Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
KESI ya madai iliyokuwa imefunguliwa na kampuni ya Pula LLC na Pula Graphite Partners, dhidi ya kampuni ya African Rainbow Minerals Ltd. (ARM) ya nchini Afrika Kusini na washirika wake sita kuhusiana na kuvunja makubaliano ya siri ya mkataba imeondolewa na wakili wa upande wa madai kwenye mahakama ya Biashara ilipokuwa inaendelea. Pula ilifungua kesi hiyo mwaka jana ikidai kulipwa fidia ya dola za Kimarekani $195.
Pula imeondoa kesi hiyo na inakusudia kuifungua tena ndani ya siku kumi. Uamuzi wa kuiondoa na kuifungua upya umefanywa kutokana na sababu za kiufundi ambalo lingeathiri kesi hiyo.
Suala lililokuwa likizungumziwa ni iwapo kuwa na azimio kutoka kwa wakurugenzi wa Pula kuidhinisha kesi hiyo lilipaswa kuambatanishwa kama sehemu ya malalamiko ya awali.
Kesi hiyo ilipowasilishwa awali Oktoba 28,2022, kulikuwa na maoni mbalimbali kutoka Mahakama ya Tanzania kuhusu iwapo ilikuwa ni lazima kujumuisha nakala ya azimio la Bodi ya Wakurugenzi ya kuidhinisha kampuni hiyo kufungua kesi ya madai kama sehemu ya uwasilishaji malalamiko.
Hata hivyo, baada ya maombi ya Pula kuwasilishwa Mwezi Oktoba, Mahakama ya Tanzania ilitoa hukumu katika kesi ya kampuni ya Sharaf Shipping Agency (T) Limited dhidi ya Benki ya Barclays Tanzania Limited tarehe 24 Februari 2022, ambayo ilisisitiza maoni ya mtizamo wa Mahakama kuwa “(a) kesi haiwezi kujibiwa kutokana na kushindwa kuambatanisha azimio la bodi la kuidhinisha kuanzishwa kwa kesi hiyo.”
Kwa sababu hii,Pula Graphite Partners na Pula Group, kwa ushauri wa Wakili wake wameondoa malalamiko yao ya sasa dhidi ya African Rainbow Minerals na watawasilisha tena kesi hiyo wakiwa wameambatanisha azimio la bodi, ambalo linaendana na marejeo ya uamuzi wa kesi yakampuni ya Wakala wa Meli ya Sharaf (T) Limited dhidi ya Benki ya Barclays Tanzania.
Uamuzi huu unakusudiwa kuhakikisha kuwa wanahisa wenye hisa chache kwenye bodi hawapuuzwi katika maamuzi ya kuchukua hatua za kisheria. Pula ni ubia wa 50-50, huku wanahisa wa Tanzania wakiwa na uwakilishi sawa.
Bodi ya Pula ilikutana kabla ya kesi hiyo kuwasilishwa awali na wakurugenzi wa Pula walikubaliana kuhusu kuchukua hatua za kisheria dhidi ya ARM na washirika wake. Licha ya hayo mawakili wa Pula walidhani mkakati bora,kwa kuzingatia uamuzi wa mahakama wa Februari, ulikuwa ni kuondoa kesi ya awali na kuifungua tena.
Rais wa Pula Mary Stith alisema,“Kuondoa na kufungua upya kesi kunatokana na kuweka vizuri masuala ya kiufundi katika taratibu za kufungua kesi . Tumefurahishwa na hatua inayopendekezwa na wanasheria wetu.Tuna nia ya kuwasilisha shauri letu kwa sababu tunaamini kwamba kesi yetu ni nzito na tunaamini kuchukua hatua hii kutahakikisha kwamba makampuni ya Tanzania yatapata nafasi ya kutosha ya kutetea maslahi yake dhidi ya washindani wa kigeni. Kufungua kwetu kesi dhidi ya ARM kusitafsiriwe kama jaribio la kukatisha tamaa uwekezaji wa kigeni.
Tumechukua hatua kwa sababu hatufikirii kuwa ni haki kwa makampuni ya kigeni kukiuka kanuni za biashara dhidi ya makampuni ya Tanzania. Kampuni za kigeni zinazotaka kufanya biashara nchini ziheshimu mikataba na makubaliano wanayosaini na makampuni ya ndani. Ndiyo njia pekee ya kuhakikisha kuwa makampuni ya Tanzania yataweza kusaidia kuendeleza Tanzania na kunufaika na rasilimali kubwa iliyonayo nchi.”
More Stories
Premier Bet yamtangaza mshindi mkubwa
Dkt. Kazungu atembelea miradi ya umeme Dar es Salaam
MSF ilivyojidhatiti kusaidia serikali katika utoaji wa huduma za afya