March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Prof.Mkumbo atembelea mradi wa Kilombero Sugar akutana na Mwekezaji

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, amewasili katika mradi wa Kilombero Sugar Company Limited uliopo Ifakara, mkoani Morogoro Region kwa lengo la kuzungumza na mwekezaji pamoja na kukagua maendeleo ya upanuzi wa uzalishaji wa sukari katika kampuni hiyo.

Katika ziara hiyo, aliyoifanya leo Mkoani hapo, Waziri Mkumbo ameambatana na viongozi mbalimbali wa mkoa, wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Kilombero,Dunstan Kyoba, ambapo kwa pamoja wamepata fursa ya kupokea taarifa ya kina kuhusu hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa mradi huo kabla ya kufanya ukaguzi wa eneo la uzalishaji.

Ziara hiyo ni sehemu ya mwendelezo wa ziara ya kikazi ya Waziri Mkumbo mkoani Morogoro, inayolenga kufuatilia, kuhimiza na kuhakikisha utekelezaji wa miradi ya uwekezaji na maendeleo unafanyika kwa ufanisi na kwa kuzingatia malengo yaliyowekwa.

Mradi wa Kilombero Sugar ni miongoni mwa miradi mikubwa ya uzalishaji wa sukari nchini, ukiwa na mchango mkubwa katika kuongeza uzalishaji wa sukari ya ndani, kupunguza utegemezi wa uagizaji wa sukari kutoka nje ya nchi, kukuza ajira kwa wananchi wa Wilaya ya Kilombero na maeneo jirani, pamoja na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika Mkoa wa Morogoro.

Kupitia ziara hiyo, Serikali inalenga kuhakikisha uwekezaji unaendelea kwa kasi inayokusudiwa, huku manufaa ya mradi huo yakionekana moja kwa moja kwa wananchi na kuchangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi wa taifa.