Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Dar
KAMPUNI ya Puma Energy Tanzania imempongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira bora na wezeshi kwa wawekezaji nchini, hivyo kuwezesha kulipa kodi kwa serikali na kuchochea maeneeleo.
Pongezi hizo zimetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Puma Energy Tanzania, Fatma Abdallah baada ya kampuni hiyo kuibuka kinara kwa kupokea tuzo nne za mlipakodi bora wa mwaka zilizotolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Rais Dkt. Samia alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo iliyofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.
“Mazingira mazuri na wezeshi yaliyowekwa na serikali chini ya uongozi wa Dk. Samia Suluhu Hassan ndiyo yametuwezesha wawekezaji kufanya shughuli zetu katika mazingira mazuri, ndiyo maana sisi Puma Energy Tanzania tumapata tuzo zote.
“Tumekuwa walipakodi wazuri hususan katika sekta ya mafuta na gesi, ndiyo sababu ya kupata tuzo zote hizo. Kwa hiyo tunamshukuru Mungu lakini tunamshukuru Rais Dk. Samia kwa kuweka mazingira yaliyo bora kwa wawekezaji kuendelea kufanya vizuri nchini,” amesema.
Fatma amesema kuwa wanaona zikopelekwa fedha zinazotokana na kodi zinazolipwa na hatimae kuchochea maendeleo makubwa yanayoletwa nchini chi ya Rais Dk. Samia.
“Tumeona miradi mikubwa iliyozinduliwa mwaka 2024 lakini kuna miradi mingine mingi ambayo bado iko katika mchakato wa kuzinduliwa, kwa hiyo tunapolipa kodi tunajua fedha zetu zinakwenda wapi,” ameeleza.
Aidha, ameongeza kuwa, tuzo zote ambazo Puma Energy Tanzania imezipata kutoka TRA zinatokana na uwajibikaji wao katika kulipa kodi kwa wakati na kwamba tuzo hizo ni chachu ya maandalizi ya mwaka ujao wa fedha kufanya vizuri zaidi.
Kupitia hafla hiyo Puma Energy Tanzania imetunukiwa tuzo ya mlipakodi anayekidhi viwango vya ubora katika ngazi ya kitaifa kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Pia kampuni hiyo kupitia kitengo chake cha Wet Cargo, imepata tuzo ya kutambua malipo ya wakati ya kampuni hiyo ya kodi na ushuru katika mwaka wa fedha 2023/2024 katika forodha na ushuru wakati wa siku ya mlipakodi nchini mwaka 2024.
Tuzo nyingine iliyopata Kampuni ya Puma Energy Tanzania Limited ni ya mshindi wa jumla katika kutambua ulipaji wa kodi na ushuru zilizolipwa katika mwaka wa fedha 2023/2024 katika forodha na ushuru wakati wa siku ya kuthamini walipakodi mwaka 2024.
Kwa upande wa tuzo ya nne imetolewa kwa kampuni hiyo kupitia kitengo cha uagizaji wa Wet Cargo kutambua ushuru na ushuru mkubwa wa kampuni uliolipwa katika mwaka wa fedha wa 2023/2024 katika forodha na ushuru 2024.
Tuzo za mlipa kodi Bora wa mwaka hutolewa kila mwaka na TRA ambapo taasisi hiyo hutoa zawadi kwa wafanyabiashara wanaolipa kodi katika makundi mbalimbali.
More Stories
Rais Dkt.Samia asajili timu ndani na nje ya Nchi kukabili Marburg
RUWASA Katavi yasaini mkataba ujenzi bwawa la Nsekwa
Wapanda miti 500,kumbukizi ya kuzaliwa Dkt.Samia