Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online
MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Charles Sangweni, ameiomba Serikali kuweka muongozo wa uwajibikaji wa mamlaka hiyo kwa jamii, utakao wezesha utekelezaji wa miradi ya kurejesha huduma kwa jamii(CSR) inayofanywa na kampuni za utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia.
Sangweni ameyasema hayo Jana katika kikao kilichowahusisha wajumbe mbalimbali akiwemo, Katibu Tawala Wilaya ya Mtwara, Wakurugenzi wa Halmashauri za Manispaa ya Mtwara Mjini na Vijijini na wataalamu kutoka PURA kilichofanyika katika ofisi za Mkuu wa Wilaya hiyo.
Ameeleza kuwa, chimbuko la kuandaliwa kwa muongozo wa uwajibikaji wa kampuni kwa jamii ni kifungu namba 222(4) Cha sheria ya petroli ya mwaka 2015, ambapo amedai kuwa hivi sasa ni wakati muafaka wa kuweka muongozo, utakaowezesha utekelezaji wa miradi ya CSR inayozingatia mahitaji na vipaumbele kwa jamii.
“Sisi kama PURA wakati mwingine tunapozunguka kukagua utekelezaji wa miradi ya CSR na kuhoji uongozi wa jamii husika kama ulishirikishwa katika kupanga aina ya mradi wa kutekeleza tunakuta kwamba baadhi ya miradi tunakuta haikuzingatia vipaumbele vya jamii husika, hali inayopelekea mradi kutelekezwa au kutotumiwa kabisa kulingana na matarajio,”ameeleza Sangweni.
Aidha kwa upande wake Mkuu wa Wilaya hiyo, Hanafi Msabaha ameipongeza PURA na kudai kuwa muongozo ni muhimu.
“Ombi langu kwenu ni kwamba, muongozo huo ujumuishe namna ya kukokotoa kiasi ambacho kampuni zitatakiwa kuchangia katika miradi ya CSR kwa sasa hakuna fomula maalumu ya kukokotoa kila kampuni ichangie vipi kulingana na faida inayotengeneza au ukubwa wa uwekezaji,”ameeleza Msabaha.
Pia ameomba kuwepo kwa muongozo mmoja kwa sekta zote kwani mradi wa CSR siyo kwenye sekta ya mafuta na gesi asilia pekee.
More Stories
Mwanasiasa mkongwe afariki Dunia
Rais Samia Kuzindua Sera Mpya ya Elimu na Mafunzo
Jokate awapa tano vijana UVCCM maandalizi Mkutano Mkuu wa CCM