Na Joyce Kasiki,Timesmajira online, Dodoma
MAMLAKA ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imewataka Watanzania kuchangamkia fursa zilizopo katika sekta ya mafuta na gesi asilia, hasa katika mkondo wa juu wa petroli, ikisisitiza umuhimu wa ushiriki wa wazawa katika maendeleo ya rasilimali hizo za taifa.
Kupitia ushiriki wake katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea jijini Dodoma, PURA imekuwa ikitoa elimu kwa wananchi kuhusu majukumu yake, nafasi za ajira, ujasiriamali na uwekezaji unaopatikana ndani ya sekta hiyo muhimu ya kiuchumi.
Akizungumza katika banda la PURA leo Juni 17,2025 Mkuu wa Kitengo cha Ushirikishwaji wa Wazawa na Ushirikiano wa Ndani, Bw. Charles Nyangi, meisema kuwa mamlaka hiyo ilianzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Petroli ya mwaka 2015 ili kusimamia shughuli zote za utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia nchini.
“Moja ya kazi kubwa ya PURA ni kuhakikisha Watanzania wananufaika na sekta hii. Ushiriki wa wazawa tunautekeleza kwa njia ya ajira, ujasiriamali kwa kutoa bidhaa na huduma, pamoja na uwekezaji katika miradi mbalimbali,” amesema Bw. Nyangi.
Aidha, amefafanua kuwa lengo la kushiriki katika maonesho hayo ni kuwaelimisha wananchi kuhusu namna wanavyoweza kushiriki kikamilifu katika shughuli za mkondo wa juu wa petroli, na kuongeza kuwa sekta hiyo ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa taifa.
Bw. Nyangi amebainisha kuwa gesi asilia imesaidia sana katika uzalishaji wa umeme, hasa kupitia miradi ya Serikali ya kuzalisha nishati ya umeme wa maji, na kwamba juhudi zinaendelea kuhakikisha nishati hiyo inasambaa zaidi nchini.
“Gesi ya asili inatumika tayari majumbani, viwandani na hata kwenye magari. Tayari inapatikana Mtwara, Lindi na Dar es Salaam, lakini Serikali inaendelea kuwekeza kuhakikisha huduma hiyo inapanuka hadi mikoa mingine,” ameongeza.
Kwa mujibu wa PURA, dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kuwa rasilimali za mafuta na gesi asilia zinawanufaisha Watanzania wote kwa njia ya ushirikishwaji wa wazawa, uboreshaji wa ujuzi wa kitaifa na uendelezaji wa fursa za kiuchumi kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
More Stories
REA yaendelea kusambaza Nishati Bora kwa wananchi,yamshukuru Rais Dkt.Samia
Vivo Energy Tanzania, yazindua Kampeni ya “Uliza Oili ya Shell”
Kampeni ya kisheria ya Mama Samia kuondoa migogoro na ukatili