May 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

PSSSF Kinara Tuzo za NBAA 2022

 

*DG PSSSF: Tuzo iwe chachu ya kufanya vizuri zaidi

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umetunukiwa tuzo ya mshindi wa kwanza ya umahiri katika uaandaji wa taarifa za mahesabu kwa mwaka unaoishia 2022, katika kundi la hifadhi ya jamii ambapo katika washindani wengine walikuwa ni Mfuko wa Bima ya taifa (NHIF) na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).

Utoaji wa tuzo ulioratibiwa na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) ulifanyika Disemba 1,2023 jijini Dar es Salaam ambapo washindi katika makundi mbalimbali walikabidhiwa tuzo zao na CPA. Jamal Kassim Ally, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Zanzibar.

Kwa upande wa PSSSF, tuzo hiyo ilipokelewa na Mkurugenzi Mkuu wake, CPA. Hosea Kashimba ambaye aliongozana na baadhi ya watumishi kutoka Kurugenzi ya Fedha, PSSSF wakiongozwa na Mkurugenzi wa fedha wa PSSSF, Bi. Beatrice Lupi.

“Kwa kweli tunamshukuru Mungu kwa tuzo hii, kwani hii mara ya pili kupata tuzo hii na ni wazi kwamba watumishi wetu wanafanya kazi kwa umahiri wa hali juu sana, hakika nawapongeza na nawaomba waendelee kufanyakazi kwa kuzingatia ubora na taratabu zote za ndani na za kimataifa” alisema CPA. Kashimba.

CPA. Kashimba alisema lengo la PSSSF siku zote ni kuishi dira yake ambayo ni kuwa Mfuko unatoa huduma bora Zaidi za Hifadhi ya Jamii nchini na ili lengo hilo lifikiwe Mfuko unatumia Wafanyakazi wenye uwezo, ari na kutumia teknolojia ya kisasa.

“Sisi PSSSF tuna maadili yetu ambayo ninaamini ndio chachu ya kufanya vizuri katika maeneo mbalimbali, maadili hayo ni; kumjali mteja, uaminifu, kufanya kazi kwa pamoja, weledi na uwazi” alifafanua CPA. Kashimba ambaye hivi alipokea tuzo ya kuwa mshindi wa kwanza katika kundi la watendaji wakuu bora kutoka taasisi za umma.

Mkurugenzi Mkuu huyo aliwahakikishia wanachama wa PSSSF kuwa Mfuko unafanya kazi kwa weledi wa hali juu hali inayosababisha kupokea tuzo mbalimbali ikiwemo hiyo ya uadaaji bora wa mahesabu.

Naye Mkurugenzi wa fedha, Bi. Lupi akizungumzia tuzo hiyo alisema, “Kwa kweli namshukuru Mungu, watumishi wote wa PSSSF hususani wa Kurugenzi ya fedha kwa kuwezesha kupatikana kwa tuzo hii, tuzo hii iwe chachu ya kuhakikisha kwamba mahesabu yetu yanaandaliwa vyema kila wakati”.

Utoaji wa tuzo hizo ulishuhudiwa na Bi. Asmaa Resmouki, rais wa International Federation of Accountants, waalikwa kutoka nchi jirani na watendaji kutoa taasisi mbalimbali.

NBAA ilikuwa na kikao chake cha mwaka jijini Dar es Salaam kuanzia Novemba 29 hadi Disemba 1,2023 ambapo Wahasibu na Wakaguzi walihudhuria, kikao hicho kilihitimiswa na sherehe ya utoaji wa tuzo za umahilli katika uandaaji wa taarifa za mahesabu.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, CPA. Jamal Kassim Ally (kushoto), akimkabidhi Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), CPA. Hosea Kashimba, tuzo  ya umahiri katika uaandaji wa taarifa za mahesabu kwa mwaka unaoishia 2022 ambapo PSSSF imeibuka kidedea miongoni mwa taasisi za hifadhi ya Jamii zilizoshiriki kinyang’anyiro hicho ambazo ni Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF). Hafla hiyo ambayo imeandaliwa na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) ilifanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.