Judith Ferdinand,Mwanza
Waziri wa Viwanda na Biashara, Profesa.Kitila Mkumbo amesema asilimia 90 ya mapato ya biashara zinazofanywa na wajasiriamali wanawake yanarudi kusaidia familia na kutatua changamoto za chakula,matibabu na elimu.
Pia mapato hayo ni fursa ya kuvunja umasikini na kuwapa wanawake nafasi ya kufanya biashara huku tafiti zikionesha mapato ya wanaume ni chini ya asilimia 50 na kuhoji zaidi ya asilimia 50 yanakwenda wapi.
Profesa .Mkumbo alitoa kauli hiyo jana wakati akifungua maonesho ya 21 ya wajasiriamali wadogo na wakati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki maarufu kama Nguvu Kazi/Jua Kali yanayofanyika Rock City Mall mkoani Mwanza,ambaye alikuwa mgeni rasmi wa maonesho hayo akimwakilisha Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.
Ambapo maonesho hayo yamebeba kauli mbiu ya ” Ukuzaji ubora na ubunifu ili kuinua ushindani wa ujasiriamali wadogowadogo wa Afrika Mashariki na ahueni baada ya UVIKO-19 yameanza Desemba 2 hadi 12 mwaka huu.
Amesema,asilimia 6O ya washiriki katika maonesho hayo ni wanawake hivyo mapato yao yataenda kusaidia katika familia zao katika masuala ya chakula,matibabu na elimu ya watoto hivyo mapato hayo ni fursa ya kuvunja mnyororo wa umasikini.
“Maonesho haya yana umuhimu mkubwa kwani nchi zote duniani ujasiriamali unachukua nafasi kubwa ,naomba nisahihishe hapa hakuna mfanyabiashara mdogo kuna biashara ndogo na biashara ya kati amesema Prof.
Mkumbo.
Kuhusu wajasiriamali Prof.Mkumbo amesema vijana ndio matajiri wakubwa watarajiwa ambao kwa upande wa Tanzania wamefanya utafiti wa viwanda na biashara uzalishaji bidhaa asilimia 98 unatokana na viwanda vidogo sana na vidogo.
Akizungumzia suala la kuwawezesha wajasiriamali wa Jumuiya ya Afrika Mashariki,Prof.Mkumbo amesema serikali zote za nchi hizo zimekubaliana kuwa na sera moja za kuendeleza wajasiriamali wadogo na wa kati.
Pia wataendelea kufanya kazi ya kuondoa vikwazo vinavyo kwamisha wafanyabiashara katika Jumuiya hiyo.
“Tuwaunge mkono viongozi wetu,ambao ambao wamepanga kuona mazingira ya kufanyia biashara yana kwenda kuboreshwa , wajasiriamali kuweni wabunifu ambao ubunifu huo pia tumeuona kwa wajasiriamali wetu katika maonesho haya,” amesema Prof.Mkumbo.
Aidha amesema,lengo la serikali ni kuwawezesha wafanyabiashara wadogo na wa kati ili wazalishe bidhaa za kutosheleza mahitaji ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
“Tumeona namba kubwa ya wanawake na vijana wamejitolea kuzalisha bidhaa za ubunifu, serikali itahakikisha inawekeza nguvu katika uwezeshaji wao ili kuhakikisha viwanda vyetu vinapata malighafi ya kutosha inayozalishwa na wazalishaji wadogo na wa kati,” amesema Prof.Mkumbo.
Mwenyekiti wa Shirikisho la Wajasiriamali wa Jumuiya ya aAfrika Mashariki Josephat Rweyemamu,amesema maonesho hayo yalianza mwaka 1999 yakiwa na washiriki 59 Sasa wameongezeka Hadi kufikia takribani wajasiriamali 1400 pia bidhaa zimeongezeka na zingine zimepata nembo za ubora.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel,amesema jumla ya wajasiriamali 1,304 wamethibitisha ushiriki kati ya hao 794 wametoka katika nchi za Kenya,Uganda,Sudan ya Kusini,Burundi,Rwanda na 510 kutoka mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar.
“Maonesho haya kwetu sisi kwa wanamwanza ni fursa ya kipekee ya kuandika historia ya Mkoa wetu wa Mwanza,yamesaidia kukua kwa pato la taifa na wajasiriamali,pia kupitia mzunguko wa fedha utasaidia Mkoa kuongeza pato,” na kuongeza kuwa
“Nindelee kutoa wito kwa wananchi wa Mwanza na mikoa jirani kujitokeza kwa wingi kujitokeza kutembelea mabanda na kununua bidhaa kwa kufanya hivyo tunainua uchumi wetu na kuendelea kutangaza bidhaa za wajasiriamali wa Jumuiya hii,”amesema Mhandisi Gabriel.
Mhandisi Gabriel amesema kuwa Mwanza ni eneo lenye ardhi nzuri na uchumi ,kuna maeneo mbalimbali ya uwekezaji na yakibiashara hivyo wafanyabiashara wajitokeze kuwekeza.
Aliongeza kuwa hakuna rushwa wala kuzungushana katika upatikanaji wa maeneo huku akitia wito kwa wananchi kujitokeze kwa wingi katika maonesho hayo ili kukuza uchumi na kuzitangaza bidhaa mbalimbali za Afrika Mashariki.
Awali Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu(Sera,Bunge,Kazi,Vijana,Ajira Walemavu),Jenista Mhagama amesema tatizo la ajira ni kwa wote hivyo maonesho hayo ni ufunguo wa ajira, kukuza uchumi pia ni nyenzo ya kubadilishana ujunzi ambao unaweza kutengeneza ajira nyingi nchini pamoja na kubadilishana elimu ya ujasiriamali na kudumisha umoja na mshikamano.
“Maonesho haya yanaendana sambamba na maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru na kuonesha thamani ya uwepo wetu,kutumia rasilimali tulizonazo,kutumia teknolojia na ujuzi kidogo lakini tukaboresha bidhaa,ambazo zinaweza kuingia kwenye masoko makubwa ya kimataifa,”amesema Mhagama
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Maendeleo ya Wajasiriamali nchini Kenya David Osiany,amesema anafarijika kuona akinamama na vijana wajasiriamali kwenye maonesho ya mwaka huu ambapo nchini Kenya sekta hiyo inachangia asilimia 83 ya
ajira.
Amesema maonesho ya wajasiriamali yanatoa fursa kuonesha dunia kuwa wananchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki si watu wa kununua bidhaa za nje ya nchi zao bali wanao ujuzi wa kutengeneza bidhaa zenye ubora.
More Stories
Walimu S/ Sekondari Ilala wafundwa juu ya maadili ya wanafunzi
Dkt. Samia afungua skuli ya sekondari Misufini, Bumbwini
Rais Mwinyi: Barabara Pemba zitajengwa kwa lami