March 29, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Prof.Muhongo achangia mifuko 250 ya saruji ujenzi shule ya sekondari Nyabakangara

Fresha Kinasa,TimesMajiraOnline,Mara.

KATIKA kuendelea kuunga mkono juhudi za uimarishaji wa Sekta ya Elimu ndani ya Jimbo la Musoma Vijijini Mkoa wa Mara  Mbunge wa Jimbo hilo Prof.Sospeter Muhongo amechangia mifuko 250 ya saruji kwenye ujenzi wa shule ya sekondari Nyabakangara ukiwa ni mkakati wake wa kuhakikisha Watoto wanasoma karibu na kuondokana na changamoto ya kutembea umbali mrefu. 

Prof.Muhongo amechangia mifuko hiyo katika harambee aliyoipiga Machi 25, 2025,kwenye Kitongoji cha Kamatondo Kata ya Nyambono jimboni humo.Ambapo pia  ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo wanachama wa Chama Cha mapinduzi ,wazawa wa Kata hiyo, Wananchi na wadau mbalimbali wa maendeleo. 

Aidha katika harambee hiyo, mifuko mingine ya Saruji 204 imechangiwa na wadau mbalimbali wa elimu, wapenda maendeleo pamoja na Wananchi. Huku pia  tripu tano za mawe zikichangwa, na pesa taslimu kiasi cha Shilingi 448,000, na tayari  matofali 3,700, yamefyatuliwa.

Akizungumza na Wananchi katika harambee hiyo,Prof.Muhongo ametanabaisha kuwa, elimu ni jambo muhimu sana katika kuleta maendeleo. Hivyo, ataendelea kuhakikisha sekta hiyo inapewa kipaumbele madhubuti ikiwemo  kuimarisha miundombinu ya elimu kwa njia shirikishi kwa kuchangia ujenzi wa shule mbalimbali mpya,maabara na Walimu wa masomo ya Sayansi. 

Ameongeza kuwa,ili Wananchi wa Musoma Vijijini waweze kuwa na maendeleo ni lazima wakubali kuhakikisha watoto wao wanasoma na kupata elimu kwa ukamilifu ili elimu hiyo baadaye ilete manufaa kwao  katika nyanja za kiuchumi na Kijamii. 

Ametoa wito kwa Wadau mbalimbali wa elimu na wapenda maendeleo ndani ya Jimbo hilo na mkoa wa Mara kwa ujumla.Kujitokeza kuchangia maendeleo ya elimu jimboni humo kwani kufanya hivyo ni kuweka hazina itakayoleta tija kwa siku za usoni na kufikia malengo ya kuwa na Wasomi wengi wenye ujuzi kwa faida ya Jamii na Taifa pia. 

“Ndugu zangu,kipaumbele chetu namba moja bado ni elimu na ndio maana tunafanya jitihada mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuendesha harambee za ujenzi wa shule na kuandaa mijadala ya kuinua kiwango cha ufaulu kwenye shule zetu.  Jambo hili ni muhimu sana tuendeleeni  kushirikiana na kushikamana kwa upendo kufanikisha maendeleo jimboni mwetu. Leo nitachangia mifuko 250 ya Saruji katika ujenzi wa  shule ya Nyabakangara lakini awali kupitia Mfuko wa Jimbo nimeshatoa mifuko 150 kwenye ujenzi huu. ” amesema Prof. Muhongo. 

Aidha, Kamati ya Ujenzi
Iliundwa hapo  jana kwa kila Kitongoji kutoa mjumbe mmoja na kamati kuwa na wajumbe saba.  Ambapo Uamuzi wa Wanakijiji ujenzi uanze mara moja na Halmashauri iharakishe upatikanaji wa ramani za ujenzi

Esta Peter ni Mwananchi wa Kijiji hicho amepongeza  ushirikiano uliopo baina ya Wananchi jimboni humo  na Mbunge wao katika kusukuma mbele ajenda ya maendeleo  ikiwemo kushiriki pamoja katika uchangiaji wa Maendeleo ya sekta ya elimu.

Masatu Paul amesema kuwa, maono ya prof.  Muhongo ni mazuri  na yanalenga kuhakikisha Jimbo hilo linakuwa na shule nyingi za Msingi na Sekondari  ili kila mtoto apate fursa ya kusoma akiwa karibu na nyumbani.Jambo ambalo litasaidia katika  kuwaandaa Wasomi wengi na mahiri ambao ni tegemeo kwa Jamii na Taifa kwa siku za usoni.

Machi  26, 2025,Prof.Muhongo atapiga  harambee ya ujenzi wa Kataryo sekondari ya Kijiji cha Kataryo Kata ya Tegeruka. Ambapo Kata ya Nyambono na Tegeruka wanaanza ujenzi wa shule ya pili kwenye Kata zao.