May 13, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Prof.Muhongo amshukuru Rais Samia kwa fedha nyingi miradi ya elimu Musoma Vijijini

Fresha Kinasa,TimesMajiraOnline,Mara.

MBUNGE wa Jimbo la Musoma Vijijini Prof.  Sospeter Muhongo  amesema kuwa,kwa dhati kabisa kutoka moyoni mwake  anamshukuru Rais  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa hatua yake njema   ya  kutoa fedha nyingi katika Jimbo la Musoma Vijijini ambazo zimesaidia kuimarisha sekta ya elimu Jimboni humo.

Ambapo amesema kuwa,Fedha zilizotolewa zimewezesha kuanzishwa na kujengwa kwa shule mpya za sekondari Jimboni humo   ikiwemo shule mpya ya Kumbukumbu ya Prof.  David Massamba iliyofunguliwa hivi karibuni Kijiji cha Kurwaki Kata ya Mugango ambayo itasaidia wanafunzi kusoma kwa ufanisi na kuenzi Historia ya Gwiji huyo na bingwa wa Lugha ya kiswahili.

Prof. Muhongo ameyasema hayo Bungeni Jijini Dodoma Mei 12, 2025 akichangia Wizara  ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na kubainisha kuwa,Wananchi wa Jimbo la Musoma Vijijini wanamshukuru sana  Rais Dkt.Samia  kwa upendo wake wa dhati aliouonesha kwa kutoa fedha ambazo zimeleta mageuzi makubwa kwa sekta ya elimu Jimboni humo.

Amesema,kwa hatua njema na nzuri zilizofanywa na Rais Dkt. Samia katika sekta ya elimu Jimboni mwake na maeno mbalimbali nchini, amewaomba  wabunge  kuipitisha bajeti ya Wizara ya Elimu kwa kuwa ndio roho ya nchi na inaleta mageuzi  makubwa hususani katika kututoa kwenye Dira ya Taifa ya Maendeleo iliyokwisha inatupeleka kwenye Dira ya  2025 mpaka 2050.

Aidha Prof.Muhongo amesema kuwa,  suala la ufundishaji, Ujifunzaji, uelewa na ufaulu lazima viende pamoja na Jimbo la Musoma Vijijini tayari limeshafanya mijadala ya elimu katika utekelezaji wake ili kuleta matokeo chanya yenye tija jimboni humo.

Aidha Prof.Muhongo amesema kuwa, ushauri wake kutokana na Dira ya Maendeleo inayoanzia mwaka huu ni pamoja na ujenzi wa shule za magorofa kutokana na uhaba wa ardhi kufuatia kuongezeka kwa idadi ya watu huku ardhi ikibaki ile ile.Huku askisema kuwa, kufika juni mwaka huu idadi ya watanzania itafikia asilimia 70.55 hivyo ujenzi wa aina hiyo za shule ni muhimu kwa sasa.

Amesema elimu ni ajira na ndio yenye soko kubwa duniani hasa kupitia masomo ya sayansi hivyo lazima kuzalisha wasomi wengi zaidi  ambao watakuja kuleta matokeo chanya na kuchangia kasi ya maendeleo katika Jamii na Taifa pia.

“Mheshimiwa Waziri ujenzi wa shule lazima ubadilike na tujenge kwa kwenda juu kutokana na ufinyu wa ardhi ambao tuko nao kwa sasa hapa nchini.Wenye duala la ajira kupitia elimu kuna upungufu mkubwa duniani hasa eneo la teknolojia hivyo mitaala yetu iendane na kuwapata Wana-sayansi…”,amesema Prof. Muhongo.

Pia ameongeza kuwa,  ili kuzipata ajira hizo sekondari zote zinapaswa kuwa na maabara pamoja na maktaba zitakazowezesha kupata wanasayansi wengi  ambao ni chachu ya maendeleo.

“Tuongeze wanafunzi wengi wanaokwenda kusoma nje, na tuchague vyuo vizuri sio kuhesabu tu yuko nje, na nadhani Wizarani mnavifahamu na mfano mzuri ni India inafanya maajabu na tunapeleka Watoto kusoma India na China. Na bado wao wanapeleka nje mwaka 2016 India ilikuwa na Wanafunzi 440,000. wanasoma nchi za nje mwaka 2023 wamekuwa na wanafunzi zaidi Mil. 1.4, kwa hiyo na sisi tupeleke wanafunzi nje..Hawa wa India wanasoma Ujerumani asilimia 60 wanafanya shahada za Engineering na mambo ya Technology. “amesema Prof. Muhongo.

Juma Bwire ni Mkazi wa Nyakatende Musoma Vijijini ameiambia Majira Online kuwa, ili maendeleo ya nchi yazidi kukua juhudi zinapaswa kuendelea kufanywa kuimarisha sekta ya elimu nchini ambayo ndio huzalisha Wasomi wa fani mbalimbali. Huku pia Wananchi akiwahimiza kuwasomesha Watoto wao  hasa Masomo ya Sayansi ambayo wigo wa ajira na faida yake katika nchi ni kubwa katika ushindani wa Maendeleo na nchi za ukanda wa Maziwa Makuu.