Na Jackline Martin,Timesmajira
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mpango na Uwekezaji, Profesa Alexander Kitila Mkumbo, ametoa wito kwa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi (TISEZA), viongozi na wananchi wa Kilwa kuendelea kutoa ushirikiano madhubuti ili kufanikisha utekelezaji wa mradi mkubwa wa kilimo na viwanda unaotekelezwa na Kampuni ya Pan Tanzania Agriculture Developments.
Amesema ulinzi wa amani, utayari wa wananchi kushiriki fursa, na usimamizi wa viwango vya juu ni misingi itakayowezesha mradi huo kuleta manufaa makubwa kwa Taifa.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi hati isiyo asili kwa mwekezaji Pan Tanzania Agriculture Developments Ltd, Prof. Mkumbo amesema tukio hilo ni hatua muhimu na ya kimkakati kwa maendeleo ya Kilwa na Taifa kwa ujumla.
Prof. Mkumbo amesema mradi huo mkubwa unahusisha uwekezaji wa dola za Marekani milioni 640, ukitekelezwa kwenye mashamba ya vijiji vya Mavuji, Migeregere, Nainokwe na Liwiti, Wilaya ya Kilwa, Mkoa wa Lindi.
Amebainisha kuwa mradi huo unajumuisha kilimo cha kisasa cha mihogo, mazao mengine na uanzishaji wa kongani ya viwanda 150 ikiwa ni sehemu ya maendeleo ya viwanda yanayolenga kuongeza thamani ya mazao.

Amesema maandalizi ya awali ya mradi yameshaanza, ikiwemo ujenzi wa barabara kuu ya kilomita 29.44 kuunganisha maeneo yote manne ya mradi, ujenzi wa majengo ya utawala, maeneo ya malazi, kituo cha utafiti wa mbegu, taasisi za mafunzo na maghala katika kijiji cha Mavuji ambacho kitakuwa kitovu cha viwanda kuanzia mwaka 2028.
Katika kijiji cha Migeregere, Waziri amesema kutakuwa na kazi za usafishaji wa ardhi, ujenzi wa miundombinu na usimamizi wa mashamba kwa teknolojia za kisasa, huku mfumo wa umwagiliaji ukitarajiwa kukamilika ifikapo 2030. Nainokwe, kwa upande mwingine, litajengwa mashamba ya kisasa yanayosimamiwa kiteknolojia hadi mwaka 2035, huku Liwiti likitekeleza kilimo cha kibiashara kwa njia endelevu.

Amebainisha kuwa mradi unakuza miundombinu ya kisasa kama mawasiliano ya mtandao, vituo vya usindikaji, mifumo ya umwagiliaji na viwanda vya kuongeza thamani, hatua itakayoiweka Tanzania katika nafasi ya uongozi wa kikanda katika teknolojia ya kilimo.
Akizungumzia uhalisia wa mradi, Prof. Mkumbo anesema umeandikishwa chini ya Sheria ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi, ambayo inalenga kuongeza ushindani, tija, ajira na mauzo ya nje.

Amebainisha kuwa mradi huo unaleta mapinduzi katika maeneo maalum ya kiuchumi kwa kuunganisha kilimo cha kisasa na viwanda ndani ya eneo la zaidi ya ekari 62,000.Kwa mujibu wa Waziri, manufaa ya mradi ni pamoja na ajira zaidi ya 300,000 ndani ya miaka 10, ushirikishwaji wa wakulima zaidi ya 10,000, uanzishaji wa zaidi ya viwanda 80, uhaulishaji wa teknolojia za kisasa, na uboreshaji wa huduma za kijamii kupitia programu za uwajibikaji kwa jamii (CSR).
Amesisitiza kuwa mradi huo unaendana na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, inayolenga uchumi shindani unaotumia teknolojia, uwekezaji katika rasilimali watu, uongezaji thamani wa mazao ya kilimo, mazingira rafiki kwa sekta binafsi na maendeleo endelevu.Prof. Mkumbo alieleza kuwa serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji, kurahisisha taratibu na kushirikiana na sekta binafsi ili kuhakikisha miradi mikubwa kama huu inatekelezwa kwa ufanisi na kwa maslahi ya wananchi.

“Kwa kukabidhi hati hii leo, tunafungua rasmi ukurasa mpya wa fursa, viwanda, ajira na ustawi wa kiuchumi kwa Kilwa na Tanzania,” alisema Prof. Mkumbo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TISEZA, Gilead Teri alisemaMwekezaji huyo hapewi ardhi ya bure bali bali anapewa ardhi na mkataba kutoka TISEZA ameongeza kuwa Ardhi yote ya Tanzania inamilikiwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa niaba ya watanzania wotePia amewaomba wadau wote wa Mamlaka ya Uwekezaji, Halmashari zote, Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa kuhakikisha kwamba tunamsaidia na kuunga mkono uwekezaji huo ili uweze kufanikiwaMkuu wa Wilaya ya Kilwa, Mohammed Nyundo, amesema wananchi wa mkoa wa Lindi wana utayari mkubwa wa kukipokea na kukitekeleza mradi huo, akibainisha kuwa ratiba ya utekelezaji ilipaswa kuendelea jana katika wilaya ya Kilwa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mavuji, Yusuph Mohammed, alisema kuwa ajira ni kilio kikubwa kwa wananchi wa eneo hilo na anaamini mradi huo utakuwa mwarobaini wa changamoto hiyo.

Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Liwiti, Samil Shamti,ameeleza dhamira ya wananchi kushirikiana kikamilifu kuhakikisha mradi huo unatekelezwa na kusimamiwa ipasavyo.Akizungumza kuhusu mradi huo, Mwekezaji Dior Feng alisema Serikali ya Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuvutia uwekezaji, si tu kwa kuwa wazi kwa biashara, bali pia kwa kuchukua hatua mahsusi za kuhimiza uwekezaji mkubwa na wenye tija.
Ameongeza kuwa kampuni ya Pan Tanzania itatumia teknolojia za kisasa zaidi za kilimo pamoja na mifumo ya usimamizi wa mashamba yenye akili, ikiwemo umwagiliaji wa kisasa katika zaidi ya ekari 50,000 ifikapo mwaka 2030, hatua itakayoiweka Tanzania kuwa miongoni mwa viongozi wa kikanda katika matumizi ya teknolojia ya kilimo na usindikaji.

More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina