Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
WAZIRI wa Elimu ,Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda amesema ,Serikali ipo katika hatua za mwisho za kuwapata wahusika wa wizi wa mitihani ambao walisababisha baadhi ya shule kufungiwa kutokana na vitendo hivyo.
Profesa Mkenda ameyasema hayo jijini Dodoma kutokana na hoja iliyoibuliwa na wamiliki wa shule binafsi baada ya kukutana nao ambapo waliomba kuvifungulia vituo vya mitihani vilivyosimamishwa na badala yake serikali iwachukulie hatua wahusika badala ya kuzifungia shule jambo ambalo linazorotesha elimu hapa nchini.
Kwa mujibu wa Waziri huyo ,wahusika hao watafahamika kwa majina yao na baada ya hapo Serikali kupitia Wizara yake itatangaza maamuzi juu ya vituo hivyo vya mitihani ambavyo vilisababisha shule kufungiwa.
“Kuna shule zimefungwa kuwa vituo vya mitihani lakini hatua tuliyofikia kwa sasa ni kuyapata majina ya waliohusika katika wizi wa mitihani hiyo …,ni lazima wajulikane na wachukuliwe hatua kali za kisheria na hapa nasema hatapona hata mmoja atakayethibitika kuwa ameshiriki ,
“Hii nasema kuanzia msimamizi wa mitihani mpaka Yule mlinzi aliyekuwa analinda mitihani naye lazima achunguzwe ili kumata muhusika halisi.”amesema Profesa Mkenda
Ametumia nafasi hiyo kuwataka wamiliki hao wa shule binafsi kusimamia malezi katika shule zao ili kuendelea kutoa kizazi chenya maadili na kuondokana na matukio yanayoripotiwa kuwa kuna baadhi ya shule zinafundisha watoto maadili yasiyofaa.
Hata hivyo amesema serikali inatambua na kuthamini mchango unaotolewa na sekta binafsi katika kuinua na kuendeleza sekta hiyo hapa nchini.
“Niwatoe wasiwasi kuwa serikali inatambua na inathamini mchango wenu katika maendeleo ya sekta ya elimu hapa nchini hivyo msifikirie kwamba tumewaacha nyuma ,hapana,tunawahitaji sana muendelee kuwekeza katika elimu yetu.”
Kwa upande wa wamiliki wa shule binafsi wameomba kuondolewa kwa gharama za mitihani kwa wanafunzi wanaosoma shule binafsi kwani hawana tofauti na wanafunzi wanaosoma shule za serikali ambao wamefutiwa gharama za mitihani.
Aidha wamemuomba Waziri Mkenda kuongeza bajeti ijayo katika idara ya udhibiti ubora wa shule wakati wanakwenda kukagua shule kwani imekuwa ikiwaumiza kuwalipa ili waende kukaguliwa.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakani
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best