December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Prof.Mbarawa ataja faida uboreshaji wa bandari

Na Judith Ferdinand,Timesmajira Online Mwanza

Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi imeeleza faida zinazotarajiwa kupatikana katika mkataba baina ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na serikali ya Dubai kuhusu ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kwa ajili ya uendelezaji na uboreshaji wa utendaji kazi wa bandari nchini.

Akizungumza Juni 14 mwaka huu na waandishi wa habari mkoani Mwanza, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa,juu ya maelezo ya awali kuhusu mapendekezo ya kuridhia mkataba baina ya serikali ya Tanzania na Dubai kuhusu ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kwa ajili ya uendelezaji na uboreshaji wa utendaji kazi wa bandari nchini.

Amesema kwa mujibu wa ibara ya 2 ya makubaliano, lengo lake ni kuweka msingi wa ushirikiano baina ya Serikali mbili kwa maeneo mahsusi yaliyoainishwa ndani ya makubaliano husika (Rejea Appendix 1 ya makubaliano) ambayo utekelezaji wake utafanyika kupitia mikataba mahsusi baina ya taasisi zilizoainishwa katika mkataba wa IGA kama taasisi tekelezi ambazo ni TPA na DP World.

Hivyo,makubaliano hayo hayana masharti yanayoifunga serikali kuhusu maeneo ya ushirikiano yaliyoanishwa pasipo uwepo wa mikataba mahsusi ya utekelezaji wa miradi itayojadiliwa na kukubaliwa na pande mbili.Prof.

Mbarawa amebainisha baadhi ya manufaa yatakayopatikana katika ushirikiano huo ni pamoja na kupunguza muda wa meli kukaa nangani kutoka siku 5 kwa sasa mpaka masaa 24.

“Hii itapunguza gharama za utumiaji wa bandari yetu,matokeo yake itaongeza idadi ya meli zitazokuja bandari ya Dar-es-Salaam kutoka meli 1,569 zilizohudumiwa mwaka 2021/22 mpaka kufikia takriban meli 2,950 ifikapo mwaka 2032/33,”ameeleza Prof.Mbarawa.

Kupunguza muda wa ushushaji wa makontena kutoka siku 4.5 mpaka siku 2,kupunguza muda wa uondoshaji mizigo kutoka masaa 12 mpaka saa 1 kutokana na uboreshaji wa mifumo ya TEHAMA.

Pia kupunguza gharama ya usafirishaji wa mizigo kutoka nchi za nje kwenda nchi za Jirani, kwa mfano kutoka dola (US$)12,000 mpaka kati ya US$6,000 na US$7,000 kwa kasha linalokwenda nchi ya Malawi, Zambia au DRC,hii italeta watumiaji wengi kwenye bandari ya Dar-es- Salaam.

Huku faida zingine zinazotarajiwa ni pamoja na kuongezeka kwa shehena inayohudumiwa kutoka tani milioni 18.41 za mwaka 2021/22 hadi kufikia tani milioni 47.57 mwaka 2032/33, sawa na ongezeko la asilimia 158.

Pamoja na kuongezeka kwa mapato ya serikali yatokanayo na kodi ya forodha inayokusanywa katika shehena inayopitishwa bandarini kutoka trilioni 7.76 za mwaka 2021/22 hadi trilioni 26.7 za mwaka 2032/33, sawa na ongezeko la asilimia 244.

Aidha kuongezeka kwa ajira zinazotokana na shughuli za bandari kutoka 28,990 mwaka 2021/22 hadi ajira 71,907 ifikapo mwaka 2032/33, sawa na ongezeko la asilimia 148.

Vilevile kufanyika kwa maboresho ya maeneo ya kuhudumia shehena ya makasha na kuweka mitambo yenye teknolojia ya kisasa,kuendeleza eneo la kuhifadhia mizigo la bandari kavu kwa kuweka miundombinu ya kisasa ya kuhudumia aina zote za shehena.

Kadhalika faida nyingine ni kuendeleza magati ya kuhudumia majahazi na abiria ikiwa ni pamoja na kushawishi uingiaji wa meli kubwa za kitalii zitakazo ongeza idadi ya watalii nchini na kuongeza pato la taifa na kusimika mifumo ya kisasa ya TEHAMA kwa ajili ya shughuli za bandari na kuwaunganisha wadau wake.

Hata hivyo faida zingine zinazotarajiwa ni mafunzo ya kuwajengea uwezo wafanyakazi wa TPA katika bandari zote (knowledge and skills transfer),uanzishwaji wa maeneo maalum ya kiuchumi na viwanda.

Sanjari na hayo faida nyingine ni kuchochea ukuaji wa sekta zingine za kiuchumi zikiwemo sekta ya kilimo,mifugo na uvuvi,kuchagiza shughuli za viwanda na biashara,kuchagiza ukuaji wa sekta ndogo za usafirishaji kwa njia ya reli (SGR, TAZARA na MGR) na barabara,watanzania kunufaika na teknolojia na ujuzi wa uendeshaji wa bandari kisasa na kujenga mahusiano ya kidiplomasia.

Mbali na hayo Profesa Mbarawa ameeleza kuwa msisitizo wa serikali ni kuhakikisha maeneo yote ya nchi yanabaki chini ya umiliki wa Serikali.

Prof.Mbarawa amewatoa hofu watanzania kwa kueleza kuwa makubaliano haya yameweka vifungu vyote muhimu ambavyo vinalinda maslahi ya nchi yetu ikiwemo ajira za watanzania,ardhi ya watanzania, ukomo wa mkataba husika, masuala ya ulinzi na usalama na masuala yote mengine muhimu yenye maslahi na nchi.

Aidha ameeleza kuwa pamoja na vipengele hivyo kama nchi imeweka bayana kuwa wakati wa kutekeleza mikataba ya miradi ambayo itaingiwa yatazingatia masuala muhimu ikiwemo mikataba itakayoandaliwa itaweka bayana kipindi cha utekelezaji wake na ukomo.

Pia muda wa marejeo ni mwaka 1 hadi miaka 5,viasharia muhimu vya ufanisi wa kiutendaji (key performance indicators) vitaanishwa,uandaaji wa mikataba ya miradi utafanywa chini ya usimamizi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuzingatia maslahi mapana ya Taifa.

Mikataba itakayoandaliwa italinda ajira za wafanyakazi wazawa na kuwajengea uwezo wafanyakazi mifumo yote ya TEHAMA itakayosimikwa na DP World inasomana na mifumo ya Serikali.

Huku taasisi mahsusi za serikali zitaendelea na utekelezaji wa majukumu yake katika maeneo ya bandari na kuhakikisha Mwekezaji anachukua hatua stahiki za masuala ya utafutaji wa masoko ya bandari ya Dar-es-Salaam.

Akijibu maswali ya waandishi wa habari ambao waliitaji ufafanuzi juu ya suala la kuwa mkataba wa ushirikiano huo kati ya Tanzania na Dubai ni wa miaka 100,Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Uchukuzi) Dkt.Ally Possi ameeleza kuwa siyo kweli mkataba huo hautakuwa wa miaka mia kama inavyosemekana.

Amefafanua kuwa haya ni makubaliano ya awali ili kutengeneza mikataba ya utekelezaji na hivyo kitaalamu huwezi kuweka ukomo hapa lakini ibara ya 23 kifungu cha kwanza inaeleza kabisa kuwa ukomo wa mkataba huu utaendana na kusitishwa kwa programu ya utekelezaji.

“Hamna miaka 100, ila ukomo upo na utakuwepo katika mikataba ya majadilioano na makubaliano tusomee kifungu namba 23 moja,wamepokea maoni ya wananchi na wameona hamna kuandika mambo mengi ni ukomo tu miaka kadhaa kwa lugha inayoeleweka na mkataba unakuwa unaeleweka zaidi,”.

Pia ameeleza kuwa kama Wizara itaendelea kutoa elimu na kuelimisha ili watu waelewe sheria za uwekezaji na jinsi gani biashara na bandari zinafanya kazi zake maana ukiyaekewa mambo haya mawili vizuri ndio utaweza kuelewa haya makubaliano ya awali ya mkataba wa ushirikiano.