, alisema, “Tuzo hii inatufundisha kuendelea na jitihada zetu za kujitahidi zaidi, kujifunza zaidi, kuwa wabunifu zaidi ili kufikia viwango bora zaidi. Sio tu katika mikakati na ubunifu, bali pia kama kampuni inayokuza fikra na maarifa zaidi. Tunamshukuru Mungu, timu yetu ya wafanyakazi, washauri wetu wataalam, walezi wetu, watu wanaojitolea, wateja, na wote waliotuunga mkono katika mafanikio haya.”
Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, PZG-PR imeweza kutekeleza kampeni na matukio makubwa ya kihistoria kama vile uzinduzi wa hati fungani ya kwanza ya kijani (Tanga Water Green Bond) katika Ukanda wa Afrika Mashariki, Uratibu na Usimamizi wa Wiki ya AZAKI 2024, na uzinduzi wa safari ya kwanza ya Jambojet kati ya Zanzibar na Mombasa.
Tuzo hii inaonesha mafanikio ya kampuni ya PZG-PR katika kuboresha na kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya mawasiliano na uhusiano wa umma, na inathibitisha juhudi na ubunifu wake unaoendelea kuboresha mazingira ya kibiashara na kijamii nchini Tanzania.


More Stories
Dkt.Mpango ashiriki dua,kumbukizi miaka 53 ya Hayati Karume
Wasira:Ilala kuna watu wameanza kampeni
TASAF yafanikiwa kupunguza kiwango cha umaskini kwa walengwa