March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Prof.Mkenda awasitiza wanafunzi wanaokwenda kusoma nje ya nchi kupitia programu ya Samia Scholarship 

Na Penina Malundo,Timesmajira 

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amewasisitiza wanafunzi wanaokwenda kusoma nje ya nchi kupitia programu ya Samia Scholarship Extended DS/AI, iliyoandaliwa na Wizara  hiyo kuhakikisha wanafata maadili, ili wakirejee walete mchango chanya kwa maendeleo ya Taifa.

Pia amewataka Wanafunzi hao kuwa mabalozi wa nchi huku wakihakikisha  wanajifunza kwa bidii, wanaheshimu sheria za nchi wanazoenda.

Akizungumza leo Januari 30,2026 katika hafla ya kuwaaga wanafunzi 16 kati ya 50 wa programu hiyo  ya Samia Scholarship  amesema vijana hao wanapaswa kutumia 

maarifa watakayopewa kwa lengo la kuleta suluhisho la changamoto za maendeleo hapa nchini.

Amesema wanafunzi hao wanapaswa kuleta   mabadiliko chanya kulingana na dira ya maendeleo ya 2050.”Programu ya Samia Scholarship ni matokeo ya dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuwekeza kwenye sayansi, teknolojia na rasilimali watu, hususan kwa vijana, ili kuandaa kizazi chenye uwezo wa kushindana kimataifa,”amesema 

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Prof.Nombo, amesema serikali itaendelea kuwekeza kwenye programu za kimkakati kama Samia Scholarship Extended DS/AI, kwa kuwa zinasaidia kujenga msingi wa maendeleo ya muda mrefu kupitia sayansi na teknolojia.

“Uwepo wa taasisi kama Nelson Mandela Institute of Science and Technology umechangia kwa kiasi kikubwa kuwajengea wanafunzi ujuzi wa kitaaluma na maisha, ikiwemo financial management na stadi za karne ya 21,”amesema 

Profesa Nombo amewataka wanafunzi kuzingatia kuwa wao ni mfano kwa vijana wengine waliopo mashuleni, na kwamba nafasi hizo zinapatikana kwa misingi ya ushindani wa kitaaluma (merit-based), hivyo wanafunzi wajitahidi katika masomo hasa ya sayansi na TEHAMA.

Mmoja wa wanufaika wa programu hiyo, Malaika Florence, amesema mafunzo ya awali waliyopata kupitia boot camp yamewajengea uwezo mkubwa katika masuala ya usimamizi wa fedha, matumizi ya teknolojia na kujiamini katika mazingira ya kimataifa.

Amesema awali wengi wao walikuwa hawana ujuzi wa msingi wa matumizi ya kompyuta, lakini sasa wamejifunza stadi za kisasa ikiwemo uandishi wa codes, matumizi ya lugha mbalimbali za programu kama Python na Java, pamoja na mbinu za kujifunza kwa kujitegemea.

Naye Aswile Simon, ambaye amepata nafasi ya kwenda kusoma katika Chuo Kikuu cha Johannesburg nchini Afrika Kusini, amemshukuru Rais Samia kwa kuanzisha programu hiyo, akisema pasipo uongozi wake vijana wengi wasingeweza kupata fursa adimu kama hiyo.

Aswile amesema wanafunzi wanatambua imani kubwa waliyopewa na Taifa, hivyo wana wajibu wa kusoma kwa bidii na kurejea nchini wakiwa na maarifa yatakayosaidia kuendeleza sekta ya teknolojia, uchumi wa kidijitali na ubunifu.