Na Mwandishi Wetu,Timesmajira
Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Prof. Haruni Mapesa amewataka Wanafunzi wa Mwaka wa Kwanza wa Chuo hicho kuhakikisha wanafuata Kanuni, Taratibu na Sheria za Chuo kama zilivyo na zinavyoelekezwa.
Prof. Mapesa ameyasema hayo leo wakati akizungumza na wanafunzi wa mwaka wa kwanza 2025/2026 kwenye kikao kilicholenga kuwakaribisha rasmi wanafunzi hao ambapo pamoja na mambo mengine ameelezea historia ya Chuo, Mipango na Maendeleo ya Taasisi kwa Ujumla
Amewataka Wanafunzi kuwa na nidhamu na kufuata sheria na kanuni za ufanyaji wa mitihani, nidhamu katika Mavazi, kuheshimiana baina yao, lakini pia kuwa na nidhamu kwa Wafanyakazi wanaohudumu katika Taasisi hiyo.
Pia Prof. Mapesa amewasihi sana Wanafunzi wa Chuo hicho kujiepusha na vitendo viovu ikiwemo kujihusisha na makundi yasiyofaa,
“Jiepusheni na matumizi ya madawa ya kulevya, hakikisheni mnaziwasilisha changamoto zinazowakabili sehemu husika ili zipatiwe ufumbuzi kwa wakati badala ya kufanya vurugu.,” amesema Prof Mapesa na kuongeza
“ Jukumu lililowaleta Chuoni ni kusoma kwa bidii na kuhakikisha mnafaulu vyema mitihani kwani ndiyo kipimo cha uelewa wa kile ambacho mtakuwa mmefundishwa, lengo likiwa ni kufikia malengo na matarajio mliyojiwekea katika kutimiza ndoto zenu mlizojiwekea katika maisha.”amesisitiza Prof. Mapesa.

Aidha amewataka wanafunzi kuzingatia na kuhakikisha wanakuwa na vitambulisho muda wote wanapokuwa Chuoni, kuhakikisha wanakamilisha usajili, kutunza mazingira pamoja na miundombinu mbalimbal ya chuo
Kwa upande wake Rais wa Serikali ya Wanafunzi Magashi Magina amewataka Wanafunzi wenzake kuzingatia yale yote yaliyoelekezwa na Mkuu wa Taasisi, ili kujiepusha na usumbufu usio wa lazima.
Kupitia kikao hicho, Wanafunzi walipata fursa ya kuuliza maswali mbalimbali ambayo yalipatiwa majibu na viongozi waliokuwepo
Kikao hicho kimehudhuriwa na Menejimenti ya Chuo, Serikali ya Wanafunzi, Wafanyakazi Waendeshaji na Wanataaluma.

More Stories
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina
Kihongosi: Msigombane kwa itikadi za vyama