NA K-VIS BLOG/KHALFAN SAID
MAKAMU
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa
Umma (PSSSF), Dkt. Aggrey Mlimuka ametembelea banda la Mfuko huo kwenye
Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yanayoendelea kwenye
viwanja vya Julius Nyerere barabara ya Kilwa na kusema amefarijika kuona
Wanachama na Wastaafu wakitoka kwenye banda hilo wakiwa na nyuso za furaha.
Ameyasema
hayo Julai 9, 2023 wakati akitoa tathmini yake baada ya kutembelea banda namba
13 la Ushirikiano wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya PSSSF na NSSF ili kujionea
jinsi Wanachama na Wananchi kwa ujumla wanavyohudumiwa.
“Nimefurahishwa
kuona huduma zinavyotolewa na wafanyakazi wetu, huduma zote zinazotolewa
ofisini zinapatikana hapa,” alisema.
Alisema amefarijika
zaidi kuona Wanachama wanaondoka katika banda hilo na nyuso zenye tabasamu na
wenye furaha.
Alisema
Mfuko umepita katika changamoto lakini sasa PSSSF iko katika hatua za
mafanikio.
“hali hii imechagizwa zaidi na hatua
za makusudi zilizochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe.
Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kutoa non cash bond, ya trilioni 2.1, fedha
hizi zimesaidia sana kuuwezesha Mfuko kuwa katika hali nzuri na hivyo kuweza
kulipa Mafao kwa Wastaafu kwa wakati.” Alifafanua Dkt. Mlimuka.
Aliwataka
watumishi wa Umma kuendelea kuchapa kazi kwani serikali inajali maslahi yao na
iko tayari kutatua changamoto zinazowakabili.
“Tunawahakikishia
hakuna haja ya kubabaika, Mafao yenu yanatunzwa vizuri na yako salama, Bodi ya
Wadhamini tunafanya kazi kwa umakini mkubwa, jukumu tulilokabidhiwa na serikali
yetu tunalitekeleza kwa uaminifu mkubwa na uadilifu mkubwa msiwe na wasi wasi
wowote.” Alisisitiza Dkt. Mlimuka.
Naye Mkurugenzi
wa Uendeshaji PSSSF Bw. Mbarouk Magawa alisema Mfuko ulipoanza miaka mitano
baada ya kuunganishwa kwa Mifuko ya PSPF, PPF, GEPF na LAPF, kazi kubwa
iliyokuwa ikifanyika ni kuunganisha mifumo ili iweze kusomana.
“Kingine
tulichokuwa tunafanya ni kuweza kuwatambua Wanachama wetu, na tuweze kuwaeleza
wanachama wajitambue kuwa sasa wao ni wanachama wa PSSSF (culture change) , hilo
tumelifanikisha kwa asilimia kubwa sana na sasa Mfuko umeanza kwenda mbele na
niwahakikishie wanachama wetu kuwa Mfuko uko imara, Mfuko unaendelea kufanya
vizuri na kuimarika zaidi.” Alisema
Kwa upande
wake Mkurugenzi wa Fedha PSSSF, Bi. Beatrice Musa-Lupi alisema PSSSF
imejiimarisha kuhakikisha Mwanachama akiwa amekamilisha nyaraka zake
zinazohitajika analipwa Mafao yake kwa wakati ndani ya siku 60 kama sheria
inavyoelekeza.
Ingawa Mfuko
umejiwekea malengo endapo Mwanachama atakuwa amekamilisha nyaraka zake zote
analipwa ndani ya siku 30, anasema Meneja Uhusiano na Elimu kwa Wanachama, Bw.
James Mlowe.
“Biashara
yote tunayofanya mwisho wa siku ni kuhakikisha kwamba Mafao yanalipwa, na Mafao
yatalipwa kwa kuhakikisha kwamba kanuni za uandaaji wa hesabu, kanuni za
utunzaji wa fedha ziko sahihi, ukaguzi unafanyika kwa kutumia taratibu
sahihi,hivyo kupelekea kiasi ambacho kinatarajiwa wakati wowote wanachama
wanapostaafu waweze kupata Mafao yao.” Alibainisha Mkurugenzi huyo wa Fedha
PSSSF, Bi. Beatrice Musa-Lupi.
Alisema
baada ya kukamilisha mchakato wa kuunganisha Mifuko kwa mafanikio ambapo kazi
kubwa ya kuhakikisha wanaweka hesabu sahihi na hesabu zinazoweza kuaminika na
umma, kazi iliyopo sasa ni kuwahudumia Wanachama kwa Viwango vya juu
vinavyoendana na sheria na kanuni.
“Kwa miaka
yote minne na sasa….. tunaelekea mitano,
Mfuko umepata hati safi kutoka
ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, CAG, vile vile tumepata hati ya kutambuliwa
uandaaji bora wa hesabu kutoka Bodi ya Hesabu na Ukaguzi (NBAA) kwa miaka minne
mfululizo.” Alifafanua.
Kwa upande
wao Wanachama wa PSSSF wameonyesha kuridhishwa kwao na huduma zinazotolewa na
Mfuko.
“Pensheni
yangu naipata kwa wakati muafaka, zile tarehe nilizoambiwa nitakuwa napata Pensheni
ndio hizo hizo napata,” anasema Abdallah Mandwanga ambaye ni Mstaafu.
Bw.
Mandwanga alisema “Wakati nafuatilia Mafao yangu ya kustaafu nilishughulikiwa
vizuri mno, ninaomba waendelee hivyo
hivyo.” Alifafanua Bw. Mandwanga.
“Nayasema
haya kutoka moyoni, na sio kuwafurahisha wahudumu hapa, nayasema haya kutoka
moyoni na nimeridhishwa sana na huduma zao kwakweli nawapa hongera kubwa.” Alisema
Bw. Mandwanga.
Aidha
Mstaafu mwingine Bw. Dominic Chanchu alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa nyuma ya mabadiliko haya.
“Sisi
tunaona ubora umeongezeka, mama Samia ameboresha hali, sisi tunakula vizuri na
tunasema Alhamdullillah, Pensheni inaingia kwa wakati, wastaafu hakuna kulia
lia siku hizi labda tu iwe vurugu zetu.” Alibainisha Bw. Chanchu.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato