NA K-VIS BLOG, DAR ES SALAAM
MFUKO wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi
wa Umma (PSSSF) umepokea gawio la zaidi ya shilingi bilioni 14.82 baada ya kodi
kutokana na uwekezaji wa hisa katika benki ya CRDB.
Aidha Waziri Nchemba amefurahishwa na
ongezeko la gawio la serikali na wanahisa wengine kuendelea kuongezeka kila
mwaka.
“Nimefurahi kuona Taasisi na Mashirika
ya Serikali, Halmashauri na Vyama vya Ushirika wamepokea gawio la shilingi
bilioni 22.22 na hivyo kufanya jumla kuu ambayo Serikali imepokea gawio kutoka
benki hiyo kuwa shilingi bilioni 46.88 ukilinganisha na gawio la mwaka jana
ambalo serikali ilipokea la shilingi bilioni 36.1.
Akizungumzia gawio hilo la PSSSF
kwaniaba ya Mkurugenzi Mkuu CPA. Hosea Kashimba, Mkurugenzi wa Fedha, Beatrice
Musa-Lupi alisema gawio hilo ni ongezeko la zaidi ya asilimia 25% mwaka jana
2021 PSSSF ilipokea gawio la shilingi bilioni 11.85 baada ya kodi.
“Fedha hizi zinasaidia kuongeza thamani
ya Mfuko kwa maana kwamba tutazirudisha kwenye uwekezaji lakini vile vile
zinasaidia kuongeza ukwasi wa Mfuko kulipa mafao kwa wakati kama unavyofanya
hivi sasa.” Alifafanua Mkurugenzi huyo wa fedha PSSSF.
“Uwekezaji huo unafanywa kwa kuzingatia
sheria iliyoanzisha Mfuko ambayo inatoa wajibu wa kukusanya michango na wajibu
wa kuwekeza ili kulinda thamani ya Michango ya Wanachama na kuleta uwajibikaji
katika kulipa Mafao.” Alisisitiza Beatrice.
Alisema Mfuko unapofanya uwekezaji
huangalia misingi ya uwekezaji kwa kuangalia mahala ambapo ni salama na kubainisha
kuwa CRDB ni moja ya maeneo salama ambayo hisa za Mfuko ziko salama na zinaleta
faida.
“Tunaamini CRDB itaendelea kufanya
vizuri na faida itaendelea kupatikana na gawio kuongezeka hivyo kuleta faida kwa
wanahisa na wanachama wetu kwa ujumla.” Aliongeza Beatrice.
Naye Fortunatus Magambo, Mkurugenzi wa Mipango
na Uwekezaji PSSSF alisema Mfuko umewekeza asilimia 13.3 ya hisa zote za benki
ya CRDB na anaamini gawio litazidi kuongezeka.
“Tunajivunia mafanikio haya na tunazidi
kuwahimiza CRDB mwaka ujao tupokee gawio kubwa ziadi ya hili.” Alisema.
Kwa upande wake Meneja Uhusiano na Elimu
kwa Umma PSSSF, Bw. James Mlowe alisema moja ya jukumu kubwa la Bodi ya
Wadhamini na Menejimenti ya PSSSF ni kulinda maslahi ya wadau ambao ni wananchama
na ndio maana wanahakikisha wanachagua wabia sahihi wa kufanya biashara na uwekezaji.
“Kama tulivyoshuhudia tumepokea kiasi
hicho ambacho si kidogo na niwaambie kuwa hii ni sehemu ndogo sana ya uwekezaji
ambayo Mfuko umefanya kwani Mfuko umewekeza kwenye maeneo mbalimbali na hili ni
hakikisho uwezo wa Mfuko kumudu majukumu yake ya kulipa Mafao.” Aliwahakikishia
wanachama wa PSSSF.
More Stories
Zaidi ya wananchi 32,000 Vijiji vya Wilaya za Morogoro na Mvomero kuanza kupata mawasiliano
Wafanyabiashara waomba elimu ya namna watakavyorejea soko kuu
DCEA,Vyombo vya Ulinzi na Usalama vyafanya operesheni ya kihistoria