Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amesema hatosita kutengua uteuzi wa wajumbe wa Bodi Mpya ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) iwapo itashindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo ikiwemo kuisimamia shirika hilo kihuduma na kibiashara.
Bodi ya ATCL inaongozwa na Mwenyekiti Profesa Neema Mori na wajumbe sita (6) waliochaguliwa kusaidia kuiongoza Shirika hilo kwa kipindi cha miaka mitatu
Akizungumza katika uzinduzi wa Bodi hiyo leo jijini Dar es salaam, Prof Mbarawa amewahasa wajumbe hao wa bodi kufanya kazi kwa ufasaha ili shirika hilo lizidi kwenda mbele;
“Bodi hii ina kazi kubwa sana ya kulisaidia Shirika hili liweze kuenda mbele hivyo kafanyeni kazi msiende kuwa watendaji”, amesisitiza Prof. Mbarawa.
Aidha, amezitaja sababu za Bodi nyingi kushindwa kusimamia taasisi na mashirika mengi ikiwemo Mwenyekiti kushindwa kusimama katika nafasi yake, kupewa offer mbalimbali na watendaji zinazowafanya kushindwa kushauri na kukataa jambo.
“Shirika hili lina manunuzi mengi hivyo msipokuwa makini na kushindwa kufanya maamuzi ya kulisaidia shirika hili mtaingizwa kwenye matatizo makubwa”, amesema Prof. Mbarawa.
Kuhusu madeni ya zamani ya Shirika hilo, Waziri Mbarawa ameahidi Serikali inaendelea kulishughulikia suala hilo ili kuisaidia Shirika hilo liweze kuleta matokeo chanya na kuingiza pato kubwa kwa Taifa.
“Serikali inahitaji kuona matokeo ya ndege 11 zilizonunuliwa zinaleta faida na Shirika kujiendesha kibiashara”, amefafanua Prof. Mbarawa.
Katika hatua nyingine, Waziri Prof. Mbarawa amesema kuwa hadi kufikia mwaka 2023 Shirika hilo litakuwa na jumla ya ndege 17 ambapo tayari ndege tano ziko katika hatua za manunuzi.
Kwa upande wake Mwenyekiti mpya wa Bodi hiyo Prof. Neema Mori, amemuahidi Waziri Mbarawa kushirikiana na wajumbe wengine kumsadia katika ufanisi shirika hilo ili liweze kutoa huduma bora na kuwa shirika la mfano.
Awali akitoa taarifa ya Shirika hilo, Mkurugenzi Mkuu wa ATCL, Eng. Ladislaus Matindi, amesema Shirika hilo limejiapnga vyema kufanya kazi kiufanisi na tija na inaendelea na kupanua safari zake za ndani na nje ya nchi.
“Hivi karibuni tumeanza za nje za Nairobi – Kenya, Lugumbashi – DRC, Ndola – Zambia na kwa safari za ndani tumerejesha safari za Mtwara na Songea pamoja na kuanzisha safari ya Dodoma na Mwanza”, amefafanua Eng. Matindi.
More Stories
TASHICO,yatoa ufafanuzi Mv.Serengeti kutitia upande mmoja
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua