March 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Prof.Muhongo aipatia mifuko 50 ya saruji kamati ya ujenzi Sekondari ya  Mmahare

Fresha Kinasa, TimesMajira Online Mara.

MBUNGE wa Jimbo la Musoma Vijijini Mkoa wa Mara Prof.Sospter Muhongo ameipatia  Kamati ya ujenzi ya Mmahare Sekondari   mifuko 50 ya Saruji Kati ya mifuko 155, aliyochangia kwenye Harambee ya ujenzi wa shule hiyo hivi karibuni,  ambayo ni shule ya tatu ya kata ya Etaro.

Amesema, Wakiimaliza ipasavyo Saruji hiyo,anaongeza mifuko mingine, huku pia akipongeza Kijiji hicho cha Mmahare kwa  Kasi nzuri ya ujenzi huo ambapo tayari kimetumia mifuko yote 150 ya Saruji aliyoitoa awali katika Kijiji hicho na Vijiji vyote  vinavyojenga Sekondari mpya ambapo  kila Kijiji kilipata mifuko 150. Na Fedha zilizonunua Saruji hiyo ni zile za Mfuko wa Jimbo. 

Hayo yameelezwa Machi 10,2025,kupitia taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo hilo ambapo taarifa hiyo pia imesema kuwa ” Ujenzi wa Msingi wa  kwanza wa Mmahare Sekondari ya Kijiji cha Mmahare Kata ya Etaro.  Ujenzi wa msingi huo utakamilishwa leo 10.3.2025.”imeeleza sehemu ya taarifa hiyo. 

Katika harambee ambayo aliiongoza Prof. Muhongo katika Kijiji cha Mmahare, Wanakijiji walichangia mifuko 155 ya Saruji, na Mbunge huyo  pia alichangia mifuko 155.  Huku akitoa wito kwa Wadau mbalimbali kujitokeza kuchangia ujenzi wa Sekondari mpya 12, zinazojengwa Musoma Vijijini. 

Taarifa hiyo imeongeza kuwa,”Naomba kuwakumbusha kwamba hivi karibuni Mbunge wa Jimbo aligawa Saruji Mifuko 150 kwa kila kijiji kinachojenga sekondari mpya. Fedha za saruji hiyo ni zile za Mfuko wa Jimbo.Kwenye miradi yote ya ujenzi ya Jimboni mwetu, Mbunge wa Jimbo huwa anapiga harambee  kuchangia ujenzi unaofanywa kwa kutumia nguvukazi na michango ya fedha za wanavijiji.”imeeleza taarifa hiyo.

Fabian Thomas ni Mkazi wa  Kijiji cha M’mahare amepongeza jitihadi za Wananchi na Mbunge Prof. Muhongo, amesema  zimeendelea kuleta manufaa  ikiwemo kusaidia Watoto kusoma karibu na nyumbani na kuondoa changamoto ya kutembea umbali mrefu kwenda masomoni.

“Mbunge hapendi Watoto watembee umbali mrefu kwenda masomoni. Ndio maana utakuta kata moja ina Sekondari tatu hii  ni kutokana na hamasa yake kwetu Wananchi. Na sisi  tunashirikiana naye kwa kila hatua pamoja na Serikali yetu kufanikisha agenda ya maendeleo jimboni mwetu.” amesema Thomas.