December 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

PURA ‘Muoneshaji bora ‘maonesho ya bidhaa zanzibar

Na Mwandishi wetu,timesmajira,online

WAZIRI wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda (Zanzibar), Omar Said Shaban ameitunukia Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) cheti cha muoneshaji bora kwenye Maonesho ya Sita ya Bidhaa za Viwanda.

Waziri Shaban ameitunukia Mamlaka cheti hicho jana DIsemba 9, 2021 katika hafla ya kuhitimisha maonesho hayo yaliyofanyika kwenye viwanja vya Maisara, visiwani Zanzibar kama moja ya waoneshaji waliofanya vizuri katika kutangaza shughuli zake kwenye maonesho hayo.

Akizungumza baada ya kupokea cheti hicho kwa niaba ya Mamlaka, Mjiolojia wa PURA Ebeneza Mollel ameeleza kuwa cheti hicho ni matokeo ya juhudi za PURA katika kutimiza jukumu lake la kuuhabarisha umma kuhusu shughuli za mkondo wa juu wa petroli kupitia majukwaa mbalimbali ikiwemo maonesho ya biashara.

“Cheti hiki ni motisha kwetu kuendelea kutoa uelewa kwa Watanzania kuhusu PURA, shughuli inazozifanya na hususani katika kuongeza ushiriki wa wazawa katika shughuli za utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia nchini,” amesema

Mollel amesema PURA imejipanga kuendelea kuwapa taarifa wananchi kuhusu fursa mbalimbali zinazotokana na utekelezaji wa miradi ya utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia sambamba na kuwajengea uwezo wa kuzitumia fursa hizo.

Amesema kuwa jumla ya waoneshaji 113 wameshiriki kwenye maonesho hayo, zikiwemo taasisi za serikali, kampuni binafsi, viwanda vidogo vidogo na wajasiriamali wa bidhaa mbalimbali.