March 26, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Prof.Muhongo apongezwa kuleta majadiliano sekta ya elimu Musoma

Na Fresha Kinasa,TimesMajiraOnline,Mara

MBUNGE wa Jimbo la Musoma Vijijini Prof. Sospter Muhongo amepongezwa kwa hatua njema ya kuleta Majadiliano  yenye mapendekezo ya Uboreshaji wa  Ufundishaji,Ujifunzaji na Uelewa wa Wanafunzi kwa lengo la kuongeza ufaulu kwa wanafunzi wanosoma shule za Msingi na Sekondari Jimboni humo.

Pongezi hizo zimetolewa na Walimu wa taaluma wa shule za msingi na sekondari   wa Jimbo la Musoma Vijijini Machi 25, 2025 Wakati wakitoa shukrani zao za dhati kwa Mbunge huyo ikiwa ni siku ya kwanza ya majadiliano hayo yanayoendelea kwa muda wa siku tatu.

Ambapo,wamesema kuwa, majadiliano hayo yamewajengea uwezo madhubuti na kuwafanya wawe mahiri katika kuwasaidia katika utekelezaji wa majukumu yao kwa ufanisi mzuri.

Wamesema,maono ya Mbunge wao Prof. Muhongo na dhamira yake ni njema sana katika kuimarisha na kuleta mageuzi chanya yenye tija kwa sekta ya elimu jimboni humo. Hivyo watahakikisha majadiliano waliyoyafanya wanayazingatia  kwa ufanisi.

Wameongeza kuwa,kutokana na mabadiliko ya muongozo wa mitaala ya elimu katika ufundishaji yapo mambo muhimu ambayo wameyapata ambayo yatakwenda kuwasaidia wanafunzi kupata ufaulu mzuri kwani  ndio shauku kubwa ya Mbunge Prof. Muhongo na wadau wa elimu katika Jimbo hilo

Mwalimu  Malima Musa kutoka shule ya Sekondari Bwasi amesema kwenye uboreshaji wa eneo la ufundishaji wamejifunza namna ya kuwasaidia wanafunzi darasini na kuelewa kile wanachofundishwa ili kufanya vizuri kwenye masomo yao kwa faida yao, Jamii na Taifa Pia.Huku akisema utoaji wa motisha kwa wanafunzi wanaofanya vizuri ni muhimu kuleta ushindani kwa wanafunzi wengine.

Pia ameongeza kuwa,wamejadiliana pia suala la kufuatilia tabia nzuri za wanafunzi na wale wenye tabia mbaya zikiwemo za utoro kurekebishwa kwa kuwashirikisha wazazi na jamii inayozunguka shule.

“Nitumie nafasi hii kutoa shukurani nyingi kwa Mbunge Prof.Sospeter Muhongo kwa kutuletea mjadala huu tunaojadiliana hapa leo, naamini kabisa,  Kila mwalimu hapa amefurahishwa na majadiliano haya ni imani yetu yanakwenda kuongeza ufaulu kwenye shule zetu ndani ya jimbo zima la Musoma Vijijini na kuleta heshima kubwa kama ambavyo Mbunge wetu anahesahimika kwa utendaji kazi wake mahiri.”,amesema Mwalimu Malima.

Kwa upande wake Mwalimu Fabian Eronje kutoka shule ya msingi Rwanga amesema baadhi ya viongozi wa kisiasa wamekuwa na vitisho kwa walimu ikiwa ni pamoja kushinikiza walimu kuhama kwenye maeneo yao jambo linaloshusha ari ya ufundishaji na kuomba eneo hilo kuangaliwa vyema.

“Mbunge amefanya Jambo la kipee Sana kuleta Majadiliano haya,hakika mambo mengi ambayo tumejadiliana,yatakuwa chachu kubwa kwetu,ameleta Wataalamu ambao wametupa mambo mengi mazuri ambayo yataleta mabadiliko kwetu sote.”amesema Fabian.

Mmoja wa Watoa mada kwenye majadiliano hayo ni  Dkt.George Kahangwa kutoka chuo Kikuu Cha Dar es laam  amesema, walimu wakiamua na majadiliano waliyoyapata mabadiliko makubwa yanakuja Musoma Vijijini na kuongeza ufaulu kwa kiwango kikubwa.

Pia ameebainisha kuwa,walimu wamepewa dhamana ya kuwasaidia wanafunzi kwenye ufundishaji na wanapaswa kufanya hivyo kwa kushirikiana na wazazi,walezi na jamii inayozunguka shule husika  kwa dhamira ya dhati na upendo.

Katika siku ya kwanza ya majadiliano hayo,yamewahusisha walimu wa shule za msingi na sekondari. Kikao cha pili kiliwashirikisha waratibu wa elimu wa Kata 21 pamoja na watendaji wa Kata ( WEO)

Dkt.Zabron Kengera akizungumza na watendaji wa Kata na maafisa elimu Kata amesema ujio wa majadiliano hayo yamekuja kutokana na kufanya vibaya kwenye matokeo ya elimu Musoma Vijijini na kutafuta ufumbuzi utakao leta mabadiliko chanya.

Amesema kushuka kwa elimu na kufanya vibaya kila mmoja anahusika wakiwemo watendaji wa Kata na afisa elimu Kata hivyo ni muhimu kuwa na majadiliano na kuacha kunyoosheana vidole.

Aidha,Machi 26,2025 majadiliano hayo yataendelea ambapo saa 3 asubuhi hadi saa 6 yatawashirikisha walimu wakuu wa shule za msingi na kuanzia saa 8 mchana hadi saa 11 jioni utakuwa mijadala kwa wakuu wa shule za sekondari zilizomo ndani ya Jimbo hilo.