Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
MKURUGENZI wa Idara ya Maendele ya Watoto kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum Sebastian Kitiku amesema,Programu Jumuishi ya Kitaifa ya Malezi ,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM ) haikuja kama mbadala wa programu nyingine za masuala ya watoto zilizotangulia.
Akifungua warsha ya wadau wanaojishughulisha na malezi na makuzi ya watoto iliyofanyika mkoani Dodoma,Kitiku amesema ,wakati wadau wakitekeleza programu hiyo katika kelimisha jamii,lazima wazingatie na programu zilizopo.
“Programu hii ,haikuja ku’replace’programu zilizopo ,imekuja kuangalia mahali ambapo hapajaweka nguvu au paliposahaulika ili kuhakikisha mtoto anakua kwa utimilifu wake.”
Kwa mujibu wa Muongozo wa Programu ya Taifa ya MMMAM, Programu hii inatambua programu zilizopo za kitaifa ambazo ambazo utekelezaji wake unajumuisha wadau wa sekta mbalimbali katika kutoa huduma zinazolenga vipengele vyote vya ukuaji na maendeleo ya mtoto.
Pamoja na programu nyingine,pia Programu hii inalenga kutumia uzoefu wa programu zilizopo ikiwemo Programu Jumuishi ya Taifa ya Lishe II ya mwaka 2021/22-2025/26 na mpango Kazi wa Taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA wa 2017/18-2021/22).
Amesema ,programu hiyo imewaleta wadau wengi pamoja ili kumlea mtoto katika maeneo muhimu matano badala ya kila mdau kufanya taratibu zake katika malezi ya mtoto.
“Programu hii imewaleta wadau pamoja ili kumlea mtoto bila kumkata vipande vipande..,mfano hapo awali kabla ya programu hii kuwepo,watu wa afya walimlea mtoto kivyao ,lakini tukasema, tulete programu hii ambayo itamlea mtoto kwa pamoja ili kuleta tija katika malezi na makuzi ya mtoto.”amesema Kitiku na kuongeza kuwa
“Moja ya sababu ya kuwekeza kwa mtoto ni kuhakikisha anapata mahitaji yote muhimu katika umri wa miaka 0 hadi minane ili kuwa na Taifa la kizazi chenye tija.”
Amesema sayansi inaeleza wazi kuwa asilimia 80 ya ubongo wa mtoto unakua katika kipindi cha umri wa miaka 0-8 ,huku akisema bila kumlea vyema mtoto inavyotakiwa katika umri huo ,kutakuwa na taifa lenye watu ambao hawana uwezo mkubwa katika kufikiri na kutafakari mambo na hivyo kushindwa kuchangia katika uchumi wa nchi.
“Kuna watu wazima sasa hivi wanaweza kungea jambo mpaka ukajiuliza maswali kutokana na alichozungumza na umri wake,hii ni kutokana na uwekezaji uliofanyika akiwa na umri wa miaka 0-8.”amesema Kitiku
Awali Mkurugenzi wa Mtandao wa Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (TECDEN) Mwajuma Rwebangira alisema lengo la kikao hicho ni kuwapitisha wadau wa Mradi wa Mtoto Kwanza ambayo inalenga katika utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT- MMMAM) ili waweze kwenda kutoa elimu kwa jamii kuhusu Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto na hatimaye kufanikiwa kwa kwa Programu hiyo ya Taifa .
“Sisi wadau wa mradi wa Mtoto Kwanza katika kutekeleza mradi huu tuhakikishe tunatumia Programu hii ili kuhakikisha tunajikita katika kutoa elimu ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto katika maeneo tunayotoka” amesema Mwajuma
Mkurugenzi wa Shirika la Bright Jamii Initiative Irene Fugara ni miongoni mwa wadau walioshiriki katika warsha hiyo ambapo amesema,Shirika la Bright Jamii limejikita kuhakikisha linatoa elimu ya Malezi kwa Mtoto ili kupambana na ukatili wa kijinsia dhidi ya Watoto ili iweze kusaidia kuondoka na tatizo hilo.
“Lazima tuijengee jamii uwezo wa kuwa na uelewa kwenye masuala ya Malezi ili iwasaidie katika kuhakikisha watoto wanalelewa kwenye mazingira mazuri na yatakayowawezesha kuwa wazalendo, jasiri na wenye kujiamini ” amesema
Naye Meneja Programu kutoka Shirika la KIHUMBE Jeremia Henry amesema Shirika hilo linashirikiana na Serikali na wadau wa maendeleo hasa upande wa miradi ya watoto na vijana katika masuala ya Afya, Malezi, Makuzi, pamoja na Lishe ndani ya jamii.
“Kupitia Programu hii Jumuishi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto tumepata uelekeo utakaotusaidia kuona ni namna gani tutatoa elimu ya Malezi kwa jamii ili tuwe na jamii yenye watu wenye Malezi bora” amesema Jeremia
More Stories
Kiswaga:Magu imepokea bilioni 143, utekelezaji miradi
Zaidi ya milioni 600 kupeleka umeme Kisiwa cha Ijinga
Kamishna Hifadhi ya Ngorongoro atakiwa kupanua wigo wa Utalii nchini