March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Prof.Mkenda:Tushirikiane kutekeleza mageuzi ya Elimu kwa manufaa ya Taifa

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf Mkenda amesema kuwa mageuzi ya elimu ni muhimu sana kwa taifa, hivyo tunalazimika kuyatekeleza ili kuandaa vijana wetu kukabiliana na changamoto za kiuchumi na kutumia fursa za teknolojia kuleta maendeleo nyanja mbalimbali Nchini.

Prof. Mkenda amesema hayo Novemba 27, 2025 jijini Dodoma akifunga Mkutano wa Umoja wa Walimu Wakuu wa Shule za Msingi Tanzania Bara (TAPSHA), akisisitiza kuwa katika moyo wa mageuzi ya elimu, ni muhimu kuwandaa vijana wetu ili waendane na mabadiliko ya teknolojia na mazingira ya kidigitali.

“Ili kuwaandaa vijana kwa soko la ajira na kukabiliana na changamoto za utandawazi, tushirikiane kutekeleza mageuzi na tuwekeze kwenye sayansi na teknolojia” amesema Prof. Mkenda.

Waziri Mkenda amesema kuwa, katika kutekeleza Sera ya Elimu ya Mwaka 2014, Toleo la 2023, pamoja na mambo mengine Wizara inafanya maandalizi kwa ajili ya kuwapokea wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na elimu ya sekondari hatua ya chini mwaka 2028.

Aidha amesema kuwa Serikali inatambua mchango wa TAPSHA katika maendeleo ya elimu, hivyo amesisitiza chombo hicho kulinda familia ya walimu. Aidha amewapongeza walimu wote Nchini kwa kazi nzuri wanaofanya.

Akimwakilisha Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI Ndug. Adolf Ndunguru, Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Elimu Dkt. Emmanuel Shindika, amesema kuwa Mkutano huo umekuwa jukwaa muhimu la kutathmini masuala mbalimbali ya kielimu na kuweka mikakati madhubuti ya utekelezaji wa Mtaala Ulioboreshwa.

Ameongeza kuwa majadiliano yaliyofanyika yameongeza uelewa na kuimarisha ushirikiano katika kuboresha elimu ya msingi nchini.

Naye, Mwenyekiti wa Umoja wa Walimu Wakuu wa Shule za Msingi nchini Tanzania (TAPSHA) Bi. Rehema Ramole ameipongeza Serikali kwa juhudi mbalimbali katika kutekeleza mageuzi ya elimu ikiwemo pamoja na kueendelea kuboresha maslahi ya Walimu, kwani wanaendelea kupandishwa madaraja.

Mkutano huo umeongozwa na kaulimbiu inayosema: Mtaala Ulioboreshwa kwa Elimu Bora: Ujuzi na Ubunifu kwa Maendeleo Endelevu ya Taifa