Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

KATIKA hatua madhubuti kuelekea mustakabali wa viwanda rafiki kwa mazingira, kampuni ya Puma Energy Tanzania imezindua rasmi kituo cha umeme wa jua chenye uwezo wa kilowati 570 katika kiwanda cha Alliance One Tanzania Tobacco Limited (AOTTL) kilichopo Morogoro. Mradi huu unadhihirisha azma ya kampuni hiyo katika kutoa suluhisho la nishati safi, nafuu na ya kuaminika kwa sekta ya viwanda nchini.
Mradi huo uko Kingolwira, takriban kilomita 200 kutoka Dar es Salaam, na tayari unaanza kuzalisha nishati mbadala kwa ajili ya kiwanda cha AOTTL katika msimu wake wa juu wa uzalishaji unaoanza Mei hadi Oktoba. Mfumo huo unajumuisha paneli za sola 1,296 na inverter sita zenye ufanisi wa hali ya juu, na umeunganishwa moja kwa moja na gridi ya taifa ili kuhakikisha usambazaji wa umeme usio na hitilafu.
Mradi huu umetekelezwa chini ya Mkataba wa Ununuzi wa Umeme (PPA) wa miaka 10 ulioingiwa mwezi Aprili 2024 kati ya Puma Energy na AOTTL. Ujenzi ulianza Machi 2025 na kukamilika ndani ya muda mfupi mwezi Aprili, huku mfumo huo ukianza kazi rasmi tarehe 4 Mei 2025.
Akizungumza wakati wa uzinduzi, Bi. Fatma Abdallah, Mkurugenzi Mtendaji wa Puma Energy Tanzania, alisema:
“Mradi huu wa sola katika kiwanda cha Alliance One ni mafanikio makubwa, si tu kwa Puma Energy bali pia kwa sekta ya viwanda hapa nchini. Unathibitisha dhamira yetu ya dhati ya kutoa suluhisho la nishati safi, nafuu na ya kuaminika kwa biashara huku tukichangia katika ulinzi wa mazingira na maendeleo ya taifa letu. Tunajivunia kuwa mstari wa mbele katika mageuzi haya ya nishati, tukionesha namna ubunifu unavyoweza kuchochea uchumi unaozingatia uwajibikaji wa kimazingira.”
Mfumo huu wa sola umebuniwa kuwa na dhamana ya utendaji ya hadi miaka 30, na hivyo kuleta ufanisi wa muda mrefu katika matumizi ya nishati na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kupunguza utegemezi wa vyanzo vya nishati visivyo endelevu.
Hatua hii ni sehemu ya maono ya Puma Energy ya kuchochea ukuaji wa sekta ya viwanda kupitia ubunifu wa nishati mbadala na rafiki kwa mazingira. Katika wakati ambapo viwanda vinakabiliwa na gharama kubwa za umeme na changamoto za kimazingira, mradi huu ni mfano halisi wa uwajibikaji wa kibiashara unaokwenda sambamba na uendelevu wa mazingira.
Kupitia mradi huu, Puma Energy inaendelea kuonesha nafasi yake kama kinara wa suluhisho la nishati nchini, na kuweka msingi wa mageuzi mapya katika matumizi ya nishati mbadala kwa ajili ya maendeleo ya viwanda vya Tanzania.
More Stories
TFS yawakaribisha wawekezaji katika vivutio vya utalii wa misitu
Waziri Bashungwa:Tumieni teknolojia za kisasa kudhibiti uhalifu unaovuka mipaka
Flightlink kuzindua Safari za Ndege za Kila Siku kwenda Nairobi wiki ijayo