December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

PSSSF:Wakulima,wafugaji ni wadau wakubwa wa mfuko kwenye uwekezaji wetu katika viwanda

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online,Mbeya

MFUKO wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umesema maonesho ya mwaka huu ya Nanenane yana maslahi mapana kwa Mfuko huo kutokana na uwekezaji ambao umefanya kwenye maeneo ya kilimo na mifugo.

Meneja Uhusiano na Elimu kwa Wanachama, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), James Mlowe (kulia) akimkabidhi mwanachama wa mfuko huo, taarifa za michango yake baada ya kutembelea banda lao kwenye viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya ambako kunafanyika maonesho ya Kimataifa ya Kilimo, Mifugo na Ufugaji(Nane Nane).

Meneja Uhusiano na Elimu kwa Wanachama, Bw. James Mlowe amesema amebainisha hayo Agosti 3, 2023 kwenye banda la mfuko huo kwenye maonesho ya Kimataifa ya Wakulima Nanenane yanayofanyika Kitaifa kwenye viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.

Amesema mfuko unayo majukumu manne ambayo ni kuandikisha wanachama, kukusanya michango, kuwekeza na kisha kulipa mafao.

“Katika eneo hili la uwekezaji,mfuko umewekeza kwenye maeneo mbalimbali mojawapo ni eneo la viwanda ambapo tumewekeza kwenye kiwanda cha kuchakata tangawizi, Mamba Miamba kilichoko Wilayani Same mkoani Kilimanjaro na Kiwanda cha chai Mponde, kilichoko Wilayani Lushoto mkoani Tanga,”amesema na kuongeza kuwa

“PSSSF imewekeza kwenye machinjio ya kisasa Nguru Wilayani Mvomero Mkoa wa Morogoro, kiwanda cha kimataifa cha bidhaa za ngozi Kilimanjaro (KLIC) hii ni fursa kwa wafugaji,”alifafanua Mlowe.

Meneja Uhusiano na Elimu kwa Wanachama PSSSF, James Mlowe akionesha pakiti ya unga wa tangawizi kwenye banda la mfuko huo kwenye maonesho ya Kimataifa ya Wakulima kwenye viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.

Pia Amesema kwa sababu hiyo wakulima na wafugaji ni wadau muhimu wa mfuko huo na kuwataka watembelee kwenye banda la PSSSF ili kujua fursa mbalimbali zinazopatikana kwenye mfuko huo katika maeneo hayo ya uwekezaji kwenye viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo na mifugo.

Akizungumzia kuhusu majukumu mengine ya msingi ya mfuko,Mlowe amesema PSSSF inatoa huduma kwa watumishi wa serikali kuu na za mitaa pamoja na mashirika ambayo serikali inamiliki hisa zaidi ya asilimia 30.

“Hata kauli mbiu ya mwaka huu ya ‘Vijana na Wanawake ni Msingi imara wa Mifumo Endelevu ya Chakula’ inatuunganisha, tunapokuwa na chakula cha kutosha tunajenga nguvu kazi imara ambayo ni vijana na hawa wanapoajiriwa serikalini wanakuja kuwa wanachama wetu,”amesema Mlowe.

Sanjari na hayo ameeleza kuwa katika kushiriki katika maonesho hayo ni ofisi kamili kwani wanawahudumia wanachama wao kama ambavyo wanavyohudumiwa kwenye ofisi zao zilizopo katika maeneo mbalimbali nchi nzima Tanzania Bara na Zanzibar.

Kwa upande wake Mhasibu Mkuu wa PSSSF, Grace Kabyemela,amewahakikishia wanachama wakiwemo wastaafu kuwa mfuko upo katika hali nzuri ya kuhakikisha wanapata mafao yao kwa wakati kwa mujibu wa sheria.

“Sheria inatutaka kuwa mwanachama anayestaafu anapowasilisha nyaraka zilizokamilika anapaswa awe amelipwa mafao yake ya mkupuo ndani ya siku 60, lakini sisi PSSSF tumejiwekea malengo ndani ya siku 30 tunafanya malipo,”ameeleza Kabyemela.

Aidha kuhusu malipo ya pensheni ya kila mwezi, Kabyemela amesema mfuko unahakikisha ikifika tarehe 25 ya kila mwezi wastaafu wanakuwa wamelipwa pensheni zao mwezi.

Mmoja wa wanachama wa PSSSF Habiba Mhina alitembelea banda la PSSSF ili kupata taarifa za michango yake na baada ya kuhudumiwa alipongeza kwa kupatiwa taarifa zake kwa haraka.

“Mimi ni Mfanyakazi kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Dodoma, nimefika banda la PSSSF kupata taarifa za michango na kwakweli chini ya dakika 5 nimepata huduma na kukabidhiwa taarifa ya michango yangu,”.